Habari kutoka 16 Juni 2009
Irani: Maandamano na Ukandamizaji
Mamia ya maelfu ya Wairani mjini Tehran na katika miji mingine kadhaa wameandamana kumuunga mkono mgombea urais Mir Husein Mousavi huku wakiipuuza amri ya serikali inayokataza maandamano. Japokuwa huduma za Twita, FaceBook pamoja na YouTube zimezuiliwa kwa kuzimwa nchini Iran, Wairani wengi wamekuwa wakitumia tovuti-vivuli ili kuvizunguka vichujio vilivyowekwa na wanaripoti habari kadiri zinavyotokea. Utawala wa Irani pia umezuia huduma za jumbe za maandishi kwa kutumia simu za mkononi (SMS), kadhalika utawala huo unachuja tovuti kadhaa zinazoakisi maoni ya wanamageuzi.