Julai 7 yatengwa ili kusherehekea siku ya Kiswahili, mradi mpya wa kuelewa tofauti za kilahaja katika lugha hii wazinduliwa

Mwezi Novemba 2021 katika  mkutano wake wa 41 jijini Paris, Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) lilitangaza kwamba tarehe 7 Julai kila mwaka itakuwa ni Siku ya Kiswahili Duniani. Kiswahili – ambacho pia hujulikana kama Swahili- ni lugha ya Kibantu iliyosambaa eneo la Afrika ya Mashariki na Kati ambako hutumika kama lugha mama au lugha ya pili na wazungumzajii wapatao milioni 80.

Licha ya kusambaa katika maeneo mengi, watu wengi duniani hawafahamu umuhimu na historia ya Kiswahili. Global Voices ilifanya mahojiano na Hannah Gibson, mhadhiri mwandamizi katika Idara ya Lugha na Isimu, Chuo Kikuu cha Essex, kuhusu mradi mpya wa miaka minne ambao yeye na watafiti wenzake wameuzindua wenye lengo la kuelewa vizuri tofauti za kilahaja zilizopo  katika Kiswahili.

Katika mahojiano haya, tutawasikia washiriki wa mradi: Hannah Gibson (Chuo Kikuu cha Essex), Fridah Kanana Erastus (Chuo Kikuu cha Kenyatta), Tom Jelpke (SOAS Chuo Kikuu cha London), Lutz Marten (SOAS Chuo Kikuu cha London), Teresa Poeta (Chuo Kikuu cha Essex), na Julius Taji (Chuo Kikuu cha Dar es Salaam) wakieleza kuhusu malengo na faida za mradi, na umuhimu wa lugha ya Kiswahili duniani na Afrika Mashariki. Aidha, wanaeleza kuhusu umuhimu wa Kiswahili kutambulika kidunia

Global Voices (GV): Nini malengo ya mradi huu wa miaka minne?

Washirika wa Mradi (WM): Mradi huu unachunguza jinsi lugha ya Kiswahili inavyozungumzwa kwa namna tofauti kulingana na maeneo waliopo wazungumzaji, pia unachunguza makundi tofauti yanayozungumza lugha hii. Mbali na kuwa lugha ya kwanza kwa jamii nyingi katika ukanda wa pwani ya Afrika Masharika, Kiswahili hutumika na jamii nyingine nyingi kama lugha kiunganishi na hadi sasa kina wazungumzaji wapatao milioni 100. 

Kwa kuwa Kiswahili kinazungumzwa katika mazingira tofauti, tunatarajia kuwa kutakuwa na utofauti mkubwa katika matumizi ya kila siku ya lugha hii.

Tunatambua kwamba wapo wanazuoni waliotafiti kuhusu baadhi ya lahaja za ukanda wa pwani katika siku za nyuma. Aidha, hivi karibuni, baadhi ya lahaja ‘mpya’ – kama vile Kiswahili cha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo- zimekuwa zikijadiliwa. Hata hivyo, hakuna uchunguzi wa kina uliofanayika kuhusu utofauti uliopo katika Kiswahili kinachozungumzwa sasa na namna ambavyo wazungumzaji hutumia utofauti huu kukidhi malengo mbali mbali. Hili ndilo jambo ambalo mradi huu unalenga kuchunguza.

 

GV: Maswali gani mnatarajia kuyajibu kuhusu utofauti wa lahaja katika Kiswahili?

WM: Kwanza, tunataka kupata uelewa wa kutosha wa utofauti uliopo sasa katika Kiswahili. Aidha, wakati tafiti nyingi za kiisimu zimekuwa zikijikita katika utofauti wa matamshi na msamiati (namna maneno yanavyotofautiana katika lahaja mbalimbali), sisi tutajikita katika tofauti za kimuundo – kwa mfano, namna mbalimbali za uundaji wa tungo.  

Swali la pili ambalo tunalenga kulijibu ni namna gani utofauti huu unahusiana na muktadha wa kiisimu ambamo Kiswahili kinazungumzwa. Maeneo mengi katika Afrika Mashariki yana muingiliano wa lugha mbalimbali, yakihusisha watu wanaozungumza lugha kadhaa katika shughuli zao za kila siku. Katika mradi wetu, tunahoji ni kwa namna gani muingiliano kati ya Kiswahili na lugha zingine zinazozungumzwa nchini Kenya na Tanzania unasababisha lugha hizi kuathiriana.

Mwisho, tunataka kufahamu lahaja hizi za Kiswahili zina manufaa gani kwa wazungumzaji na utambulisho wao na namna gani uzungumzaji wa lahaja fulani unaweza kuathiri – au kuakisi – masuala kadhaa ya kijamii. 

GV: Nani washiriki wa utafiti huu? Na kwa nini utafiti huu ni muhimu kwenu?

WM: Mradi huu unaendeshwa kwa ushirikiano kati ya vyuo vikuu vinne toka nchi tatu – Kenya, Tanzania na Uingereza. Watafiti wanatoka katika Chuo Kikuu cha Kenyatta, SOAS Chuo Kikuu cha London, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Essex – kila mshiriki anachangia ujuzi na uzoefu wake katika mradi.  

Tunafurahi sana kutekeleza mradi huu na kujikita katika umuhimu wa Kiswahili. Tafiti nyingi za kiisimu kuhusu lahaja za lugha zimekuwa zikijikita katika mazingira ya Ulaya au zimekuwa zikiegemea katika ukanda wa Kaskazini mwa dunia (kwa mfano kwa kupitia utafiti wa lugha ya Kiingereza), kwa hiyo tumefurahi kufanya utafiti huu unaokipa nafasi Kiswahili.

GV: Utafiti huu una umuhimu gani katika hali ya sasa na maendeleo ya lugha ya Kiswahili?

WM: Idadi ya wazungumzaji wa Kiswahili inaongezeka, na maeneo ambako Kiswahili kinazungumzwa na kufundishwa yanaongezeka pia. Uelewa wa lahaja za Kiswahili una manufaa na maana kubwa. Kwa mfano, unaweza kuchangia kuboresha namna lugha hii inavyofundishwa. Pia unaweza kutusaidia kuelewa vizuri namna ambavyo wazungumzaji wanakitumia Kiswahili na aina ya taarifa ambazo wanazipata. Aidha, unaweza kutupatia mwanga kuhusu umuhimu wa Kiswahili kwa utambulisho wa wazungumzaji na jamii zao na namna ambavyo mabadiliko yanaendelea kutokea.    

Kwa mtazamo wa kitaaluma, utafiti huu unachangia, kukuza na kuendeleza tafiti zilizopo za lugha ya Kiswahili.

GV: Je, mradi unatarajiwa kukamilika lini na watu watawezaje kupata matokeo?

WM: Mradi unafadhiliwa na Wakfu wa Leverhulme na utakamilika ndani ya miaka minne. Umeanza mwezi Septemba 2021 na utakamilika mwezi Agosti 2024. Pamoja na kutumia tovuti ya mradi ambayo itazinduliwa hivi karibuni na kuboreshwa mara kwa mara, matokeo ya utafiti pia yatasambazwa kupitia mtandao. 

Jambo muhimu kwetu ni kuhakikisha kwamba taarifa zote tunazokusanya zinaweza kumfikia mtu yeyote anayezihitaji bila gharama zozote na zinaweza kuwafikia watu ambao wangependa kufanya utafiti zaidi kuhusu lugha ya Kiswahili.

GV: Mwezi uliopita, shirika la UNESCO lilitangaza kwamba terehe 7 Julai kila mwaka itakuwa ni siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani. Nini maoni yako binafsi na maoni yenu kama watafiti wa lugha hii juu ya uamuzi huu?

WM: Tumefurahi sana kusikia maamuzi haya na kwa uhakika tutasherehekea siku hii kwa kuandaa tukio maalum ndani ya mradi.

GV: Kwa nini siku hii ni muhimu?

WM: Ni jambo jema kuona lugha ya Kiafrika ikisherehekewa katika ngazi ya kimataifa na kidunia – uamuzi huu umekuja kwa kuchelewa. Umuhimu, historia na nafasi ya lugha ya Kiswahili bado havijulikani kwa watu wengi duniani na utambuzi huu unaweza kutusaidia kujifunza zaidi kuhusu lugha hii – labda inaweza pia kuwavutia watu kujifunza!  

Matarajio yetu ni kuona Kiswahili kikisherehekewa kwa kuzingatia muundo wake – wa kuhusisha lahaja zake, na makundi mbalimbali ya wazungumzaji ambao kwao lugha hii inaweza kuwa na maana tofauti na pamoja na mazingira tofauti yenye mchanganyiko wa lugha ambako kinazungumzwa. 

GV: Nini faida za muda mfupi na muda mrefu zitakazotokana na Kiswahili kama lugha ya kwanza ya Kiafrika kutengewa siku maalum ya maadhimisho?

WM: Ni matumaini yetu kwamba huu unaweza kuwa mwanzo wa maadhmisho ya kimataifa ya lugha nyingine nyingi za Kiafrika. Kiswahili ni lugha kubwa na ni jambo jema kuona kwamba inatambulika na kusherehekewa. Pia ni muhimu kuhakikisha kwamba Kiswahili hakibaki kuwa mwakilishi pekee wa lugha zingine za Kiafrika bali kiwe mfano wa umajumui wa kiisimu uliopo katika mazingira yetu.

GV: Watu wanawezaje kupata taarifa zaidi kuhusu mradi huu?

WM: Angalieni sehemu hii. Tutakuwa tukitoa taarifa mara kwa mara mtatandaoni kwa Global Voices. Kwa hiyo tutarejea kuwajulisha namna tunavyoendelea. 

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.