· Oktoba, 2012

Habari kutoka Muhtasari wa Habari kutoka Oktoba, 2012

Madagascar: Global Voices katika Kimalagasi Yapiga Hatua Kubwa

Mradi wa Lingua wa Global Voices katika lugha ya Ki-Malagasi

Mradi wa Lingua wa Global Voices katika lugha ya ki-Malagasi umechapisha mtandaoni posti yake ya 5,000. Mradi huo ulianza mwezi Septemba 12, 2007 ukiwa kati ya miradi ya mwanzo kabisa ya  Mradi mkubwa wa Lugha za Kiafrika. Kwa sasa mradi huo unaendeshwa na watafsiri wa ki-Malagasi wapatao 16 miongoni mwao akiwamo mmoja wa watafsiri wadogo kabisa wa Global Voices , mwenye umri wa miaka 16 aitwaye Radifera Felana Candy.

DRC Kongo: Misuguano Kati ya Kinshasa na Paris Mkutano Unapoanza

Le Potentiel anaandika kwamba [fr] tathmini ya Uvunjaji wa Haki za Binadamu nchini DRC Kongo iliyofanywa na Rais wa Ufaransa Hollande haikuchukuliwa kijuu juu na serikali ya Kongo wakati ambapo Mkutano wa nchi zizungumzazo Kifaransa ndio kwanza umeanza mjini Kinshasa, DRC. SErikali hizi mbili zinaonekana kutofautiana sana kuhusu mambo kama kifo cha mtetezi wa Haki za Binadamu Ndg Chebeya, tume ya taifa ya uchaguzi na uhitaji wa kamati itakayosimamia masuala ya haki za binadamu.

Je, Una Swali Lolote kwa Jimmy Carter?

Rais wa zamani wa Marekani Jimmy Carter anapokea maswali kupitia mitandao ya kijamii ya Facebook na Twita (#CarterQA) kama sehemu ya kuadhimisha miaka 30 ya Kituo cha Carter (Carter Center) kinachojishughulisha na “kupigania masuala ya amani na kupambana na magonjwa duniani kote”. Rais Carter atakuwa anayajibu maswali hayo kwa njia ya video tarehe 19 Oktoba, 2012.

Trinidad na Tobago: Ufisadi na Utawala wa Sheria

Hivi karibuni, masuala ya utawala wa sheria yamekuwa yamekuwa yakitawala serikali iliyoko madarakani. Kwa kuwa na kipengere cha 34 ambacho hakifahamiki sana miongoni mwa wananchi, hali ya mambo imebadilika na kuwa utawala wa kiimla, na […] tunaweza kuona ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka yamebadilisha kabisa tabia za wale tuliowaona kama nguzo na mifano ya kuigwa katika jamii yetu.

Jumbie's Watch anaandika kuhusu utawala na kuheshimiwa kwa sheria katika nchi ya Trinidad & Tobago.

Ghana: Vikwazo Vinavyowakabili Wanawake Kimaendeleo

Betty Mould Iddrisu, Jaji na Waziri wa Sheria wa Ghana, anaandika [fr] kwenye blogu ya pambazuka.org:

Kufikia ngazi za juu kabisa za utawala si rahisi, na hata unapopanda mpaka juu kabisa, bado unajikuta unakabiliwa na hisia za watu zenye uadui na watu wanakuwa na mashaka na uwezo wako, kwa sababu tu wewe ni mwanamke. Mwanamke akikamata madaraka ya juu humbidi kufanya kazi kwa bidii zidi kuliko mwanaume ili kuthibitisha uwezo wake, lakini bado hata akifanya hivyo anakumbana na uadui pamoja na mfumo unaomwona kuwa duni, iwe katika majukumu yake kama meneja na kiongozi, na hata katika mazingira yoyote ya kazi ambayo yanatawaliwa kwa kiasi kikubwa na wanaume.

China: Hatua za Kubana Uhuru wa Habari Majimboni

Jing Gao kutoka blogu ya Tofu anaeleza namna serikali ya Fuji ilivyo na mikakati michafu dhidi ya Yunnan na jinsi inavyochukua hatua za kuzuia uchapishaji wa habari zinazoweka wazi kashfa za ufisadi zinazomkabili afisa mmoja wa serikali.

Côte d'Ivoire: Wafanyakazi wa Afya Wagoma baada Miezi Minne Bila Mshahara

S.B anatoa maoni juu ya kuanza kwa mgomo usio na ukomo unaoratibiwa na wafanyakazi wa taasisi za afya mjini Abidjan. Katika mtandao wa Connection Ivorienne, anabainisha [fr] kwamba:

Kufuatia mabadiliko ya utolewaji wa huduma za afya ambazo zilitolewa bure kabisa baada tu ya kumalizika kwa mgogoro wa baada ya uchaguzi, sera iliyoanzishwa na serikali ya Côte d'Ivoire, ambayo sasa imeelekeza baadhi ya huduma tu ndizo zitakuwa bure, wafanyakazi wa taasisi kadhaa za afya hawajapata mishahara yao kwa wakati. Kibaya zaidi ni kwamba wakubwa wao hawakupata fungu lolote kwa ajili hiyo kwa zaidi ya miezi kumi na sita.

Tunisia: Mgomo Waanza jijini Thala

Kupitia mtandao wa twita, Tounsia Hourra (m-Tunisia huru) anasema [ar] kuna mgomo mkubwa umeanza jijini Thala, kwenye jimbo la Kasserine, leo [Oktoba 8, 2012]. Mgomo huo umekuja kama hatua ya kupinga kukua kwa kasi kwa ukosefu wa ajira na kuzorota kwa maendeleo ya jiji hilo.


@tounisiahourra
: اضراب عام في تالة ( ولاية القصرين ) اليوم احتجاجا على ارتفاع معدلات البطالة واهمال صيانة المدينة

@tounisiahourra: Mgomo mkubwa jijini Thala (jimbo la Kasserine) leo kupinga kuongezeka kwa ukosefu wa ajira na kuzorota kwa maendeleo ya jiji hilo.