Waganda Wasema Hapana Dhidi ya Kodi ya Mitandao ya Kijamii Kwa Sababu Inawanyonya Wanawake, Vijana na Maskini

Waganda wameinuka kupinga kodi mpya ya mitandao ya kijamii na akaunti za fedha katika simu.

Tarehe 1 Julai 2018, serikali ya Uganda ilianza kutoza kodi mitandao ya kijamii kwa wananchi kulipia shilingi za uganda 200 (sawa na dola za kimarekani 0.05) kwa kutumia mitandao ya kijamii hali iliyoibua lawama kubwa kutoka kwa waganda.

Kwa wastani pato la taifa la Uganda ni dola za kimarekani 604.00. Kwa matumizi ya mitandao ya kijamii na kutuma ujumbe kila siku inagharimu hadi asilimia tatu ya wastani wa mapato ya mwaka ya mwananchi wa kawaida wa Uganda.

Mapambano ya kupinga kodi ya mitandao ya kijamii ilichukua mlengo wa sheria tarehe 2 Julai pale wananchi husika walipopiga hodi mahakamani wakilalamika kwamba kodi hiyo inavunja katiba ya Uganda.
Walalamikaji walitoa hoja kwamba kodi hiyo ni kinyume na haki za binadamu za waganda kama ilivyoelezwa “katika vifungu vya katiba ya mwaka 1995 ya Jamhuri ya Uganda “.

Gazeti la Kenya linaripoti:

Ombi liliwekwa na timu ya mawakili vijana chini ya kampuni yao ya Sheria ya Mtandao kwa kushirikiana na watu binafsi wanne ambao ni Mr Opio Bill Daniel, Mr Baguma Moses, Mr Okiror Emmanuel na Mr Silver Kayondo dhidi ya mwanasheria mkuu wakihoji kikatiba uhalali wa kulipa kila siku (shilingi za Uganda 200) [sawa na dola za kimarekani 0.05] kwa ajili ya kutumia majukwaa ya mitandao ya kijamii.

Ombi hilo lililenga baadhi ya vifungu hasa vya sheria ya marekebisho ya mwaka ya 2018 ya ushuru wa bidhaa na huduma , ambayo iliweka kodi kwenye huduma za matumizi ya simu.

Kodi hiyo inavunja haki za msingi za uhuru wa kutoa maoni na kupata habari ambazo zimeelezwa katika katiba ya Uganda lakini pia zinalindwa kwa mikataba ya kimataifa ikiwemo Mkataba wa kimataifa wa haki za kiraia na kisiasa na Azimio la Haki za binadamu Duniani — ambapo Uganda imesaini mikataba hiyo yote.

Pia, walalamikaji waliiomba mahakama kutoa amri ambayo itaondoa moja kwa moja malipo ya kodi ya mitandao ya kijamii. Gazeti la PCTech linaripoti:

Wanaiomba mahakama kutoa amri kwa serikali, mamlaka nyingine zinazohusika, mawakala na maafisa wake kusimamisha mara moja kuweka kodi yoyote kwa ajili ya mtandao na matumizi ya mitandao ya kijamii. Pia, wanaiomba kutoa amri inayoelekeza serikali na chombo cha kudhibiti mawasiliano; Tume ya Mawasiliano Uganda kudhibiti huduma za mtandaoni katika njia inayowafanya watumiaji kupata mtandao kwa uhuru na kwa uwazi.

Mwanasheria wa Uganda Silver Kayondo aliapa “kupambana hadi mahakama ya Afrika juu ya haki za binadamu “:

Raymond Mujuni aliungana na walalamikaji wa Kodi ya mitandao ya kijamii katika kuwalinda waandishi wa habari na matumizi ya mitandao ya kijamii na matangazo ya kidijitali. Tunaelekea mahakamani kuandikisha kesi dhidi ya mwanasheria mkuu, Tume ya mawasiliano na mamlaka ya mapato Uganda.Tutapambana hadi mahakama ya Afrika juu ya haki za binadamu.

Jamii ya Global Voices ambayo tunawakilisha imechukua uamuzi juu ya suala hili na imepanga kutuma ujumbe wa mshikamano kwa wanaharakati wa Uganda siku ya Jumatatu, Julai 9.

Hapana kwa bango la kampeni dhidi ya kodi ya mitandao ya kijamii. (Picha na Innocent Amanyire @NinnoJackJr na imetumia kwa ruhusa)

Kutokana na vita ya sheria, maswali kuhusu usawa, haki na upatikanaji wa mtandao vinahitaji uchunguzi zaidi. Kutokana na utafiti uliofanywa na mamlaka ya taifa ya teknolojia ya habari, asilimia 77 ya waganda hawawezi gharama za matumizi ya msingi ya mtandao na 22 asilimia tu ya idadi ya watu katika nchi ya Uganda wanatumia mtandao.

Badala ya kuwekeza katika miundo mbinu ambayo ingepanua upatikanaji wa uunganishwaji wa kihamisha taarifa-pepe kwenye mitandao kwa waganda, serikali imeweka kodi ya mitandao ya kijamii ambayo inazuia kabisa upatikanaji wake na wakati huo ikichota fedha kutoka kwenye hazina yake yenyewe.

Ukosoaji unaona kodi hiyo kama ina sura ya kodi mara mbili kwa sababu muda wa maongezi na taarifa –pepe vinakuwa vimeshakatwa kodi. Sasa watumiaji wengi wanasema hawawezi kukabili malipo ya sh. 200 zaidi kwa siku kupokea na kuwasiliana kupitia majukwaa ya mtandaoni; pia kama inavyojulikana matumizi mtandaoni ni muhimu.

Kodi hiyo inaongeza na kupanua nafasi ya kutopata mtandao sio tu kwa vijana na watu maskini lakini pia kwa wanawake na inaongeza jinsia kutengwa kidijitali.

Kuwasamehe matajiri: Kutoza kodi maskini. Mitandao ya kijamii

Vijana wa Uganda waliopo mstari wa mbele katika mitandao ya kijamii wanataka kodi ya mitandao ya kijamii kupunguzwa

Uganda ni nchi yenye kiasi kikubwa sana cha ukosefu wa ajira katika Afrika Mashariki. Taarifa ya sensa ya mwaka 2014 Uganda inaonesha zaidi ya milioni 18 ya watu wenye miaka kati ya 14 na 64, asilimia 58 yao hawana ajira. Wakati huo, asilimia 52 ya waganda wanamiliki simumpanguso na asilimia 71 ya watumiaji simu hizo wanaishi vijijini. Kutokana na ripoti ya 2014 ilitolewa na Tume ya mawasiliano ya Uganda.

Vijana kati ya miaka 15 na 24 wapo mstari wa mbele katika kutumia simumpanguso na ni asilimia 28 ya watu wa Uganda. Wengi wao wanategemea simu zao kupata kazi hasa kupitia mtandao wa WhatsApp ambao huendeshwa na fedha zilizopo kwenye simu . Wanaona kuwa kodi ya mitandao ya kijamii inaua tu ujasiriamali, urahisi wa kufanya biashara na ubunifu.

Ushirikiano wa sera ya TEHAMA kimataifa katika Afrika Mashariki ilieleza kuwa gigabaiti (GB) moja tu ya taarifa-pepe itagharimu watumiaji wa mitandao karibu asilimia 40 ya wastani wa mapato yao kwa mwezi:

Gharama ya kumuunganisha mwananchi maskini wa Uganda itapanda kwa 10% ambayo itakuwa GB moja tu ya taarifa-pepe ambayo itagharimu karibu 40% ya mapato yao kwa mwezi. Matajiri wa Uganda watapata ongezeko la 1% katika gharama za kuunganisha!

Kutokuheshimu wananchi ambao tayari wana mzigo mkubwa

Kodi ya mitandao ya kijamii imeanzishwa kutokana na mkanganyiko wa “kodi ya umbea kwenye mitandao ya kijamii “mwezi Aprili 2018 na inaonekana ni kutowajali wananchi ambao tayari wanamzigo mkubwa. Wakati ule, Rais Mseveni alipoandika:

Sitapendekeza kodi kwa matumizi ya mtandao kwa ajili ya madhumuni ya elimu, utafiti au rejea…..hayo lazima yatabaki kutolewa bure. Hata hivyo, Ulugambo (Umbea)katika mitandao ya kijamii (maoni, chuki, matusi, maongezi ya kirafiki) na matangazo kupitia mtandao wa Google na sijui nani mwingine ambaye atalipa kodi kwasababu tunahitaji rasirimali kukabili athari za lugambo.

Serikali kuainisha matumizi ya mitandao ya kijamii kuwa ni shughuli ya anasa kumefichua ukosefu mkubwa wa elimu ya kidijitali miongoni mwa watengeneza sera katika serikali ya Mseveni.

Mwandishi wa habari Uganda Daniel K. Kalinaki kwa ufupi alieleza matokeo ya kila siku kwa wananchi wa Uganda kutokana na “kodi ya umbea” na “kodi ya mitandao ya kijamii “:

Kimsingi, kutokana na kodi ya mitandao ya kijamii kunaleta matatizo mawili. Kwanza, mtu asiyehusika anaingia gharama mara mbili: Mtumiaji wa Facebook anakuwa ameshalipia kodi kupitia simu ya mkononi, taarifa-pepe na umeme pia; mara chache sana wanavyovizalisha havilipiwi kodi. Inaonekana kodi inachukua fedha mlangoni halafu tena inatoza gharama ya viti katika uwanja mtupu.

Pili, kwa ujumla watu hawafanyi umbea au kutukana watu kwa ajili ya kuishi; wanafanya hivyo kwa sababu hawana la kufanya, wana masikitiko na hawana kazi. Kuweka kodi ili kunawafanya wawe kimya badala yake ni sawa na kuwaomba watu ambao hawana mtama wale keki ya velveti chokoleti nyekundu. Kodi ya mitandao ya kijamii na ya fedha ya muda wa maongezi kwenye simu imewafanya vijana na watu maskini wengi ukijumuisha watu waishio vijijini ambao waliokuwa hawajalipa kodi moja kwa moja kupitia mfumo wetu wa kodi. Unaweza kusikia kelele hizo kutoka Kidera hadi Kyotera.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.