Ajong Mbapndah wa Pan African Vision anazungumza na Gershom Ndhlovu kuhusu siasa zinazozunguka ugonjwa na kifo cha Rais wa Zambia Michael Sata:
Rais Michael Sata siku za hivi karibuni amefariki dunia jijini London na inaonekana afya yake na huduma za tiba alizopatiwa ziligobikwa na usiri, kwa nini wananchi wa Zambia hawakupewa taarifa za kuzorota kwa afya ya Rais?
[Gershom Ndhlovu]: Tovuti ya habari, Zambian Watchdog, iliwajulisha wananchi kuhusiana na kuzorota kwa afya ya rais Michael Sata kwa zaidi ya miaka miwili kabla ya kifo chake. Tovuti hiyo hiyo iliweza kuweka wazi matibabu ya siri aliyokuwa akipatiwa [rais] huko ughaibuni. Maafisa waandamizi wa serikali na makada wa chama tawala hawakufurahishwa na habari hizo zilizokuwa zikifuatilia kwa makini na kuweka wazi hali ya Mhe Sata na kulikuwa na majaribio mengi ya kuifungia tovuti hiyo ambayo kwa nyakati kadhaa ilizuiwa kuifanya isipatikane kwa wasomaji wanaoishi Zambia.
Kuhusu swali la kwa nini ilikuwa hivyo, ni dhahiri serikali na chama tawala kilitaka kuonesha kwamba Rais alikuwa yu na afya njema na akiendelea na kazi zake. Huenda hawakutaka kukiri ukweli kwa sababu katiba inataka kuondolewa madarakani kwa kiongozi, ikithibitishwa na baraza la madaktari kwa ombi la baraza la mawaziri, kwamba afya yake ina matatizo. Kwa hakika, raia mmoja alijaribu kulishinikiza Baraza la Mawaziri liitake bodi ya madaktari kuchunguza afya ya rais kupitia Mahakama Kuu lakini ombi lake lilitupiliwa mbali.