Ndani ya nchi nyingi duniani, unyanyasaji wa kijinsia ni tatizo la zamani. Lakini katika wakati huu wa kidigitali kukiwa na harakati za hashitagi kama vile #Mimipia na majukwaa ya kijamii ambapo unyanyasaji wa kijinsia unaweza kusambazwa na kuonekana, uwiano wa nguvu baina ya wananyanyasaji na wanaonyanyaswa umeonekana kuhama.
Mfano wa hivi karibuni toka Pakistan, ambapo video ilionesha mwanaume akiwafuata wanawake na kuwabughudhi ilienea Facebook na Twita ikisababisha umma kulaani kitendo hicho na kusababisha mtu huyo kukamatwa.
Mwaka 2016 huko bonde la Kalash katika mkoa wa Chitral Kaskazini mwa Pakistani, Aimal Khan alianza kufuata kundi la wanawake akiwarekodi kwa kutumia simu yake. Alitoa maneno ya dharau dhidi ya wanawake hao na akaendelea kuwataka wapige picha naye, pamoja na kukataliwa na kutishiwa nao kuwa watamripoti polisi. Khan aliwaambia hata yeye ni afisa wa polisi.
Wakati haioneshi ni lini hasa video hiyo ilitengenezwa, Khan aliiposti huko YouTube tarehe 19 Julai 2016. Miaka miwili baadaye, ukurasa wa Facebook unaoitwa ‘Waislamabadi’ uliiweka video hiyo katika tovuti za mitandao ya kijamii na ilisambaa sana. Watu walianza kuwatagi polisi wakiwataka wamkamate mtu huyo. Juni 19 2018, polisi wa Chitral waliitikia wito huo wakisema kuwa wanajaribu kufuatilia mahali alipo.
Wakati huo huo video nyingine iliibuka ambapo Aimal Khan alionekana akiomba radhi kwa kitendo kile. Juni 22, alikamatwa na polisi wa Chitral, ambapo walitumwa polisi wa kike kutekeleza zoezi hilo. Pia polisi walitoa maelezo kuwa Khan sio afisa wa polisi kama alivyodai hapo awali.
Mitandaoni, watu walionesha kuunga mkono kukamatwa kwake.
Proud to see a lady constable with full traditional dress cuffing the guy who was involved in a ladies harassment case in chitral Pakistan.#womenpower #ChitralPolice #kpkpolice #GAPakistan https://t.co/N0fNQPmpTc
— King Khan (@BadshahSindhi) June 22, 2018
Aimal Khan, the person who harassed women in Kalash Valley, Chitral has been arrested by Chitral Police. Thanks to all those who stood with the marginalized women of Kalash valley and shared the vedio on social media. This is the power of social media. #stopwomenharrasment https://t.co/LXGpxQTU32
— irfanuddin (@irfanuddinbaba) June 22, 2018
Lakini pia maswali yaliulizwa kuwa ni kwa kutumia kifungu kipi cha sheria Khan alikamatwa?
Sir @ChitralPolice can I ask you a friendly question?
How was Aimal Khan arrested when there was no FIR against him by the actual victims?
Under what law? (Continued)
Cc: @JavedAzizKhan, @alibabakhel @DC_Chitral https://t.co/udfDgMn6lh
— Shahzad Khan (@shazadk) June 24, 2018
Cha kushangaza wengi ni kuwa muda mfupi baadaye Aimal Khan aliachiwa kwa dhamana. Anasubiri kesi yake
Global Voices iliongea na Afisa wa Polisi wilaya ya Chitral Bwana Furqan Bilal, ambapo alisema;
Aimal Khan aliachiwa kwa dhamana baada ya kufunguliwa mashtaka kwa kifungu cha sheria kinachoruhusu dhamana. Katika Ripoti ya Taarifa ya Awali Aimal Khan ameshitakiwa chini ya vifungu vya 354 (kumbughudhi mwanamke), 419 (kudanganya kwa kujifanya mtu mwingine), 294 (kufanya vitendo vya kuchukiza maeneo ya umma) na 341 (kuzuia isivyo halali) vya Makosa ya jinai ya Pakistani badala ya vifungu vya Makosa ya Mtandao ya Pakistani. Kesi yake itaanza kusikilizwa hivi karibuni.
Wanaharakati wanatatizwa na sheria zilizotumika katika Ripoti ya Taarifa ya Awali. Ingawa Sheria ya Kuzuia Makosa ya Kimtandao inahusika na unyanyasaji wa aina hii na ingeweza kutumiwa katika shauri hili la Khan, sheria ilikuwa haijapitishwa mpaka Agosti 2016 baada ya kitendo hiki kufanyika huko Chitral.
Nighat Dad, mtaalamu wa teknolojia na sheria anayeendesha shirika lisilo na maslahi Mfuko wa Haki za Kidigitali na huchangia maudhui ndani ya Global Voices, alifafanua kwa Global Voices kuwa Sheria ya Makosa ya Jinai ya Pakistan yenyewe haina msaada katika mashauri yanayohusiana na video za kudhalilisha.
Dad pia alizungumza kuhusu mitandao ya kijamii kuchochea kwa sehemu kubwa kukamatwa kwa Aimal Khan, akigusia athari za jamii kupiga kelele juu ya suala hilo na kuchochea polisi kuchukua hatua. Alibainisha kuwa kukamatwa kwa haraka kwa Khan kumepeleka “ujumbe chanya kwa jamii” lakini ni jukumu la vyombo vya sheria pamoja na mahakama kulipeleka jambo hili mbele na kuhakikisha haki inapatikana.
Matukio kama haya sio mapya. Julai 2017, Meenah Tariq wa Lahore alikwenda kwenye Bonde la Hunza katika mkoa wa Gilgit-Baltistan huko Pakistan kwa kutalii. Alidhalilishwa na vijana wa kiume akiwa njiani. Kwa kuwa hakujua jinsi ya kuwafungulia mashtaka, alichukua picha zao na kuanzisha kampeni mtandaoni ambayo ilienea kote.
Katika shauri la Tariq mamlaka za nchi zilichukua hatua stahiki. Wakati kamishna msaidizi wa Hunza, Anas Goraya alipofahamu suala lake alifungua simu ya msaada wa dharura kwa ajili ya kukabiliana na mambo hayo huko Hunza.
Tariq alishirikisha matokeo ya simulizi yake huko Facebook, ambapo alielezea jinsi ilivyokuwa vigumu kushirikisha jambo lake mtandaoni–na kuvumilia wimbi la udhalilishaji uliofuatia–na hisia alizozipata baada ya kuthibitisha kuwepo kwa simu ya msaada kwa ajili hiyo:
Ni mara ngapi ulishaambiwa ni kazi bure kulalamika? Ni kazi bure ukiongea, hakuna kitakachobadilika? Huu ni uthibitisho kuwa sio mara zote ni hivyo. Huu ni uthibitisho kuwa tunatakiwa kuongea kuhusu mambo tunayokumbana nayo, kuwa na mazungumzo hayo, anzisha majadiliano hata kama ni vigumu.
Kukamatwa kwa Aimal Khan kufuatia kelele za raia katika mitandao ya kijamii ni ishara nzuri. Lakini katika shauri hili swali linalobaki ni je haki itatendeka?