Kukifanya Kiswahili kionekane: Utambulisho, lugha na Mtandao

Mizizi ya miti iliyojikita kwenye ukuta wa karne ya 15 uliopo kisiwa cha Kilwa Kisiwani, Tanzania. Mnamo mwaka wa 1981, magofu ya sultani hodari wa Kiswahili kisiwani humo yalitangazwa kuwa eneo la UNESCO la urithi wa dunia. Picha na David Stanley, Januari 1, 2017, CC BY 2.0.

Kidokezo cha mhariri: Makala haya ya kibinafsi yaliandikwa kufuatia kampeni ya Twitter iliyoandaliwa na Global Voices Ukanda wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa ushirikiano wa Mradi wa Rising Voices pale kila wiki, mwanaharakati tofauti wa lugha alishiriki maoni yake kuhusu muingiliano wa haki za kidijitali na Lugha za Kiafrika kama sehemu ya mradi, “Matriki utambulisho: Tishio la ukandamizaji wa uhuru wa kujieleza mtandaoni barani Afrika.”

Kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), utofauti wa lugha na utamaduni una umuhimu kimkakati kwa watu ulimwenguni kote katika juhudi za kuimarisha umoja na mshikamano wa jamii.

Utofauti huu wa lugha na utamaduni ulishinikiza kongamano kuu la UNESCO kutangaza Siku ya Kimataifa ya Lugha ya Mama (IMLD) mnamo Novemba 1999, siku inayokumbukuwa mnamo Februari 21 kila mwaka. Kuimarisha IMLD, Umoja wa Mataifa (UN) ulitangaza Mwaka wa Kimataifa wa Lugha za Asili (IYIL 2019), ili kuzingatia hatari ya kuangamia kwa lugha za asili ulimwenguni.

Hivi leo, kuna zaidi ya lugha 7,100 zinazozungumzwa kote duniani,asilimia 28 yazo zikizungumzwa barani Afrika pekee. Licha ya hili, Kiingereza kinaongoza mtandaoni katika eneo hili. Miaka ishirini iliyopita, asilimia 80 ya maudhui ya dunia mtandaoni yalikuwa yanaegemea Kiingereza. Kwa sasa, hata hivyo, maudhui ya Kiingereza yanasemekana kupungua hadi kiwango cha kati ya asilimia 51 hadi 55.

Swala kizushi, kwa hivyo, ni: je, kupungua huku kunaashiria kuwa sasa watu wanapendelea lugha zao za asilia kuliko Kiingereza, ukizingatia kuwa ni chini ya asilimia 15 tu ya idadi ya watu duniani inayozungumza Kiingereza kama lugha yao ya kwanza?

Kiswahili: Ujio wa Uzao?

Kiswahili kinatambuliwa kama mojawapo wa lugha rasmi za Umoja wa Afrika (AU), kando na Kiiengereza, Kireno, Kifaransa, Kihispania na Kiarabu.
Kiswahili pia ni lugha ya matumizi mapana ya mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika mashariki (EAC).

Rwanda, taifa mwanachama wa EAC, kupitia bunge lake la chini, ilipitisha msuada wa kukifanya Kiswahili kuwa lugha rasmi mnamo 2017 – kando na Kinyarwanda, Kifaransa na Kiingereza. Licha ya kutumiwa kwa madhumuni ya utawala, Kiswahili kitajumuishwa kwenye mtaala wa elimu wa nchi hiyo.

Nchini Uganda, mnamo Septemba 2019, serikali iliidhinisha uanzishaji wa Baraza la Kitaifa la Kiswahili. Kifungu cha 6 (2) cha Katiba ya Uganda pia kimeelezea kuwa “Kiswahili kitakuwa lugha rasmi ya pili nchini Uganda na kitatumika katika mazingira kadri Bunge litakavyoweza kuagiza kwa sheria.”

Mnamo 2018, Afrika Kusini, nchi inayojivunia lugha rasmi 11, ilirasimisha Kiswahili kama somo la hiari katika mtaala wake, kuanzia mwaka wa 2020.
Mnamo mwaka wa 2019, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ilipitisha Kiswahili kama lugha rasmi ya nne ya Jumuiya hiyo.

Muonekano finyu wa Kiswahili Mtandaoni

Karibu Nairobi. Picha na Rachel Strohm, Septemba 20, 2019, (CC BY-ND 2.0)

Licha ya kuwa lugha ya Kiafrika inayozungumzwa sana, na takribani watu milioni 150 – haswa katika Afrika Mashariki, kanda ya maziwa makuu, kusini mwa Somalia, na maeneo mengine ya kusini mwa Afrika, muonekano wa Kiswahili mtandaoni ni finyu.

John Walubengo, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Multimedia cha Kenya, anachanganua kwenye makala yake katika Nation, jarida la kila siku nchini Kenya, kuwa ukosefu wa lugha na utamaduni mtandaoni unaunda “jamii yenye ‘mtazamo mdogo’ wa dunia.

Walubengo anaelezea kuwa tamaduni nyingi za kiasili huishia kusalimisha “utambulisho wao kwa ‘hali za Kiingereza’ za ufanyaji mambo.” Ukweli huu wa kusikitisha hata hivyo unaweza kubadilishwa tu iwapo jamii asilia “zitapigania kuhifadhi utambulisho wao mtandaoni na vile vile nje ya mtandao,” anasema.

Hata hivyo, yote si ya kutamausha. Kuna mashirika kadhaa yaliyojitolea katika mstari wa mbele kuendeleza na kukuza Kiswahili mtandaoni.

The Internet Corporation for Assigned Names and Numbers

(ICANN),  shirika la kimataifa lenye wadau wengi linaloratibu Mfumo wa Majina ya Mtandao(DNS), Anwani za Mtandao (IP) na nambari za mfumo huru, lilianzisha Majina ya Kikoa ya Kimataifa (IDNs), yanayowezesha watu kutumia majina ya kikoa katika lugha na maandishi ya kiasili.Kiuhakika, huundwa kwa kutumia herufi kutoka maandishi tofauti, kama vile Kiarabu, Kichina, au Kisiriliki.
Herufi hizi kisha husimbwa na kiwango cha Unicode na kutumiwa kama inavyoruhusiwa na vikoa vya IDN, seti ya viwango vilivyoainishwa na Bodi ya Usanifu wa Mtandao (IAB), na vikundi vyake vya kampuni ndogo; Tume ya Kazi ya Uhandisi wa Mtandao (IETF) na Tume ya Utafiti wa Mtandao (IRTF).

The Universal Acceptance Steering Group (UASG)

UASG ni jamii ya viongozi wa tasnia, inayohimiliwa na ICANN, ambayo huandaa jamii mtandaoni kwa watumiaji bilioni moja wafuatao wa mtandao.
Huku kunafanikishwa kupitia mchakato unaojulikana kama Ukubalikaji Ulimwenguni (UA), ambao huhakikisha kwamba programu na mifumo ya mtandao inashughulikia vikoa vyote vya viwango cha juu (TLDs) na barua pepe kulingana na vikoa hivyo kwa njia thabiti – pamoja na vile vilivyoko kwenye maandishi yasiyo ya Kilatini na vile ambavyo ni zaidi ya herufi tatu.
UA hutumikia wanamtandao ulimwenguni kote katika lugha zao asili na kwa majina ya vikoa ambayo yanatambulisha utamaduni wao. Kwa hivyo, kukuza mtandao wa lugha nyingi.

ICANNWiki
Shirika hili lisilo la kifaida linalotoa ukurasa wa wiki ulioendelezwa na jamii kwenye masuala ya ICANN na Utawala wa mtandao, kwa muda mrefu limeshirikiana na mashirika, taasisi za elimu na watu binafsi nchini Kenya na Tanzania. Huku kumewezesha Waafrika Mashariki kujenga, kutafsiri na kuongeza rasilimali za Wiki kwa maono yao, lugha na mtazamo.

Mradi huu wa Kiswahili – ambao mie kama mwandishi nimeweza kujihusisha nao rasmi – umeziba pengo la habari zinazohusiana na maswala ya Utawala wa Mtandao kwa kujanibisha maudhui ya ICANNWiki kukuza ushiriki katika jamii zinazolengwa.

Localization Lab

Localization Lab, ni jamii ya kimataifa yenye washiriki wa kujitolea wanaohimili utafsiri na ujanibishaji wa miongozo ya utumiaji na vifaa vya kidijitali vya usalama kama vile TOR, Signal, OONI, Psiphon.  Teknolojia hizi zinaangazia usalama, faragha, na ufichojina kwa kuhakikisha kuwa wanaharakati wa lugha za kiasilia wana nyugha salama za kufikia taarifa mtandaoni. Localization Lab imetafsiri zaidi ya vifaa 60 kwenye lugha 180 tofauti kote duniani,

Kondoa Community Network (KCN)

KCN mtandao jamii wa kwanza kufanyia majaribio teknolojia ya mawimbi ya Televisheni almaarufu TVWS, “teknolojia isiyounganisha na nyaya inayotumia mawimbi yasiyotumika ya redio yaliyopo ndani ya masafa ya mita bendi 470 hadi 790 MHz” kutatua changamoto ya uunganishwaji mtandaoni vijijini nchini Tanzania.

KCN inawafunza wanavijiji kuunda na kuwa wenyeji wa maudhui asilia yenye manufaa na muktadha wao.

Matogoro Jabhera, mwanzilishi wa KCN na mhadhiri msaidizi katika Chuo Kikuu cha Dodoma, Tanzania, aliliambia shirika la Global Voices kupitia simu ya Skype, kuwa anaamini maudhui asilia yanatoa motisha kwa “watu zaidi waliopo nje ya mtandao” kujiunga mtandaoni kwa sababu wanaweza wakaelewa “taarifa zao asili […] ikilinganishwa na hali ya sasa pale maudhui mengi yapo kwenye lugha ya Kiingereza.”

Watumiaji ‘bilioni wafuatao’ mtandaoni

Ulimwengu unatarajia kuwaunganisha “watumiaji bilioni wafuatao mtandaoni” na milioni 17 ya watumiaji hawa wanakadiriwa kuunganishwa mtandaoni wakitumia lugha kama utambulisho wao wa kidijitali.

Kwa hivyo, ukosekanaji wa maudhui asilia huenda ukawa na athari kubwa mno  ukizingatia ujumuishwaji kidijitali.
Bayana, huku kutaathiri haki za kidijitali – haswa, ufikiaji mtandao, haki ya kufikia maelezo mtandaoni, na haki ya kutumia lugha zao asilia kutengeneza, kushiriki, na kusambaza taarifa na maarifa kupitia mtandao.

Hivyo ni muhimu kuweka mikakati itakayoendeleza utengenezaji wa programu za TEHAMA na huduma, vile vile utumiaji wa lugha asilia, ili kuhakikisha ujumuishwaji wa kidijitali kwa wote.

Hatua hii, ikihimiliwa na juhudi zenginezo kama vile ujanibishaji wa vifaa vya kufunzia na kujifunzia, na mipango ya kusoma na kuandika ya TEHAMA vijijini, inaweza kuchochea mapinduzi ya kidijitali, na hivyo basi kukuza haki za kidijitali za watumizi wa mtandao na kuziba pengo la mgawanyiko wa kidijitali.

Hatimaye, mchakato huu utaharakisha ulindwaji, uheshimiwaji na ukuzaji “lugha zote za Kiafrika na lugha zingenezo ndogo mtandaoni” kama inavyoafikiwa katika kanuni za Azimio la Afrika la Haki za mtandao na Uhuru.

Mradi wa Mantiki Utambulisho umefadhiliwa na Mfuko wa Haki za Kidijitali Afrika  unaoendeshwa na shirika la Ushirikiano wa Sera za kimataifa za TEHAMA kwa ajili ya Afrika ya Mashariki na Kusini (CIPESA)

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.