Je Sera ya Lugha Tanzania inabagua lugha za asili?

Wanafunzi kutoka shula ya msingi ya Zanaki, Tanzania. picha kutoka World Bank Photo Collection is licensed under CC BY-NC-ND 2.0

Wanafunzi kutoka shule ya msingi ya Zanaki, Tanzania. picha kutoka World Bank Photo Collection is licensed under CC BY-NC-ND 2.0

Kuna takribani lugha 150 nchini Tanzania, lakini lugha ya Kisawhili imepewa upendeleo mkubwa, hasa katika muktadha wa elimu ya msingi. Wanazuoni Hannah Gibson (Chuo Kikuu cha Essex) na Gastor Mapunda (Chuo Kikuu cha Dar es Salaam) wanatoa maoni yao kwa ufupi kuhusu hali hii kwa kutumia matokeo ya utafiti unaochunguza Sera ya Lugha nchini Tanzania na katika nchini nyingine za Afrika.

Katika makala haya tunaeleza kwa ufupi maoni yetu kuhusu muktadha wa lugha za asili na Kiswahili, kwa kuzingatia sera ya lugha inavyoshughulikia lugha hizi. Tutaongelea kwa kifupi kuhusu hali ya wingilugha ya Tanzania, na namna ambavyo sera ya lugha inashughulukia uhalisia huo.

Kutokana na utafiti mkubwa wa Mradi wa Lugha Tanzania (MLUTA) wa mwaka 2009, kuna takribani lugha 150 nchini Tanzania. Katika baadhi ya maeneo ya Tanzania, watoto hukutana na lugha ya Kiswahili wanapoanza masomo yao. Baadhi ya maeneo hayo ni yale ya wanoongea lugha mbalimbali kama vile Kisukuma, Kiha, na Kiraqw kwa mfano. Kuna maeneo mengine Kiswahili hutumiwa kwa kiasi kidogo sana, na maeneo mengine ni kama hakitumiki kabisa, isipokuwa katika shughuli za kiserilaki, mara kwa mara kidini, na katika mikutano ya hadhara. 

Kuhusiana na sera ya lugha, tunachoweza kusema ni kwamba matamko ya kisera yanayohusu  lugha nchini Tanzania, yanapatikana hasa katika Sera ya Elimu na Mafunzo (1995, 2014), Sera ya Utamaduni (1997), na miongozo na matamko mbalimbali kuhusu vyombo vya habari. Kwa ujumla wake, matamko hayo yote hayataji matumizi rasmi ya lugha za asili. Ama kwa hakika, ni Sera ya Utamaduni tu ndiyo inayotamka kwamba “Lugha za asili zitaendelea kutumika kama hazina na chanzo cha kukuza Kiswahili”; na wala haitaji matumizi rasmi ya lugha za asili. Lakini jambo ambalo linashangaza zaidi ni pale ambapo vyombo vya serikali vinahusisha lugha za asili na ukabila na utengano wa kitaifa.

Kwa mfano, gazeti la Majira la tarehe 30 Oktoba 2003 lilimnukuu msemaji wa Tume ya Utangazaji akipiga marufuku redio kutumia lugha za asili kwa madai kwamba matumizi ya lugha hizo ni hatarishi. Hoja yetu ya msingi inahusu namna ambavyo sera ya lugha nchini Tanzania ni baguzi, na inatoa upendeleo mkubwa kwa lugha ya Kiswahili; na kwa kufanya hivyo, kuzihujumu jamii ambazo hazitumii lugha ya Kiswahili kama lugha kuu ya mawasiliano. 

Hata hivyo, utafiti wetu wa kina, unaonesha wazi kwamba matumizi ya Kiswahili katika maeneo mengi ya vijijini katika baadhi ya mikoa katika elimu ya msingi hayasaidii uelewa wa watoto katika masomo yao. Hata ukilinganisha tu matokeo ya mitihani ya taifa ya Darasa la Nne na hata la Saba, tofauti baina ya eneo moja na jingine ni kubwa sana. 

Kwa mfano, katika utafiti wetu huko wilayani Nzega, Tabora, takribani nusu ya watoto wa Darasa la Nne katika shule tuliyoitembelea mwaka 2020 walikariri darasa. Kwa hiyo, Darasa la Nne lilikuwa na watoto mara mbili ya wale waliopo kwenye madarasa mengine. 

Matokeo dhaifu kwenye mitihani hii ya kitaifa katika maeneo ambayo jamii hazitumii lugha ya Kiswahili kwa asili yamebainishwa pia kwenye tafiti za watu wengine. Kwa mfano, Ripoti ya Uwezo ya mwaka 2017 inaonesha kwamba ufaulu wa watoto wa Darasa la Tatu katika utahini wa kusoma, kuhesabu na kuandika ni asilimia 35 tu. Na wanaonesha pia kwamba, hata kwa watoto wa darasa la saba, bado idadi kubwa hawana uwezo wa kujibu maswali ya Darasa la Pili.

Mwanafunzi katina shule ya msingi ya Zanaki. Picha kwa hisani ya World Bank Photo Collection. Leseni ya picha CC BY-NC-ND 2.0

Mwanafunzi katina shule ya msingi ya Zanaki. Picha kwa hisani ya World Bank Photo Collection. Leseni ya picha CC BY-NC-ND 2.0

Je hii tafsiri yake ni nini? Tunadhani kwamba hii ni kuwapotezea watu muda wao, na kwa namna fulani kuwadhalilisha. Tunatoa hoja hii kwa sababu, mtoto anayesoma kwa miaka saba, na bado hawezi kujibu maswali mepesi ya mtoto wa Darasa la Pili, mtoto huyo huchukuliwa kwamba ni mjinga. Lakini hiyo si ukweli. Wana ujuzi za kutosha na unayofaa, lakini hawajapata ujuzi wa kutosha wa lugha ya Kiswahili.

Bila shaka jambo baya zaidi linalosababishwa na sera baguzi ni kuwafanya wazungumzaji wa lugha hizi za asili kuzidharau lugha zao; na wao wenyewe kujiona kwamba hawana maana wala thamani yoyote. 

Katika utafiti wetu mmoja huko Mkoani Ruvuma, mzazi alipoulizwa kama angependa mtoto wake wa Darasa la Pili afundishwe kwa lugha ya Kingoni, alijibu,

“Hapana, sitaki kabisa. Mimi mwenyewe ninazungumza Kingoni. Kimenisaidia nini? Hadi leo mimi ni maskini kwa sababu ya lugha ya Kingoni”.

Je, ni kweli kwamba lugha ndiyo iliyomsababishia ufukara? 

Kwa maoni yetu, kutothamini lugha za asili si jambo jema kabisa, kwa sababu ukweli unabaki palepale kwamba Tanzania ni nchi yenye lugha nyingi. Halikadhalika, ni haki ya kila mwananchi kuheshimiwa na kupewa fursa ya kutambulika kwa namna mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kutumia lugha yake ya asili. Hili linapaswa kushughulikiwa kisera.

Kwa hiyo, pamoja na kusherehekea Kiswahili kutangazwa na UNESCO kuwa miongoni mwa lugha za dunia, hatupaswi kujizubaisha na kusahau kuwa na lugha nyingine zinapaswa kuthaminiwa. Watoto wanapomaliza masomo yao ya msingi wakiwa hawajapata maarifa yaliyokusudiwa, mwisho wake ni wao kukosa kujiamini na kujiheshimu. Kwa maoni yetu, ubaguzi huu haupaswi kufumbiwa macho.

Utafiti huu unatokana na mradi wa ‘Bringing the outside in’, ambao ni mradi wa kimataifa unaoangalia sera za lugha nchini Tanzania, Zambia na Botswana. Wanaotaka kujua zaidi kuhusu mradi huo wanakaribishwa kuangalia tovuti ya mradi ambayo ni  https://multilingual-learning.com/

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.