Nchini Tanzania, Serikali kukanusha uwepo wa UVIKO -19 kwawanyima wananchi taarifa muhimu za afya

Kijana akitazama simu yake ya kiganjani nchini Tanzania, Desemba 9, 2018. Picha na Riaz Jahanpour, kwa mradi wa USAID / Mawasiliano ya Maendeleo ya ki-Dijitali kupitia mtandao wa Flickr, CC BY 2.0.

Kirusi cha kwanza cha Korona kiliripotiwa nchini Tanzania katikati ya mwezi Machi, 2020. Hata hivyo, baada ya takwimu kuendelea kupanda na kufikia wagonjwa 509 na vifo 21 mwishoni mwa mwezi Aprili, serikali ya Tanzania ilitangaza kuwa “hakuna hata mgonjwa mmoja wa UVIKO-19″ mwezi Juni.

Mwezi huo huo, Kassim Majaliwa, Waziri mkuu wa nchi hiyo, aliliambia bunge kwamba kulikuwa na wagonjwa 66 tu  nchini kote, lakini hakutoa ufafanuzi zaidi.

Tangu wakati huo, serikali imekuwa kimya kuhusiana na virusi vya Korona huku matamko makali ya kisiasa kukanusha uwepo wa virusi hivyo yakiendelea kutolewa bila kuambatana na takwimu zozote za wagonjwa wala vifo.

Leo, shughuli nyingi zinaendelea kama kawaida, ikiwa ni pamoja na sekta ya utalii nchini Tanzania, inayovutia maelfu ya wageni kuingia nchini humo kupitia viwanja vya ndege visivyo na utaratibu wa kufanya ukaguzi wa kutosha.

Uwanja wa ndege Zanzibar ulipata alama ya chini kabisa ya nyota mbili kwenye tathmini ya afya na usalama iliyofanywa na Skytrax Wanaohakiki Hali ya Usalama katika Viwanja vya Ndege dhidi ya UVIKO-19, kipimo pekee cha uhakika kuthibitisha hatua zinazochukuliwa na mamlaka za viwanja vya ndege kuimarisha tahadhari wakati wa mlipuko wa ugonjwa huo. Kwa mujibu wa repoti hiyo ya Skytrax, “wagonjwa wapya wawili walioambukizwa aina mpya ya kirusi cha Afrika Kusini walithibitika kusafiri kuingia Denmaki mnamo Janurari 19, wakitokea Tanzania.”

Tamasha kubwa la muziki linalosubiriwa kwa hamu ambalo hufanyika mara moja kwa mwaka, Sauti za Busara, litafanyika katikati ya mwezi Februari visiwani Zanzibar, kwa hisani ya Umoja wa Ulaya nchini Tanzania na baadhi ya balozi za nchi za Ulaya zilizoko nchini Tanzania, wakati huu ambapo nchi inakabiliwa na hatari kubwa ya aina hiyo mpya ya kirusi wa Korona inayosambaa katika nchi za Uingereza, Afrika Kusini, na Brazil.

Mnamo Januari 24, Jimbo Kuu Katoliki la Arusha lilitoa waraka wa maonyo kwa waumini wake dhidi ya uwepo wa UVIKO-19 nchini Tanzania, na kuwaasa waumini wake kufuata tahadhari zote muhimu za afya  ili kujilinda na kusambaa kwa virusi hivyo makanisani.

Ingawa kumbukumbu zinaonesha kuwa Tanzania ina wangonjwa wachache ukilinganisha na nchi nyingine, ukimya wa serikali kuhusu takwimu za UVIKO-19 umeleta hali ya wasiwasi miongoni mwa wataalam wa afya na wanaharakati wa haki za binadamu, ambao  wamezuiwa kuzungumza na kuongelea UVIKO-19  katika majukwaa ya mitandaoni.

Nchi hiyo ilifanya marekebisho ya toleo la 2018 la Kanuni za Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta (Maudhui ya Mtandaoni mwezi Julai, ikizuia “maudhui yenye taarifa zinazohusiana na mlipuko wa ugonjwa hatari au unaoua nchini au kokote pale bila ruhusa ya mamlaka husika.”

Ingawa hatua za awali za kudhibiti maambukizi ya virusi zilichukuliwa, hivi sasa shule, vyuo, ofisi, na shughuli nyingine za kijamii zimerudi katika hali ya kawaida. Hata hivyo, virusi hivyo vinaendelea kusambaa nchini humo.

Rais John Magufuli ameonesha wasiwasi na ubora wa vifaa vya maabara na uaminifu wa watalaam wake baada ya majaribio ya siri kudaiwa kufanyika kwa kutumia mapapai na mbuzi kuleta majibu kuwa vilikuwa na maambukizi ya virusi hivyo. Rais alisema alisema kutoa takwimu hizi kulikuwa kunaleta tahayaruki isiyo na sababu na muda mfupi baadae, alimfukuza kazi Nyambura Moremi, mkurugenzi wa maabara ya afya ya taifa, kwa madai ya kuchakachua matokeo ya vipimo. Timu ya kushughulikia UVIKO-19 iliyoundwa na waziri nayo iliishia kuvunjwa.

Mwezi June, Magufuli alimshukuru Mungu kwa kumwondoa kirusi huyo  kutoka Tanzania, kufuatia siku tatu za maombi ya kitaifa. Alitoa tangazo hilo hadharani akiwa kwenye ibada ya Jumapili, katikati ya waumini waliokuwa wakimsifu, wakidai kuwa Mungu amejibu maombi yao. Magufuli aliwasifu waumini hao kwa kutokuvaa barakoa, pamoja na wito wa Shirika la Afya Duniani kuwaomba watu wavae barakoa kuzuia kuenea kwa virusi hivyo.

Magufuli, aliyepewa jina la utani la “bulldozer” kufuatia msimamo wake mkali dhidi ya vitendo vya ufisadi, alichaguliwa kwa mara ya pili mwezi Oktoba 2020 katika uchaguzi uliokosolewa sana kwa kuwabana wapinzani.

Kabla ya uchaguzi huo, Watanzania walishangazwa na kuzimwa kwa mitandao ambapo majukwaa yote makubwa ya mitandao ya kijamii ikiwa ni pamoja na Instagram, WhatsApp na Twitter yalifungwa yasipatikane. Mpaka leo, Watanzania wengi hawawezi kuingia kwenye mtandao wa Twita bila kutumia teknolojia ya kutumia mitandao ya siri yaani VPN.

Kwa zaidi ya miaka mitano, utawala wa Magufuli umebana mno uhuru wa demokrasia na shughuli za kiraia sambamba na kuminya uhuru wa kujieleza na haki ya kupata taarifa kwenye majukwaa ya kidijitali.

Kufuatia msimamo mkali wa serikali kukana uwepo wa UVIKO-19, Watanzania hawaruhusiwi kutoa takwimu zozote za UVIKO-19 ambazo serikali haijazihakiki, hii ikiwa na maana kwamba wananchi wa kawaida ikiwa ni pamoja na waandishi wa habari na wataalam wa afya wanazuiwa kutoa maoni kuhusu UVIKO-19 kwenye majukwaa ya kidijitali au kupata taarifa muhimu.

Haki ya kupata taarifa za UVIKO-19 imegeuka kuwa “upendeleo wa tabaka la watu fulani,” kwa mujibu wa daktari mmoja wa hospitali ya taifa aliyeongea na Global Voices kwa masharti ya kutokufahamika, akiogopa kufukuzwa kazi.

Tofauti na nchi nyingine zenye timu maalum zinazofanyia kazi taarifa za UVIKO-19, Tanzania ina tovuti yenye taarifa chache zilizopitwa na wakati kuhusu UVIKO-19.

Matamshi ya kukataa uwepo wa UVIKO-19 yanaonekana kukubalika na Watanzania wengi, ikiwa ni pamoja na wataalam wa afya, wanaopuuza hatua muhimu za kuchukua tahadharani kama kuvaa barakoa na kuepuka misongamano.

Global Voices ilitembelea hospitali kadhaa ikiwemo Muhimbili, hospitali ya rufaa ya serikali iliyoko jijini Dar es Salaam, mji mkuu wa kiutamaduni nchini humo, pamoja na Hospitali ya  Benjamin Mkapa jijini Dodoma, mji mkuu wa kisiasa, na kushuhudia tahadhari chache zikichukuliwa kukabiliana na kuenea kwa virusi vya ugonjwa wa korona.

Watu wanaruhusiwa kuingia kwenye maeneo ya hospitali bila kuvaa barakoa, kuna vifaa vichache vya usafi na kunawa mikono na vile vilivyopo havina maji au vimevunjika, hali iliyoshuhudiwa, kwa mfano, kwenye wodi ya wanawake wajawazito Muhimbili.

Wakati utawala wa Magufuli haujaonesha kujali madhara ya virusi hivi kwa maisha ya kila siku ya wananchi, mawaziri wengi wa serikali yake na idara zake wanakubali kwamba UVIKO-19 upo.

Waziri wa Fedha wa Tanzania awataka wafanyakazi wa Wizara yake kuchukua tahadhari zote kujilinda na virusi vya korona, wakati huo huo akisema Tanzania haisumbuliwi na UVIKO-19. Picha ya gazeti la Mwananchi.

Kwa mfano, Magufuli alipoapishwa kwa mara ya pili mwaka jana, mamlaka za serikali zilichukua tahadhari nyingi dhidi ya UVIKO-19, wakiwalazimisha wahudhuriaji wote kupima joto la mwili na kuosha mikono yao kwenye sehemu maalumu zenye maji na vipupushi.

Mnamo Januari 25, Waziri wa Fedha wa Tanzania, Dk. Philip Mpango  aliwataka watumishi wa wizara yake  kuchukua tahadhari dhidi ya UVIKO-19 na kwa wakati huo huo akikanusha kuwepo kwa ugonjwa huo nchini Tanzania, wakati wa mkutano wake jijini Dodoma, yalipo makao makuu ya kisiasa.

Wataalam wengi wa ndani wanaogopa kuzungumza,   kwa hofu ya kuchukuliwa hatua.

Global Voices ilizungumza na mtalaam mmoja wa afya aliyeamini kwamba Tanzania inaweza kuwa inakabiliwa na wimbi la pili ya mlipuko lakini akifikiri wananchi walifichwa taarifa hizi. Mtaalam huyo hakutaka kutajwa jina, akiogopa kuchukuliwa hatua.

Mtaalam mwingine wa afya aliiambia Global Voices kwa sharti ya kutokutajwa jina kwamba watu lazima wafahamu mwenendo wa hali ya UVIKO-19 ili waweze kuchukua tahadhari kujilinda na kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo kwa jamii zao. Alisema kwamba kuwaacha watu gizani kunafanya kazi yao iwe ngumu lakini aliamini kwamba Watanzania watajaribu kujilinda wenyewe kwa kuchukua tahadhari zote kama inavyoshauriwa na Shirika la Afya Duniani (WHO). Aliiambia Global Voices:

Politicians have taken over the whole COVID[-19] issue and they are playing a dangerous game, but when people will start dying they will start sacking medical staff.

Wanasiasa wameteka suala hili zima la UVIKO-19 na wanacheza mchezo hatari, lakini watu watakapoanza kufa wataanza kuwafukuza wafanyakazi wa afya.

Daktari mwingine aliyezungumza na Global Voices kwa sharti la kutokutaja jina lake alisema kwamba ingawa kuna matumaini ya kupata kinga, matamshi ya serikali ya Tanzania kukanusha uwepo wa ugonjwa huo yatakwamisha upatikanaji wake, kwa sababu serikali haijachukua hatua yoyote kuitafuta kwenye masoko ya dunia, na  badala yake kukimbilia tiba za mitishamba.

Mwezi Desemba 2020, Msemaji wa Waziri wa Afya Gerald Chamii alionesha mashaka yake kwa chanjo zinazopigiwa chapuo duniani, akiliambia jarida la East African:

It takes not less than six months to find a vaccine or cure for a certain disease. We have fared on our own since the pandemic spread, I am not sure if it is wise to have a vaccine imported and distributed to the citizens without undertaking clinical testing to approve if it is safe for our people.

Haichukui hata miezi sita kupata chanjo au tiba ya ugonjwa fulani. Tumejikwamisha wenyewe tangu mlipuko uanze, sina hakika kama ni busara kuingiza kinga hiyo na kuisambaza kwa wananchi bila kufanya majaribio ya kitabibu kuthibitisha usalama wake kwa watu wetu.

Kupata taarifa ni suala muhimu kwa demokrasia na maendeleo. Sheria za matumizi ya mtandao nchini Tanzania zimetumiwa vibaya zikilenga kunyamazisha sauti na wale wanaozungumza kupinga namna Tanzania inavyoshughulikia suala la UVIKO-19.

Uhuru wa kujieleza, ikiwa ni pamoja na haki ya kupata, kupokea, na kusambaza habari, imelindwa na sheria za kimataifa. Nchini Tanzania, haki ya kuhabarishwa, na kupata taarifa na kusambaza taarifa, inatambuliwa na Ibara 18(1) na 18(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hata hivyo, haki hizi zinaonekana kuwa nadharia zaidi kuliko uhalisia.

Katika hali ambayo serikali inakanusha uwepo wa UVIKO-19 na kuwepo kwa sheria zinazozuia watu kupeana taarifa na kutoa maoni kuhusu ugonjwa huu, mtandaoni na mtaani, Watanzania wanaachwa bila taarifa za msingi na wengi wanaogopa kuzungumza.


Makala haya ni sehemu ya mfululizo wa makala zinazochunguza kuingiliwa kwa haki za kidijitali wakati wa hatua za kuwafungia watu ndani kudhibiti kusambaa kwa UVIKO-19 katika nchi tisa za Afrika: Uganda, Zimbabwe, Msumbiji, Aljeria, Naijeria, Namibia, Tunisia, Tanzania na Ethiopia. Mradi huu umefadhiliwa na Mfuko wa Haki za Kidijitali Afrika unaendeshwa na Ushirikiano wa Sera za Kimataifa za TEHAMA kwa Afrika Mashariki na Kusiki mwa Bara la Afrika  (CIPESA).

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.