Tunayo furaha kubwa kutangaza ujio wa mwandishi na mtafiti wa Kikenya Nanjala Nyabola kujiunga na Global Voices kama mkurugenzi wa mradi wetu wa Advox. Kwa nafasi yake kama mkuu wa kitengo hicho cha utetezi, atatoa mwongozo wa kiuhariri kuhusu uandikaji wa habari, utafiti, uanaharakati na utetezi wa uhuru wa kujieleza na haki za kidijitali.
Kazi anazofanya Nanjala zinahusisha teknolojia, vyombo vya habari na jamii. Ana Shahada ya kwanza ya Sanaa katika Masuala ya Afrika na Sayansi na Siasa kutoka Chuo Kikuu cha Birmingham, Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Masuala ya Afrika na Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Uhamaji wa Nguvu kutoka Chuo Kikuu cha Oxford, na Shahada ya Uzamivu ya Sheria (JD) kutoka Shule Kuu ya Sheria ya Harvard.
Nanjala ameshika nafasi kadhaa za masuala ya utafiti, ikiwa ni pamoja na Taasisi ya Maendeleo ya Nchi za Kigeni (ODI), Taasisi ya Oxford ya Mtandao (OII), na nyinginezo, na amefanya kazi kama mtafiti huru kwenye miradi kadhaa ya haki za binadamu kwa upana, na haki za kidijitali kwa umahususi, duniani kote.
Pia ni mshiriki wa Maabara ya Stanford ya Asasi za Kiraia za Kidijitali, Kituo cha Uvumbuzi katika Uongozi wa Kimataifa (CIGI), Maabara ya Utafiti wa Kidijitali katika Baraza la Atlantic, Kituo cha Haki Miliki na Teknolojia ya Habari (CIPIT) cha Chuo Kikuu Strathmore, ni Kituo cha Ushirikiano wa Kimataifa (CIC) cha Chuo Kikuu cha New York (NYU.)
Nanjala amechapisha kwenye majarida kadhaa ya kitaluma ikiwa ni pamoja na African Security Review na The Women's Studies Quarterly na amechangia kwenye machapisho mengine mengi. Pia huandika safu kwa ajili ya The Nation, Al Jazeera, The Boston Review, na mengineyo.
Nanjala ni mwandishi wa vitabu viwili, “Digital Democracy, Analogue Politics: How the Internet Era is Transforming Politics in Kenya” (Zed Books, 2018) na “Travelling While Black: Essays Inspired by a Life on the Move” (Hurst Books, 2020).