Makala haya na taarifa ya habari ya radio iliyoandaliwa na April Peavey kwa ajili ya kipindi cha The World kilionekana kwa mara ya kwanza kwenye tovuti ya PRI.org mnamo Novemba 5, 2015, na kimechapishwa tena hapa kama sehemu ya makubaliano ya kushirikiana maudhui.
Tritha Sinha ni mwanamke ambaye siku zote anafahamu kile anachokitaka. “Nimekuwa nikitaka kuwa huru na kuacha kumtegemea baba yangu kwa fedha za kujikimu au kuwategemea rafiki zangu wa kiume au kaka na watu kama hao,” anasema.
Sinha ni nguzo inayotengemeza bendi yenye makazi yake jijini New Delhi na Paris iitwayo Tritha Electric. Alikulia eneo la Kolkata na anasema, nchini India, wanawake waliomzunguka hawakuwa watu wenye furaha. Walikuwa wakiishi katika maisha ya ugandamizi. “Nimeshuhudia mama yangu pamoja na shangazi zangu wakilia, wakati mwingine hata walimu katika shule nilizosoma -na hali hiyo ilinifanya nijisikie kwamba kuna mambo hayaendi ipasavyo.”
Muziki, Tritha Sinha anasema, ulikuwa njia ya kutokea -tiketi ya kuelekea kwenye uhuru wa kifedha na kujitegemea.
Uhuru huo ulianza tangu akiwa mdogo. Tritha Sinha alianza kuimba akiwa na miaka mitano tu.
Alijilipia ada ya chuo kwa kuimba kwenye filamu za ki-Hindi. Lakini kuimba nyimbo zilizoandikwa na wengine halikuwa jambo linalomtosheleza. Ah, hapana, alihitaji kuandika nyimbo zake mwenyewe nakumiliki bendi yake mwenyewe.
Hapo ndipo bendi ya Tritha Electric inaanza.
Sinha anaiita muziki wa ethno-punk .
Sehemu ya ethno ni kuendeleza asili yake ya muziki wa ki-Hindi na punk, anasema, inamsaidia kuelezea mapambano ya kuwa mwanamke anayejitegemea nchini India leo.
Albamu mpya ya bendi ya Tritha Electric inaitwa Pagli. Maana yake ni ‘mwanamke mtukutu’ kwa lugha ya ki-Bengali. Na nyimbo zote kwenye albamu hiyo zinasimulia hadithi ya mwanamke anayejisikia kufungwa na mila. Lakini anavunja mila hiyo na kujipatia uhuru. Ni kama Tritha Sinha mwenyewe.
Anasema, “Kuugundua uhuru wakati mwingine tunahitaji kupitia nyakati ngumu au hata ukichaa wakati mwingine ili kuelewa nini maana ya uhuru na kwa jinsi gani uhuru waweza kuwa muhimu kwa utu wetu wa ndani. Na hiyo ndiyo iliyofungua mlango wa mafanikio yangu kimziki.”