Siku ya Ada Lovelace: Kuwapongeza Wanawake Wanajishughulisha Kupigania Teknolojia na Uwazi Ulimwenguni

Wazo hili likiwa linashajiishwa na makala ya Ellen Miller iliyotoka katika blogu ya Sunlight Foundation, ambayo inaelezea kazi za wanawake wanaotumia teknolojia ili kuhamasisha uwazi huko Marekani. Kwa hiyo tuliamua kuongeza kwenye orodha hiyo kwa kuwaelezea wanawake kadhaa kutoka sehemu mbalimbali ulimwenguni wanaotumia teknolojia kuzishinikiza serikali kuwa wazi na zinazowajibika zaidi. Maelezo yafuatayo yaliandikwa na kutafitiwa na Renata Avila, ambaye ni kiongozi wa Creative Commons huko Guatemala, pia ni Mkurugenzi wa Primer Palabra, na ni mtafiti wetu wa lugha ya Kihispania huko Latini Amerika kuhusu Mtandao wa Teknolojia wa Kutetea Uwazi.

Huko Meksiko, Irma Eréndida Sandoval, anaongoza maabara ya kuhifadhi nyaraka juu ya ufisadi na kutafiti kuhusu sera zilizo bora zaidi za uwazi. “Laboratorio de Documentación y Análisis de la Corrupción y la Transparencia” katika UNAM, the Autonomous National Mexican University, ni moja ya taasisi zinazoheshimika sana katika Latini Amerika.

Kule Iceland, mbunge Birgitta Jónsdóttir anapigia chapuo Vuguvugu linalojulikana kama Icelandic Modern Media Initiative, ambalo ni pendekezo la mbingu iliyo salama wa ajili ya uandishi wa habari za upelelezi nchini humo, jambo ambalo anaamini kuwa litakuza uhuru wa kujieleza na uwazi ulimwenguni kote kwa kutoa kinga kwa makundi yanayopigia kelele maovu na wanaojitolea kuanika maovu hasa kinga dhidi ya vikwazo vya kudaiwa fidia.

Ni muhimu siyo tu kupitisha sheria nzuri ili kuhamasisha uwazi na uwekaji bayana wa mambo bali pia kukinga nchi iliyo huru isije ikawa isiyoonekana sana. Mwanaharakati kutoka Ujerumani, Franziska Heine, alianzisha upigiaji debe unaofikiriwa kuwa wenye mafanikio zaidi katika historia ya Ujerumani, na huo ulikuwa na lengo la kuzuia sheria ambayo ingewapa askari polisi wa Ujerumani haki ya kutengeneza na kutunza orodha ya vikwazo hasa kuhusu tovuti ambazo zingezuiliwa na Makampuni ya Kijerumani ya Kutoa Huduma za Intaneti. Upigiaji debe huo ulitiwa saini zaidi ya mara 134,000. Franziska ni sehemu ya vuguvugu linalopinga ubanaji wa vyombo vya habari na anajishughulisha na mambo mbalimbali na asasi mbalimbalizinazopambana na ufuatiliaji, upekenyuzi, ubanaji katika kupeana habari ambavyo vyote vinatishia haki za kiraia.

Lakini sheria nzuri na raia wanaojituma kudai haki zao bado havitoshi; nyenzo pia ni muhimu ili kuwawezesha wanawake sehemu mbalimbali duniani kuchukua hatua ili kuhamasisha uwazi. Margarita Padilla, ambaye ni mhandishi katika masuala ya Teknolojia ya Habari (IT) na ambaye aliwahi kuwa mkurugenzi wa jarida la Mundo Linux anajaribu kuleta tofauti. Yeye hubuni na kuendeleza mifumo iliyo na mkabala wa kijamii na pia huhamasisha uwekaji bayana wa mambo katika tovuti yake ya Sin Dominio.

Mercedes de Freitas
wa kutoka Venezuela ni Mkurugenzi Mkuu wa Transparencia Venezuela, ambayo ni tawi la taasisi ya Kimataifa ya Uwazi, Transparency International, na pia alipata kuwa mwanachama wa Ashoka Changemaker kutokana na kazi yake ya kuhamasisha ushiriki wa kiraia na kukuza uwajibikaji wa serikali.

Hii ni mifano michache tu ya wanawake duniani wanaotumia teknolojia ili kupambana na ufisadi, kukuza utendaji wa taasisi, na kutengeneza sera bora zaidi za kuwahusisha raia na papo hapo kuwafanya watendaji wa serikali kuwajibika. Kama ambavyo makala ya hivi karibuni ya Alexandra Starr inavyoeleza, maeneo yote haya mawili ya teknolojia na serikali yamewatenga wanawake katika ushiriki pamoja na ukweli kwamba wamekuwa na rekodi nzuri ya kushughulikia sera na teknolojia kwa njia iliyo yakinifu zaidi na kwa mbinu za hali ya juu kuliko wanaume walio wengi.

Kampuni za utengenezaji mifumo inayoendesha kompyuta na majengo ya mabunge sehemu mbalimbali duniani bado yanatawaliwa na wanaume, lakini jambo hili sasa linabadilika kwa kasi kubwa, yote ni kwa sababu ya kizazi kipya cha wanawake wanateknolojia, wanaharakati na wanasiasa. Sitakuwa nimetenda haki kama sitataja kazi za watafiti wetu wa kike na watafiti wakosoaji ambao, hatuna budi kusema, wamejidhibitisha kuwa wachapa kazi hodari miongoni mwa wanachama wa timu yetu ya Mtandao wa Teknolojia wa Kutetea Uwazi.

Renata Avila, ambaye ndiye aliyeandika taarifa/maelezo ya wanawake wote hao hapo juu, yeye ni mwanasheria, mwanaharakati wa haki za binadamu, kiongozi wa Creative Commons huko Guatemala, na mkurugenzi wa Primer Palabra. Amewahi kufanya kazi na Taasisi ya Rigoberta Menchu Tum, Chuo Kikuu cha Harvard, Sauti ya Umma (the Public Voice), na Wanawake katika Usalama wa Kimataifa (Women in International Security). Unaweza kumpata katika Twita: @avilarenata.

Sopheap Chak ni mhitimu wa masomo ya amani katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Japan. Kwa sasa hivi anaongoza Mtandao wa Vijana wa Kikambodia wa Mabadiliko (the Cambodian Youth Network for Change), ambao umeundwa na wanaharakati vijana nchini humo. Hapo kabla alikuwa ni ofisa utetezi wa Kituo cha Haki za Binadamu nchini Kambodia (CCHR) ambapo alisaidia kuongoza kile kilichojulikana kama “Black Box Campaign” yaani Kampeni ya Boksi Jeusi, lengo likiwa ni kupambana na ufisadi ndani ya jeshi la polisi nchini Kambodia. Anapatikana kwa Twita: @jusminesophia.

Rebekah Heacock ambaye hivi sasa anafanya masomo ya shahada ya uzamiri katika Chuo Kikuu cha Columbia kinachoshughulika na Masuala ya Kimataifa na ya Umma, yeye pale anasoma uhusiano kati ya masuala ya Taarifa, Mawasiliano na Teknolojia (ICT) na maendeleo. Yeye pia huhakiki blogu ya Chuo Hicho cha SIPA, inayojulikana kwa jina la The Morningside Post. Aliwaji kuishi na kufanya kazi nchini Uganda, Afrika ya Mashariki, ambapo wa kushirikiana na mtu mwingine aliandaa na kuongoza mfululizo wa makongamano kuhusu maendeleo baada ya vita kwa ajili ya wanafunzi wa vyuo vya Marekani na Afrika. Anapatikana kwa Twita: @rebekahredux.

Manuella Maia Ribeiro
ni mhitimu wa hivi karibuni kutoka Chuo Kikuu cha São Paulo alikosoma Menejimenti ya Sera ya Umma. Tangu mwaka 2007 amekuwa akitafiti jinsi serikali zinavyohamasisha uwazi, uwajibikaji na ushrikishaji kwa kupitia teknolojia za habari na mawasiliano. Anapatikana katika Twita: @manuellamr.

Namita Singh
ni mtafiti na mshauri anayechunguza vyombo vya habari shirikishi. Alisomea vyombo vya habari na mawasiliano ya umma katika Chuo Kikuu cha Delhi na ana shahada ya Uzamiri katika Sanaa kuhusu Sayansi ya Jamii kutoka katika Taasisi ya Tata inayotoa Sayansi ya Jamii huko Mumbai. Namita anatarajia kuanza masomo yake ya Shahada ya Uzamivu (Ph.D) ya Utafiti huko Uingereza kuhusu michakato na taathira ya video shirikishi. Anapatikana kwa Twita: @namitasingh.

Carrie Yang
ni mwanafunzi aliyefanya masomo ya baada ya shahada ya kwanza kuhusu vyombo vya habari vipya katika Chuo Kikuu cha Kichina cha Hong Kong. Mwelekeo wa utafiti wake uko katika uandishi wa habari wa kiraia na maendeleo ya vyombo vipya vya habari. Alisoma somo la Kiingereza katika Chuo Kikuu cha Guangdong ambacho ni Chuo cha Mambo Ya Nje huko Guangzhou, China. Anapatikan kupitia Twita: @Carrie_Young.

Sylwia Presley ni mwanablogu, mpiga picha na mwanaharakati anayependelea kufuatilia utafuatji masoko wa vyombo vya habari vya kijamii ambavyo kwa ajili ya sekta zisizo za kutengeneza faida na vyombo vya habari vya kijamii kwa ajili ya kuleta mabadiliko katika jamii. Amewahi kuandaa matukio mbalimbali likiwemo lile la BarCamp Transparency huko Uingereza majira ya joto yaliyopita kule Oxford, ambapo ana matumaini kwamba jambo hilo litafanywa katika nchi mbalimbali za Ulaya msimu wa joto wa mwaka huu. Anapatikana katika Twita: @presleysylwia.

Aparna Ray kwa taaluma yeye ni mshauri anayejitegemea kuhusu utafiti yakinifu na anapenda sana kujifunza kuhusu watu, tamaduni, jamii na vyombo vya habari vya kijamii pamoja na mifumo ya kompyuta ya kijamii. Anaandika katika Kiingereza na KiBangla (hiyo ya pili ikiwa ndiyo lugha aliyozaliwa nayo), na kwa hiyo hushughulikia makala za KiBangla katika Global Voices. Anapatikan kwa njia ya Twita: @aparnaray.

Laura Vidal
ni raia wa Venezuelea anayesomea Elimu ya Sayansi huko Parisi, Ufaransa. Yeye huendesha blogu inayoitwa Sacando la Lengua inayohusu lugha, fasihi na miingiliano ya watu katika Jamii, na anaamini kabisa kwamba kila utamaduni ni wa pekee na ni muhimu sana, na kwamba tukijifunza tamaduni hizo tunapata kujiona wenyewe vizuri zaidi.

Je, unawafahamu wanawake wengine wanaofanya kazi katika maeneo ya teknolojia na uwazi? Tafadhali tuunganishe na tovuti zao, blogu, na anwani zao za Twita kupitia sehemu iliyo hapa chini!

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.