Gambia Yajitoa Jumuiya ya Madola, Yaiita Jumuiya Hiyo ‘Ukoloni Mambo-Leo’

President of the Gambia Yahya Jammeh addresses United Nations General Assembly on 24 September, 2013. UN photo by Erin Siegal. Used under Creative Commons license BY-NC-ND 2.0.

Rais wa Gambia Yahya Jammeh akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Septemba 24, 2013. Katika hotuba yake, alilaani ushoga, akiuita “tishio kuu la kuwepo kwa binadamu”. Picha ya UN na Erin Siegal. Imetumiwa kwa Leseni ya Creative Commons BY-NC-ND 2.0.

Gambia, Nchi ndogo ya Afrika Magharibi imetangaza kupitia kituo cha runinga cha taifa kwamba imejitoa kwenye Jumuiya ya Madola, ushirikiano wa nchi zipatazo 54 zilizowahi kuwa makoloni ya Ufalme wa Uingereza.

Tamko lililotolewa Jumatano, Oktoba 2, 2013 limesema kwamba “serikali imesitisha uanachama wake wa Jumuiya ya Madola na kuamua kwamba Gambia kamwe haitakuwa mwanachama wa taasisi yoyote ya ukoloni mambo-leo na kamwe haitakuwa sehemu ya taaisis yoyote inayotanua ukoloni.”

Hakuna sababu nyingine zaidi zilizotolewa na serikali, ila ni wazi kuwa mahusiano kati ya Gambia na Uingereza mwaka 2013 yamekuwa magumu. Mwezi Aprili, Ripoti ya mwaka ya Haki za Binadamu na Demokrasia ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza ilikosoa rekodi ya haki za binadamu nchini humo chini ya Rais Yahya Jammeh, ikionyesha ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu ikiwa ni pamoja na ukamataji wa raia usiofuata sheria, kufungwa kwa magazeti kinyume cha sheria na unyanyasaji wa makundi madogo. Majibu ya nchi hiyo kwa ripoti hiyo yalikuwa makali: “Uingereza haina uhalali wa kimaadili kufundisha maadili ya haki na demokrasia kwa nchi yoyote iliwahi kuwa koloni lake barani Afrika”.

Baada ya Gambia kutangaza uamuzi wa kufutilia mbali uanachama wake wa chombo hicho cha kimataifa kinachoongozwa na Queen Elizabeth II, watumiaji wa mtandao duniani kote wameitikia uamuzi huo kwa hisia tofauti.

Mathew Jallow, mwandishi wa habari raia wa Gambia aliyefukuzwa nchini humo, aliichukulia hatua hiyo kuwa nzuri kuutangaza “ujinga” wa Rais Jammeh. Jammeh, alitwaa madaraka kwa mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 1994, kwa miaka mingi amekuwa akichukiwa na dunia kwa utawala wake wa kikandamizaji, utawala ambao umejaa mauaji, kubanwa kwa uhuru wa habari na maoni, kuuawa kwa mashoga, ukandamizaji mkubwa wa wapinzani wa kisiasa:

Nyuma ya kila wingu zito jeusi, pana utepe mwembamba wa shaba. Kujitoa kwa Gambia ya Yahya Jammeh kutoka Jumuiya ya Madola inatosha kuwa habari hasi kwa mwaka mzima wa taarifa za magazeti. Leo, kila nchi duniani itajua habari hizi za kujitoa na kila nchi mwanachama wa Jumuiya ya Madola, ikiwa ni pamoja na Marekani, itathibitishiwa wasiwasi wowote kuhusiana na madai yetu. Hili ndilo linalofanywa na madikteta siku zote. Hujichimbia makaburi yao wenyewe katika harakati za kuimarisha tawala zao na kujididimiza ndani ya tawala zao zinazoharibikiwa. Asante Yahya Jammeh. Jitihada zetu zisingetangaza ujinga wako vizuri zaidi ya ulivyofanya mwenyewe.

Akitoa maoni katika ukurasa wake wa mtandao wa Facebook, mwandishi wa Gambia Sainey MK Marena alichambua hali ilivyo (bandiko lake limetumiwa kwa ruhusa):

Kujitoa kwa Gambia kutoka Jumuiya ya Madola kunavutia vichwa vya habari za kimataifa. Swali kuu ni kwa nini tunajitoa kwenye Jumuiya ya madola wakati ambapo nchi kama Msumbiji na nyinginezo zinatamani kujiunga na chombo hicho. Gambia imekuwa na inaendela kufaidika na Jumuiya ya Mdola katika maeneo mengi ikiwa ni pamoja na elimu/ufadhili, michezo na hivi karibuni Jumuiya hiyo ilipendekeza kuundwa kwa Tume ya Taifa ya Haki za Binadamu. Mantiki yangu ni kwamba Gambia kama taifa lingine lolote ina haki ya kijitoa kutoka kwenye umoja au shirika lolote lakini iwe hivyo kwa sababu zenye uzito na za kweli. Mwaka 2003, Zimbabwe chini ya Mugabe ilijitoa kwneye Jumuiya hiyo kwa sababu wanazozijua wao lakini nchi ndogo kuliko zote barani Afrika ingechukua hatua kwa mwelekeo tofauti.

Hata hivyo, Sefa-Nyarko Clement alionekana kutokukubaliana, akaandika kwenye mtandao wa Facebook:

Hatua nzuri, Gambia. Ingawa siungi mkono vitendo vya mauaji na sera mbovu za Baba Jammeh, ninaunga mkono kujitoa kwake kutoka Jumuiya ya Madola. Kwa hakika, Jumuiya ya Madola imepoteza umuhimu wake.

Kwenye mtandao wa twita, mtumiaji Abdou ‏(@abs2ray) alikosoa tabia ya rais:

Kimsingi siko kinyume na kitendo cha Gambia kujitoa kwenye Jumuiya ya Madola lakini kama kawaida Yahya haonyeshi mwelekeo kwa mara nyingine.

Wakati majadiliano juu ya mahusiano duni ya Jammeh kidiplomasia yakiendelea, bado si bayana kile ambacho nchi hiyo masikini sana itakifaidi kwa kujitoa kwenye Jumuiya ya Madola.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.