Muswada wa Uhalifu wa Mtandaoni Unawapa Mamlaka Zaidi Polisi, Kuliko Wananchi

A young man using his

Kijana akiandika ujumbe wa maandishi kwa kutumia simu yake ya mkononi jijini Dar Es Salaam, Tanzania. Picha na Pernille Baerendtsen, imetumiwa kwa ruhusa.

Pernille Baerendtsen amechangia kuandika makala haya.

Mnamo Aprili 1, 2015, Bunge la Tanzania iipitisha muswada wa makosa ya mtandao unaojaribu kudhibiti picha za ngono kwa watoto, udhalilishaji wa mtandaoni, utengenezaji wa maudhui yenye mrengo wa ubaguzi wa rangi au chuki kwa wageni, kutuma ujumbe kwa mtu bila ridhaa yake, udukuzi wa mawasiliano na kuchapisha taarifa za uongo –vyote hivyo katika sheria moja.

Wakati wa kikao hicho cha bunge, miswada mingine miwili iliwasilishwa kwa mjadala: Muswada wa Upatikanaji wa Habari, Muswada wa Habari pamoja na Muswada wa Takwimu. Hata hivyo, muswada wa makosa ya mtandao ni mpya, na toleo lake lililowekwa mtandaoni (na si toleo lililofanyiwa marekebisho bungeni) lilisababisha mjadala mkali ndani ya muda mfupi.

Kama ilivyo kwenye nchi nyingine, makosa ya mtandaoni na uhalifu wa kifedha kwa hakika ni tishio la muda mrefu kwa Tanzania. Lakini muswada huu unashughulikia mambo mengi zaidi ya uhalifu huu. Na kwa sasa muswada huu umepitishwa na bunge pamoja na kukosolewa vikali na wanasiasa wa upinzani, wadau wa mitandao ya kijamii na wanaharakati wa haki za binadamu. Wakosoaji wakuu wa muswada huu kutoka kwenye asasi za kiraia wanasema wataipeleka serikali mahakamani kama rais atauidhinisha muswada huu kuwa sheria. Gazeti linalochapishwa nchini Tanzania, The Citizen, limebainisha maeneo kadhaa makuu kwenye muswada huo yatakayowaathiri watumiaji wa mtandao wa intaneti.

Katika uchambuzi uliofanywa na CIPESA, kikundi cha sera za teknolojia ya habari na mawasiliano, Mwandishi na mchambuzi wa Uganda Juliet Nanfuka anaandika kwamba lengo kuu la muswada huo wa makosa ya jinai linapaswa kuwa kulinda haki za raia wawapo mtandaoni. Badala yake, anasema, muswada huo unaonesha “kupuuza uhuru wa habari na kujieleza, [unatoa] mamlaka makubwa kwa polisi, na [kuchukua] ulinzi unaotarajiwa kwa wananchi wa kawaida.”

Muswada huu unazuia kuchapishwa kwa “taarifa zinazopotosha, zenye udanganyifu au zisizo na ukweli”, kipimo ambacho Nanfuka anasema kinaleta tishio la wazi kwa haki ya kujieleza kwa uhuru na uwazi mtandaoni. Muswada huo unawapa polisi mamlaka makubwa ya kupekua nyumba za watu wanaohisiwa kuvunja sheria hiyo, kukamata vifaa vyao vya kieletroniki, na hata kudai data zao kutoka kwa makampuni yanayotoa huduma za mtandao. Aidan Eyakuze na Ben Taylor, wote wawili wakifanya kazi kwenye asasi huru inayofanya kazi zake Afrika Mashariki iitwayo Twaweza, walikuwa na hoja kwamba muswada huo unatoa nguvu nyingi mno kwa polisi bila namna nzuri ya kuwadhibiti:

…muswada unampa mamlaka hata afisa mdogo kabisa wa polisi kupekua na/au kumnyang’anya raia kifaa cha kompyuta au data, ikiwa ni pamoja na maudhui ya ujumbe, bila sababu au usimamizi unaoeleweka. Hii ni pamoja na kudai taarifa za mtumiaji kutoka kwenye makampuni yanayotoa huduma za intaneti na mitandao ya simu za mkononi.

Mwanablogu wa ki-TanzaniaThinklessactmore alibainisha kwamba polisi wanaweza kutumia sheria hii “kuwabughudhi wanaharakati wa mtandaoni kwa kisingizio cha kuwa na mashaka na udhalilishaji wa mtandaoni bila kufuata utaratibu wa kisheria.” Mtumiaji wa mtandao wa Twita Sultan Rajab, ambaye ni mshauri mwelekezi wa masuala ya kodi na kifedha nchini Tanzania, alisema alifikiri muswada ni mzuri, lakini alikuwa na wasiwasi na mamlaka waliyopewa polisi:

@JMakamba it is a good bill/law. I am worried about the power given to our police. Ignorant & low income earners might suffer.

— Sultan Rajab (@SultanKipupwe) April 1, 2015

Ni muswada/sheria nzuri. Nina wasiwasi na mamlaka waliyopewa polisi. Wananchi wasio na elimu na wenye kipato kidogo wanaweza kupata msukosuko mkubwa.

Muswada huu pia unaeleza kwamba kutuma taarifa “bila idhini ya anayetumiwa” kwa njia za kieletroniki ni kosa la jinai. Wakati kipengele hiki kikikusudia kudhibiti vitendo vya usambazaji wa ujumbe wenye madhara kwa anayeupokea, bado kinaweza kutafsiriwa kwa upana. Maria Sarungi Tsehai, mtaalam wa mawasiliano na muasisi wa taasisi ya Change Tanzania [Mabadiliko Tanzania], aliuliza:

@jpb4rretto: @MariaSTsehai How is any message transmitted with solicitation? Call me and ask me to write you and email? #CyberCrimeBill

— Maria Sarungi Tsehai (@MariaSTsehai) April 2, 2015

Inawezekanaje ujumbe wowote kutumwa kwa idhini ya anayeupokea? Kwa kunipigia na kuniomba nikuandikie barua pepe?

Muswada wa makosa ya mtandaoni unahusiana na miswada mipya iliyotajwa awali ya Upatikanaji wa Habari, Sheria ya Habari, na Takwimu– yote ikiwa na uwezekano wa kuwa na madhara makubwa kwenye uhuru wa habari nchini Tanzania. Lakini tofauti na Muswada wa Makosa ya Mtandaoni, miswada hiyo mitatu haikuonekana hadharani katika matoleo yao ya hivi sasa.

Wachambuzi kwenye mitandao ya kijamii na waandishi wa habari wanajadiliana namna gani wanafikiri serikali inaweza kuwa na maslahi fulani kwa kuzuia miswada hii isionekane hadharani, wakati huo huo ikiharakisha mchakato. Baadhi wanahoji ikiwa ni kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi utakaofanyika mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka huu nchini Tanzania. Chama kinachotawala nchini Tanzania, Chama cha Mapinduzii (CCM), kwa miaka kadhaa iliyopita kimekuwa kikipata ushindani unaoendelea kukua siku kwa siku kutoka kwenye vyama vya Upinzani nchini humo. Wakati huo huo, waandishi wa habari na vyombo vya habari vimekuwa vikipata misukosuko na kutishwa.

Wakiandika kwenye blogu ya Washington Post, Keith Weghorst na Ruth Carlitz wanadhani kwamba kuharakishwa kwa miswada hiyo “kunaendana na tabia ya chama hicho kinachotawala ya kutaka kung’ang’ania madaraka kwa gharama yoyote.” [Waandishi hao] wanaandika, “kadri serikali inavyodhoofisha uhalali wa mashambulizi ya upinzani –kwa kuhodhi upatikanaji wa taarifa za umma –ndivyo inavyokuwa kwenye nafasi nzuri ya kuzuia kashfa na utendaji duni zisiwadhuru kwenye uchaguzi.”

Thinklessandactmore alifurahishwa kwamba Tanzania imetambua uhitaji wa kudhibiti matumizi ya mtandao, lakini akasema muswada huo uliwahishwa mno kupelekwa bungeni:

Ni muhimu kuwa na sheria ambayo itadhibiti shughuli za mtandaoni na watumiaji wa mtandao wa intaneti lakini hilo lifanyike kwa namna sahihi. Hakuna uharaka wa kuw ana sheria hiyo; haikuwepo kwa miaka 53 tangu tupate uhuru. Kama itachukua mwaka au miaka miwili kuwa na sheria bora ya makosa ya mtandaoni, iwe hivyo. Tufanye utafiti wa kutosha kuhusu suala hili; tukusanye maoni tofauti kabla ya kupeleka muswada huo bungeni.

Lwanda Magere, injia wa program za kompyuta, aliwatuhumu waandishi wa muswada huo kutumia mbinu ya “kunukuu bila marekebisho”:

Cyber Crime Bill Tanzania: copied and pasted, almost zero ability to implement.

— Lwanda Magere (@nndekindo) April 7, 2015

Muswada wa Makosa ya Mtandaoni Tanzania: Umenukuliwa mahali bila marekebisho yoyote, hivyo hakuna uwezekano wa kutekelezeka

Mwanablogu wa Tanzania PATO kwa utani alituma picha inayowaonesha wabunge kadhaa waliopitisha muswada huo:

These are your MPs that passed the #CyberCrimeBill y'day! Vote wisely in October fellas! pic.twitter.com/pEScSHYYPZ

— PATO♠️ (@PatNanyaro) April 2, 2015

Hawa ndio wabunge wenu waliopitisha Muswada wa Makosa ya Mtandaoni jana! Pigeni kura kwa busara mwezi Oktoba jamani!

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.