Waandishi wa habari wanawake nchini Uganda wanabeba ‘mzigo maradufu’ kutokana na mashambulizi ya mtandaoni pamoja na udhalilishaji

Mwandishi wa habari wa Uganda Gertrude Uwitware Tumusiime ameonja matukio ya “mzigo maradufu” wakati akifanya kazi kama mwandishi wa habari mwanamke nchini Uganda. Picha ya Skrini kutoka “The Other Side: Gertrude Uwitware Tumusiime” kwenye YouTube.

Nchini Uganda, waandishi wa habari wanawake wanaotumia vifaa vya kidijitali kuripoti, kutoa maoni na kupata habari hukabiliwa na mashambulizi na udhalilishwaji kwa sababu wanachunguza na kuchapisha maudhui nyeti ya kisiasa.

Dhuluma za mtandaoni zimekuwa mbinu mpya ya udhibiti. Waandishi wa habari wanawake wanaubeba mzigo maradufu wa dhuluma inayotokana na jinsia mtandaoni ikiwa ni pamoja na vitisho vinavyohusiana na kuandika habari za kisiasa.

Vitisho hivi vinavyoendelea vimesababisha waandishi wa habari wanawake kujiondoa kwenye  mijadala ya masuala ya umma – na kuacha taaluma ya uandishi wa habari kutawaliwa zaidi na wanaume

Joy Doreen Biira, mwandishi wa habari. Picha na Wazabanga kupitia Wikimedia Commons CC BY 3.0.

Mnamo Novemba 2016, mwandishi wa habari wa Uganda, Joy Doreen Biira, aliyekuwa akifanya kazi katika televisheni binafsi ya Kenya Television Network (KTN) nchini Kenya, alirejea nyumbani Uganda kwa ajili ya sherehe ya kitamaduni.

Wakati Biira akiwa kwao, vikosi vya usalama vya Uganda vilipambana na walinzi wa ufalme wa Rwenzururu katika mkoa wa Rwenzori magharibi mwa Uganda, na ikulu yao ikateketezwa kwa moto. Mapambano hayo ya kufyatuliana risasi yalisababisha vifo vya watu 62, wakiwemo polisi 16.

Biira aliandika hisia zake kuhusiana na tukio hilo la shambulizi la kijeshi kwa kuchapisha maoni yake kwenye Facebook mnamo Novemba 27:

It’s so sad what I’ve witnessed today with my own eyes — part of the palace of the kingdom I’m from, the Rwenzururu Kingdom, burning down. It felt like watching your heritage deplete before my eyes.

Inasikitisha sana kile nilichokishuhudia leo kwa macho yangu mwenyewe – sehemu ya jumba la ufalme huko nitokako, Ufalme wa Rwenzururu, likiteketea kwa moto. Nilijihisi kana kwamba nilikuwa nikitizama urithi ukiangamizwa mbele ya macho yangu.

Siku hiyo hiyo, Biira alikamatwa na kutuhumiwa “kusambaza picha tata za matukio hayo ya kutisha ya mapigano kati ya vikosi vya usalama na walinzi wa mfalme wa Rwenzururu … kwa kundi la WhatsApp lenye wanachama wengi,” kwa mujibu wa Committee to Protect Journalists (CPIJ). Alichapisha pia “video ya Instagram ya jumba la mfalme likiwaka moto na kuandika habari zake kwenye Facebook,” taarifa za CPJ zilisema.

Maafisa wa usalama nchini Uganda walidaiwa kumlazimisha Biira “kufuta machapisho kwenye mitandao ya kijamii” na “vifaa vyake vya kidijitali vikatwaliwa,” kwa mujibu wa ripoti ya Freedom House ya 2018.

Biira alishtakiwa kwa kosa la kuunga mkono ugaidi kwa kuchukua video za shambulio la kijeshi kwenye ikulu ya mfalme – kosa ambalo adhabu yake ni kifo chini ya sheria ya kupambana na ugaidi kama mtu akipatikana na hatia. Hata hivyo, siku moja baadaye, aliwachiliwa kwa dhamana.

Kisa hicho cha Biira kilizua shutuma kali kwenye mitandao ya kijamii kupitia kauli mbiu kamaa vile #FreeJoyDoreen na #JournalismIsNotaCrime.

Mwanamtandao huyu alimshutumu Rais wa Uganda Yoweri Museveni kwa tabia yake ya kuwanyamazisha waandishi wa habari:

#FreeJoyDoreen Rais @KagutaMuseveni hana budi kuacha tabia ya kuwanyamazisha waandishi. Kitendo hicho ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu katika bara letu.

Wakili wa Biira, Nicholas Opiyo, alichapisha twiti iliyoonyesha mashtaka rasmi aliyokabiliwa nayo Biira:

Nakala ya dhamana ya Joy—anayeshtakiwa na kosa la kusaidia ugaidi (kichekesho!)  #journalism (uandishi wa habari) si uhalifu @KTNKenya @KTNKenya  #FreeJoyDoreen

Opiyo aliiambia Global Voices kuwa kesi ya Biira ilitupiliwa mbali na kufutwa mnamo Machi 2017 baada ya utawala kufanya uchunguzi na kukosa ushahidi wa kumfungulia mashtaka mahakamani.

“Sawa na kesi nyinginezo kama hizi, mtu hutua mzigo kwenye nafsi lakini hubaki na hisia ya uonevu, ukosefu wa haki, na maumivu,” alisema Opiyo, ambaye pia ni mkurugenzi mtendaji wa Chapter Four Uganda, ambalo ni shirika la haki za binadamu. Opiyo aliongeza kwamba kukaa jela siku kadhaa na kustahimili maumivu ya kutiwa nguvuni ni hisia ambazo kamwe hazimtoki mtu.

Mashambulizi ya kulenga mtandaoni

Ni nadra sana kwa waandishi wa habari wanawake wanaokumbwa na dhuluma mtandaoni kupata haki, na mara nyingi huwa na wakati mgumu kuhakikisha kwamba malalamiko yao yanachukuliwa kwa uzito na kuchunguzwa ipasavyo.

Mnamo Aprili 2017,  Gertrude Tumusiime Uwitware, mtangazaji wa runinga ya NTV Uganda, alimtetea Stella Nyanzi, mwanaharakati msomi aliyeukosoa utawala wa Museveni kwa kutotimiza ahadi za kampeni za kuwasambazia taulo za sodo wasichana masikini.

Watawala walimlazimisha Uwitware kufuta machapisho yake ya Twitter na Facebook yenye maoni ya kumuunga mkono Nyanzi. Alipokea vitisho kwenye Facebook na kisha kutekwa nyara na watu wasiojulikana kwa takribani saa nane, kulingana na ripoti ya haki za binadamu ya Uganda ya 2017. Watekaji nyara wake walidaiwa kumhoji kuhusu uhusiano wake na Nyanzi, wakampiga vibaya na hata kuzikata nywele zake.

Uwitware baadaye alipatikana katika kituo cha polisi jijini Kampala. Hata hivyo, utawala haujatoa taarifa zozote hadi leo kuhusu uchunguzi wa kutekwa kwake.

Waandishi wa habari za kisiasa – hasa wale wanaoangazia siasa za vyama vya upinzani – mara kwa mara wanashuhudia vitisho zaidi ikilinganishwa na wale wanaoangazia masuala mengine. Lakini waandishi wa habari wanawake wana hali iliyo mbaya zaidi kwa sababu serikali inaamini wao ni dhaifu na wanatishwa kwa urahisi zaidi, kwa mujibu wa Mukose Arnold Anthony, Katibu wa Usalama wa Vyombo vya Habari na Haki za Binadamu katika Chama cha Waandishi wa Habari wa Uganda (UJA), ambaye alizungumza na Global Voices kupitia WhatsApp mnamo Aprili 3.
Linapokuja suala la unyanyasaji wa kingono mtandaoni, “waandishi wa habari wanawake wanaogopa kujiweka wazi…japo wachache…wanaeleza bayana–wengi wao huishia kuumia nalo kimoyomoyo,” Anthony alisema.

Hutokea kwa waandishi wa habari wanawake kukumbana na madhara zaidi ya kisaikolojia, ukiukwaji wa faragha yao, kuharibiwa utambulisho, upunguzaji fursa zao za kwenda huku na kule, udhibiti, na upotezaji wa mali kwa sababu ya kazi zao, kwa mujibu wa utafiti wa UNESCO kuhusu uhuru wa kujieleza barani Afrika uliochapishwa mnamo 2018.

Na, kwa mujibu wa utafiti wa Mtandao wa Haki za Binadamu kwa Wanahabari-Uganda wa 2018, asilimia 12 ya wanahabari wanawake wamekumbana na dhuluma na ukiukwaji, vikiwemo vitisho vya vifo na kukamatwa. Robo tatu ya waandishi wa habari wanawake wamekumbana na ukiukwaji haki katika mikono ya maofisa wa serikali kama vile polisi, wakuu wa wilaya na maofisa wengine wa usalama.

Mashambulio na unyanyaswaji

Mwanahabari wa Uganda Bahati Remmy amekumbana na mashambulio na unyanyaswaji akiwa katika shughuli za kazi kama ripota mwanamke. Picha kupitia akaunti ya Paydesk ya Bahati Remmy, imetumika kwa ruhusa.

Bahati Remmy, mwanahabari mwanamke wa Uganda ambaye kwa sasa anafanya kazi Marekani, aliiambia Global Voices kuwa aliacha kufanya kazi ya uandishi nchini Uganda kwa sababu alihisi kupoteza shauku baada ya tukio la kutisha alipokuwa anaangazia taarifa za uchaguzi nchini Uganda mnamo 2016.

Polisi wa Uganda walimkamata Remmy wakati akifanya matangazo ya moja kwa moja kupitia runinga ya NBS inayomilikiwa na mtu binafsi ili kuangazia kuzuiliwa nyumbani kwa kiongozi mkuu wa upinzani Dk. Kizza Besigye katika mji wa Kasangati.

Remmy aliiambia Global Voices:

The police engaged in a running battle not to allow any journalists to cover the story concerning Besigye.

Polisi walizua hali ya taharuki wakati wa kuwazuia wanahabari kuangazia taarifa kumhusu Besigye.

Polisi walinipapasa matiti yangu kwenye gari lao, wakanivua nguo kituoni na kuniacha uchi mbele ya kamera, kwa mujibu wa Remmy.

Pia alifuatiliwa na kunyanyaswa na ofisa wa polisi kwenye Facebook kwa sababu serikali ya Uganda ilidhani kwamba alikuwa ameshirikiana na Besigye kuichafulia nchi taswira. Aliiambia Global Voices kuwa ujumbe wa maandishi kutoka kwa watu wasiojulikana uliachwa mlangoni pake ukitoa vitisho vya kumteka iwapo angekataa kutoa siri ya njia atakayotumia Besigye kutoka nyumbani kwake.

Baada ya kisa cha ukamatwaji wa Remmy, Mtandao wa Haki za Binadamu za Wanahabari – Uganda uliandaa kura ya maoni kupima hali halisi ya mambo kuhusu kisa hicho. Waliuliza: “Polisi ya Uganda ilidai kuwa ripota wa runinga ya NBS Bahati Remmy alikiuka maagizo halali na pia aliwazuia polisi kuifanya kazi yao hivyo kuwafanya kumkamata. Je, unakubaliana na hili?

Magambo Emmanuel aliandika:

It is a lame excuse and total lie because there is video footage that shows how Bahati was arrested. Police should stop shifting their problems to innocent journalists.

Ni sababu dhaifu na uongo mtupu kwa sababu kuna mkanda wa video unaoonyesha jinsi Bahati alivyokamatwa. Polisi wanapaswa kuacha kuyaelekeza matatizo yao kwa wanahabari.

Davide Lubuurwa aliandika:

…Whoever tries to let the people know how the state is standing is to be arrested. A very big problem is coming to Uganda soon. What bothers me most is that whoever tries to say something that is not in support of the current regime is taken to be a rebel so the Ugandan people must wake up.

…Yeyote anayejaribu kuwajuza watu kuhusu hali ya taifa lazima akamatwe. Tatizo kubwa linakuja Uganda hivi karibuni. Kinachoniudhi ni kwamba yeyote anayejaribu kutamka jambo lisilounga mkono utawala uliopo anachukuliwa kana kwamba ni mwasi kwa hivyo ni sharti watu wa Uganda wazinduke.

Wanahabari wengi wanawake nchini Uganda wameacha kazi ya uandishi wa habari hasa zile zinazoikosoa serikali kwa hofu ya kushambuliwa na kudhulumiwa na utawala. Wataalamu wa habari wameelezea kuwa serikali na vyombo vya usalama huwapigia simu wahariri na kuwaagiza “kutochapisha habari zinazoipa serikali mwonekano hasi.”

Mashambulio haya huwa hayaripotiwi – haswa na wanawake – hali inayosababisha ugumu wa kuelewa kina halisi cha tatizo hili.
Remmy aliiburuta serikali ya Uganda kwenye Tume ya Haki za Binadamu ya Uganda, lakini hadi leo, hakuna lililojiri kuhusu kesi yake. Tume inakosa uhuru unaotakiwa kufanya maamuzi kwa upande wa wale wanaowasilisha malalamiko dhidi ya serikali. Wajumbe wake saba, pamoja na mwenyekiti wake, wanateuliwa na rais, kwa idhini ya Bunge. “Wana upendeleo,” Remmy alisema, huku akiongezea:” Wana mrundikano wa kesi, na kesi nyingi wanazotaka kuzisikiliza ni zile zinazowasilishwa na serikali.”

Vitisho vingi vinavyowakumba wanahabari wanawake mtandaoni vinahusiana kwa karibu na vile vya dhuluma dhidi yao nje ya mtandao.

Remmy anaamini kuwa haki, hali na hadhi ya wanahabari wanawake zinapaswa kuzingatiwa nyakati zote kwa sababu mashambulio dhidi ya wanawake yanakandamiza sekta ya uwanahabari kwa jumla.

Uganda inapojiandaa kufanya uchaguzi wa urais na ubunge mnamo 2021, mashambulio na udhalalishwaji wa waandishi wa habari wanawake na serikali unapaswa kukomeshwa kwa sababu unaathiri ufikiaji wa habari, uhuru wa kujieleza na haki za demokrasia za raia wa Uganda.

“Uhuru wa waandishi wa habari unasalia kuwa mtoto anayepuuzwa katika mfumo wa nchi,” Remmy aliiambia Global Voices.

Makala haya ni sehemu ya mfululizo unaoitwa “Jedwali la Utambulisho: Jukwaa la kudhibiti vitisho vya mtandaoni dhidi ya uhuru wa kujieleza barani Afrika,” Machapisho haya yanahoji kauli za chuki zenye utambulisho au kubagua kwa misingi ya lugha au asili ya kijiografia, habari potovu na udhalilishwaji (haswa dhidi ya wanaharakati wanawake na waandishi wa habari) uliokithiri mtandaoni katika nchi saba za Kiafrika: Algeria, Kamerun, Ethiopia, Nigeria, Sudani, Tunisia na Uganda. Mradi huu umefadhiliwa na Mfuko wa Haki za Kidijitali wa Afrika wa shirika la Ushirikiano wa Sera za kimataifa za TEHAMA kwa ajili ya Mashariki na Kusini mwa Afrika (CIPESA).

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.