Afya Duniani: Siku ya Vyoo Duniani Yatoa Harufu


Ingawa inaweza kusikika kama vile masihara, Siku ya Vyoo Duniani inatilia maanani kwenye suala ambalo si la mzaha linalowakwanza karibu nusu ya watu wote duniani – ukosefu wa vyoo na mfumo wa usafi.

Watu wanaweza kuwa wanaona aibu kuongea wazi kuhusu hili suala, lakini kila mmoja hujisaidia, kwenye choo au la. Siku ya Vyoo Duniani inasaidia watu kusherehekea umuhimu wa usafi na kuwaelimisha watu bilioni 2.5 ambao hawana vyoo na mfumo wa usafi wenye uhakika. Video hii iliyotengenezwa na asasi isiyo ya kibiashara WaterAid inaonyesha starehe ya kuwa na choo.

Kusherehekea kopo lako kunaweza kuonekana kama ujinga, lakini kutokuwa na kopo siyo tu kunaweza kukusababishia aibu, kukosa heshima na masuala mengine ya kiusalama, bali pia kunaweza kukusababishia magonjwa yanayoweza kuzuilika na hata kifo. Pale watu wanapokosa vyoo, wanalazimika kujisaidia mitaani kweupe, kwenye viwanja au vichochoroni. Matokeo? Uchafuzi wa maji ya kunywa na vyanzo vya chakula, jambo ambalo linapelekea hatari nyingi za kiafya. Ukosefu wa mfumo wa usafi ndiyo sababu kubwa ya maambukizi na huua watu milioni 1.8, hasa watoto, kila mwaka. Hata nchi zenye vyoo vya kutosha huwa zinakabiliana na matatizo yanayotokana na vyoo vichafu vya umma mpaka utupaji majitaka unaoharibu njia za maji.

Vanilla, anayeblogu kwenye Let's Look At It This Way kutokea Singapore, anasema kuwa watu wanapaswa kutilia maanani vyoo:

“ Ninajua kwamba hii ni mada chafu kwa watu wengi. Ni bahati mbaya kwamba hii mada bado ni ‘mwiko’ kuiongelea wazi na watu wengi hawana uelewa kuhusu ukubwa wa tatizo. Ninashindwa kuelewa ni kwa jinsi gain hii inaweza kuwa mada isiyo na maana wakati, kwa wastani, huwa tunakwenda chooni mara 2500 kwa mwaka, au mara 6-8 kwa siku. Wakati wa maisha yetu, hutumia muda wa miaka 3 vyooni.”

Chini ya maandalizi ya asasi isiyo ya kibiashara The World Toilet Organisation, Siku ya Vyoo Duniani inasherehekewa dunia nzima kwa matukio mbalimbali. Ili kuuelimisha umma zaidi, wiki hii WaterAid ilitangaza uzinduzi wa zana mpya ya Kutafutia Vyoo nchini Uingereza ya simu za mkononi za iPhone. Zana hiyo ya bure inawasaidia Waingereza kutafuta choo cha umma kilicho karibu zaidi wakati pia inawakumbusha jinsi walivyo na bahati ya kuwa na vyoo safi na salama. Tukio kubwa zaidi leo, linaloitwa Mchuchumao Mkubwa, linawataka watu wasimame na wachuchumae kwa dakika moja katika sehemu za umma ili kuongeza utambuzi. Picha hizi zinaonyesha watu waliochuchumaa dunia nzima, pamoja na hii ya watoto wa chekechea huko Singapore:

Blogu inayotokea Brunei, the world according to panyaluru …, pia inaonyesha kuridhika na vyoo kwa kuliweka suala hili kwenye muktadha sawia:

“Fikiria ikiwa tunatembea mbele ya mlolongo wa maduka kule Kiulap au Gadong. Mara tu tumbo linaunguruma kama vile ambavyo haujawahi kusikia. Halisimami kukupa mapumziko. Linaunguruma na kuunguruma. Ngurumo. Taa ni ya manjano tayari kubadilika kuwa ya kijani. Lakini hakuna vyoo unavyoviona. Hakuna hata choo kimoja cha umma kwenye mlolongo wa maduka… ongezea pia kuwa hakuna maji, karatasi ya chooni, hakuna chochote! Hiyo inaweza kuwa siku mbaya zaidi katika maisha yako, jinamizi baya, au jinamizi baya zaidi ya yale yaliyowakuta watoto kwenye filamu za Elm Street. Katika siku hii, hebu na tuvienzi vyoo.”

Ukiachilia mbali upande makini wa suala hili, watu wengi wametumia mzaha kuadhimisha siku ya Vyoo Duniani. Huko Uingereza blogu ya London City Drains imeweka chemsha bongo ya vyoo yenye maswali 10, wakati katika video hii mwalimu wa sekondari Matt Cheplic anaimba kuhusu siku hii.

Baadhi ya wanablogu wanasema kuwa vyoo pekee vinaweza visiwe jibu. Sandhya, anayeblogu kwenye Maradhi Manni nchini India, anasema wanaume wengi hawatumii vyoo vilivyopo:

Kwenye mji kama Chennai, ambako hali ya hewa ni ya joto kwa karibu miezi 10 ya mwaka, huwaona wanaume wanakojoakando ya barabara kila wakati. Wkati wanawake wanaweza kujidhibiti na kwenda nyumbani kujisaidia, kwa nini wanaume hawawezi kufanya hivyo, sijui kwa nini. Kwa hiyo, kwanza watu wote wanabidi wapigwe faini kali kwa kufanya kosa hili (naam, ni kosa) pale pale wanapokamatwa. Nimewahi kuwaona wakifanya hivyo kwenye ukuta wa vyoo vya umma! Kule Srinagam, nimewahi kuwaona wakikojoa kwenye ukutra wa boma la hekalu pamoja na kuwa kila mtaa unaolizunguka hekalu una vyoo, ambavyo vilikuwa visafi, lakini vya kulipia!”

Wakati ukosefu wa mfumo wa usafi unaathiri kila mtu, miiko inayozunguka suala la vyoo inawaathiri vikubwa wanawake zaidi ya wengine. Katika baadhi ya nchi, staha huwalazimisha wanawake kufanya shughuli zao kwenye makonde kabla ya jua kuchomoza au kujizuia mpaka mpaka baada ya jua kuzama, jambo ambalo linasababisha madhara ya kiusalama na kiafya. Joanne Sprague, anayeblogu kwenye Overturning Boulders nchini India, anabaini kuwa wanawake hawapo kwenye mzunguko wa kwenda haja asubuhi mijini Chennai, wakati huko Ethiopia blogu ya AN ADVENTURE IN ADDIS inabaini hali kama hiyo pia:

“Nimekuwa nikisikia mara nyingi juu ya ukosefu wa vyoo kwa wanawake au ukosefu wa vyoo kwa ujumla; kwamba wasichana wa rika la kuwa wali huko mashambani huamka saa 10 za alfajiri kwenda nje kwenye giza kufanya shughuli zao ili wasitaniwe na wavulana shuleni au huacha kwenda shule kabisa. Wanaume hukojoa kila mahali, sigara mkononi na kuna kuna dhana kuwa wanawake hawapaswi kufanya hivyo, kama wanafikiriwa hata kidogo… ninataka kuona bango kubwa kwa lugha ya Ki-Amhara linalosema “wasichana nendeni pia’ lenye picha ya mwanasesere anayevutia wa kike aliyeketi chooni.”

Kusherehekea Siku ya Vyoo Duniani, mwanablogu Jonathan Stray, anawachukua wasomaji kwenda ziara ya kimataifa ya vyoo ambavyo ameshawahi kuvizuru, kuanzia Thailand na Uingereza mpaka Afrika Magharibi na Oman, na anahitimisha:

“Sisi watu wa Magharibi na vyoo vyetu vya kuvuta na karatasi za chooni na chemchemi zinazong’ara ni tofauti na wengine wengi; wengine wote waliobaki hufikiri kuwa bafu ni sehemu iliyolowana, inayonuka, ikiwa wanayo hayo mabafu. Choo kizuri kinamaanisha kuwa pengine una kiwango kizuri cha maisha, kwa hiyo burudika na choo chako. Siku njema ya Vyoo Duniani!

Picha ya choo cha vigae imepigwa na nedrichards kwenye Flickr, Haki Miliki Huru.

2 maoni

  • Matatizo ya uchafu sugu kwenye vyo sana sana zaid Africa wengi hawatili manani kwenye usafi wa choo nandomaana ukienda kwenye vyoo vyetu majumbani utakuta ndio ya chooni chafu kupo la chooni chafu tile’s zimefifia kabisa sink toilet sink ndo usiseme kabisa haritamabiki hata kutumia, so kwa mazingira kama haya ningum kuuepuka uchafu, vile vile kwenye usafi waache kutegeana wasafishe kweli kweli tena kwa wakati, niliwahi kama mtaalam wa maswara ya usafi ushauri wangu ni mhuo,

  • Kwa sisi wa africa bado sana

jiunge na Mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.