Sisi ni Sauti za Dunia: Miaka Mitano Baadaye

Ifuatayo ni ya kwanza katika mlolongo wa makala zinazounga mkono kampeni ya kuchangisha fedha kwenye mtandao ili kutunishamfuko wa Global Voices mwaka 2009-10. Kama unapenda kuunga mkono kazi yetu, tafadhali tembelea ukurasa wetu wa Michango. Ahsante!
—-
Mkurugenzi wa Sauti Zinazokua, David Sasaki ameandika kumbukumbu ya kuvutia kwa ajili ya siku ya kuadhimisha miaka mitano ya Global Voices. Miaka mitano iliyopita mwezi huu, David alisafiri katika Marekani kuanzia California mpaka Havard kwa ajili ya warsha ya siku nzima kuhusu kublogu ulimwenguni. Warsha hiyo – zaidi kidogo ya wasaa wa kushirikiana mawazo – iliitwa “Sauti za Dunia Kwenye Wavuti.” Tovuti unayoisoma leo ilianza kama blogu ambayo Ethan Zuckerman na mimi tuliitengeneza ili kuandaa warsha hiyo. Lengo letu, tukiliweka kirahisi, lilikuwa kujadili jinsi ya “kutumia kublogu na zana za kublogu ili kuwasaidia watu katika nchi tofauti kufanya mazungumzo yenye maana na ya moja kwa moja baina yao.” Majadiliano ya siku hiyo yalikuwa ni sehemu ya kongamano kubwa la Wavuti na Jamii lililoandaliwa na Kituo cha Berkman cha Wavuti na Jamii chuoni Harvard. Taasisi ya Jamii Wazi kwa ukarimu ilitufadhili fedha kiasi ili kuwasafirisha wanablogu kutoka sehemu mbalimbali duniani. Tulilitangaza tukio hilo kwenye wavuti, na wengine wengi – kama David – walijitokeza. Tunashukuru.

Hii ni makala niliyoiandika mara baada ya mkutano. Hii ni posti ya blogu ya Ethan “siku iliyofuata.” Hatukutoka na mpango mahsusi wa kuitawala dunia – au hata mradi thabiti. Washiriki walikubaliana kuanzisha ukurasa wa ushirika katika wavuti ili kushirikiana habari, pamoja na Mazungumzo ya Maandishi Kwenye Wavuti (Internet Relay Chat (IRC) kwa ajili ya mikutano mingine kwenye wavuti, pamoja na kikusanya blogu kitakachoendeshwa na washiriki wa kongamano pamoja na wengine kama wao ambao tulianza kuwaita “wanablogu kiungo.” Hatukuwa na hakika tungeelekea wapi baada ya pale.

Jambo moja, hata hivyo, lilikuwa wazi: umma amuzi wa wanablogu wenye maadili yanayofanana na yetu ulikuwa unaanza kujitokeza duniani kote. Ilionekana kama ni wazo zuri “kuunganisha nukta zote” (kama Jeff Ooi anavyosema) baina ya watu hawa na kuunda jukwaa linalotokana na jamii hii inayokua. Katika majuma yaliyofuata baada ya kongamano, baadhi ya washiriki walitumia ukurasa wa ushirika kwenye wavuti ili kuyaweka maadili ya jamii hii. Matokeo yake yalikuwa ni Ilani ya Global Voices. Ni muhimu kuiweka (Ilani hiyo) tena hapa katika ujumla wake kwani kila kitu ambacho Global Voices inakifanya leo hii kinaendelea kuendeshwa na maadili hayo ya msingi:

Tunaamini katika uhuru wa kujieleza: katika kulinda haki ya kutoa kauli – na haki ya kusikiliza. Tunaamini katika upati huru wa nyenzo za kujieleza.

Ili kufanikisha hilo, tanataka kumwezesha kila mmoja ambaye anataka kujieleza kuwa na njia za kujieleza – na kila mmoja anayetaka kusikiliza, awe na njia za kusikiliza.
Shukrani kwa nyezo mpya, kauli hazihitaji kudhibitiwa na wale wanaomiliki njia za uchapishaji na usambazaji, au na serikali ambazo zinaweza kudhibiti fikra na mawasiliano.

Hivi sasa, mtu yeyote anaweza kuwa na nguvu za vyombo vya habari. Kila mtu anaweza kusimulia simulizi yake kwa dunia.

Tunataka kujenga madaraja katika mabonde yanayotenganisha watu, ili kwamba tuweze kuelewana zaidi. Tanataka kufanya kazi kwa ufanisi zaidi, na kutenda kwa nguvu zaidi.

Tunaamini katika nguvu ya kukutana moja kwa moja. Mshikamano kati ya watu kutoka dunia tofauti niwa kibinafsi, kisiasa na wenye nguvu. Tunaamini kuwa maongezi yanashinda mipaka ni muhimu kwa mustakabali ambo ni huru, wa haki, wenye kuneemesha na endelevu – kwa raia wote wa dunia hii.

Huku tukiendelea kufanya kazi na kuongea kama watu binafsi, pia tunataka kutambua na kukuza malengo na maslahi tunayoshirikiana pamoja. Tunaahidi kuheshimu, kusaidia, kufundisha, kujifunza na kusikiliza kutoka kwa kila mmoja wetu.

Sisi ni Sauti za Dunia.

Hivi sasa tuna timu ya watu wa mataifa mbalimbali ambao wanashika nafasi kama wasimamizi wa sehemu mbalimbali za Global Voices. Lakini roho ya ya GV ni mamia ya watu wanaojitolea ambao wanatenga muda kutoka kwenye kazi zao, masomo, na majukumu ya kifamilia ili kusaidia kujenga majadiliano ya umma wa dunia yaliyo huru zaidi na shirikishi.

Wanachama wa jamii ya Global Voices katika Mkutano wa Delhi India, mwaka 2006. Picha na Jace.

Wanachama wa jamii ya Global Voices katika Mkutano wa Delhi India, mwaka 2006. Picha na Jace.

Habari ya kina ya jinsi Global Voices ilivyokua na jinsi matawi yake tofauti yanavyofanya kazi – kujumuisha Sauti Zinazokua, Idara ya Utetezi ya Global Voices pamoja na Idara ya Lugha ya Global Voices – inaweza kupatikana kwenye sehemu nyingi, pamoja na sehemu Kuhusu ya tovuti hii na ile ya Maswali Yanayolizwa Kila Mara (FAQ). Habari kuhusu mradi huu zipo hapa. Tangu mwaka 2004 tumekuwa na mikutano inayokutanisha watu mjini London (2005), Delhi (2006) na Budapest (2008). Tunatazamia kuwa na mkutano mwingine mwaka 2010 (mahali na tarehe vitatangazwa hivi karibuni).

Mwaka 2006 mimi na Ethan tuliandika makala kwa ajili ya jarida la Nieman Reports ambamo tulitaka kuelezea uhusiano kati ya Global Voices na uanahabari. David anayo makala nyingine nzuri sana inayohusu kwa nini shughuli za kivuko, utetezi na ufasiri ni muhimukatika kuwasaidia watu kuvishinda vikwazo vya kuongea, kisikilizwa, na kuwasikiliza wengine.

Watu wengi duniani wanakerwa kwa kuwa vyombo vya habari vikuu vya kiingereza duniani havitilii maanani nchi zao kwa muda mrefu, na kuandika tu habari mbaya kuhusu nchi zao, au vyombo hivyo huendeleza tu imani potofu kuwahusu. Wanaiona GV kama jukwaa la thamani ambalo wanaweza kukuza simulizi na mitazamo yao kwa hadhira pana zaidi duniani. Wengine wanakereka na kwamba vyombo vya habari vya ndani ya nchi zao vinashindwa kuripoti juu ya sehemu nyingi za dunia, wanafanya vibaya, au wanaripoti katika namna iliyopinda ambayo inaunga mkono mtazamo wa dunia wa serikali zao, na hivyo wanaamini kuwa kwa kutafsiri maudhui ya GV katika lugha zao za nyumbani wanaweza kuboresha ufahamu wa dunia wa jamii zao. Wengine wanatilia makini kuzisaidia jamii ambazo hazijachukua hatua za kunufaika na teknolojia mpya ili kuzitoa simulizi zao nje. Wengine wamejiunga kwa dhumuni la pamoja dhidi ya kuchuja habari na ukandamizwaji wa wale ambao wanatumia haki yao ya kujieleza kwa uhuru kwa mujibu wa kipengele cha 19 cha Azimio la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu.

Jamii ya GV haijaruhusu kujikwamisha katika mijadala isiyoisha kama wanablogu ni wanahabari au la, au wavuti unamaanisha nini katika biashara ya habari. Kadhalika GV haijifungi katika mizozo kuhusu je Wavuti utakuwa ni nguvu ya demokrasi duniani au la. Kama jamii tunatilia mkazo kukunja mikono ya mashati yet una kuingia kazini ili kukabiliana na tatizo hai zaidi: kuziba mapengo yaliyo kwenye mjadala wa umma duniani, na kufanya tunaloweza kuhusu mizani isiyo sawa, uonevu na ukiukwaji wa haki katika vyombo vya habari duniani. Haijalishi namna utakavyobainisha kazi hii, tunaamini kuwa kile tunachokifanya kina thamani na kinabadilisha mambo.

Tunashukuru kwamba mashirika kadhaa yameiona kazi yetu kuwa ina thamani kwa ufadhili wao kifedha. Tumeendeleza uhusiano na vyombo vya habari ambavyo vinafuatilia kazi zetu na kututaka kwa sababu – kwa namna yoyote utakavyoeleza tunachofanya – jamii yet uni chanzo chenye thamani cha habari za dunia na mitazamo mipya. Hii ni sababu ambayo Reuters ilitoa usaidizi wa kiini katika miaka yetu mitatu ya kwanza, na sababu ambayo mashirika mengi ya habari yanaendelea kufanya kazi na wahariri wet una kuwasiliana na watu wanaojitolea kwa ajili ya mahojiano. Wakati hatuwezi kusema kuwa tumebadilisha kabisa uanahabari wa ulimwengu, tunaamini kuwa tumeweza kuyaelekeza macho ya vyombo vya habari kwenye habari nyingi ambazo vinginevyo zisingeweza kuripotiwa, na kutoa mitazamo mipya juu ya hamari nyingi za kimataifa. Jambo hilo pekee limeifanya jitihada hii kuwa ya thamani.

Jambo la kusisimua zaidi ni jinsi Global voices ilivyobadilisha maisha ya wahariri wetu, watu wanaojitolea na jamii pana ya wanachama. Tumekuwa kituo ambacho kundi la kuvutia la watu wenye vipaji, werevu na wanaojali wengine hupata kuridhika, kutambuliwa duniani, na usaidizi wa kijamii. Bonyeza hapa ili kusoma juu ya jinsi ambavyo Sauti Zinazokua ilivyozileta sauti zenye utofauti katika mazungumzo ya kitaifa na ya kidunia, na maana ya jambo hilo kwa watu binafsi na kwa jamii husika. Ili kuapata kionjo cha namna ambavyo waandishi wetu wa kujitolea walivyo, soma na kusikiliza baadhi ya wasifu wa wanablogu hao hapa.

GV pia imekuwa na msukumo kwa jamii mbalimbali za wanablogu duniani ambazo tuna uhusiano rasmi nazo – zaidi ya kuweka viunganishi na kutafsiri baadhi ya makala zao za kwenye blogu katika wakati tofauti tofauti. Mfano mmoja tu: Ethan hivi karibuni alielezea mazungumzo yanayofungua macho na mwanablogu kijana wa jamii ya Kyrgiz, Bektour Iskander kuhusu athari za baadhi ya kazi zetu huko Asia ya Kati.

Kile kitakachotokea kutoka katika mazingira ya uanahabari duniani yaliyo na demokrasia zaidi kidogo, yaliyo wazi na shirikishi bado hakijajulikana wazi. Katika mkutano wa 2004, mwanablogu wa Kiirani Hossein Derakhshan alielezea matumaini kwamba kuenea kwa uanahabari wa kiraia kwenye wavuti kutazifanya jamii kuwa za kidemokrasi zaidi na kwa serikali kuapta ugumu zaidi katika kuhalalisha vita. “Hoder” kama anavyojulikana kwenye wavuti, amefungwa na utawala wa Amhedinejad kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa, haieleweki kama uhusiano mpana kati ya Wairani na Wamagharibi utakuwa ndiyo sababu kuu katika uamuzi wa Marekani wa ama kuivamia au kutoivamia Irani. Waandishi kama Evgeny Morozov wanadai kuwa kinyume na matumaini ya awali kuhusu wavuti kuwa nguvu ya demokrasi, tawala za kiimla zinang’amua jinsi ya kutumia wavuti ili kuimarisha nguvu zao na kukandamiza upinzani – na kwamba wavuti katika nchi nyingi inatawaliwa na upindishaji wa habari, utoaji wa habari potofu na chuki. Wengine kama Clay Shirky na Patrick Meier wanadai kwamba bado kuna sababu ya kutumaini. Na bado wengine wanaonyesha kuwa wengi wa watu duniani wana matatizo makubwa zaidi – kama vile kuishi tu – na yote hapo juu pamoja na kazi za Global Voices hazina maana kwao.

Miaka mitano iliyopita Ory Okolloh – ambaye aliendelea na kuanzisha jukwaa lililofanikiwa sana la kuripoti la jamii Ushahidi – alitoa maoni fulani yanayopaswa kurejewa katika muktadha wa midahalo hii. Hivi ndivyo nilivyoripoti maneno yake wakati huo:

Mwanablogu wa Kenya Ory Okolloh hategemei kuwa Afrika itabadilishwa na kublogu katika wakati wowote hivi karibuni. Kuunganisha utengano wa kidijitali pengine ni jambo la chini sana katika matatizo mengi ya Afrika. Haidhuru, ory anafikiri kuwa kublogu ni jambo muhimu – kama si jambi linalobadilisha – kwa idadi ndiogo ya Waafrika wanaoblogu. “Kwa vijana, hatujasikilizwa, hatuna sehemu katika Afrika ndani ya siasa au katika majukwaa mengine kuweza kujieleza,” anasema Okolloh. “Nafikiriinaweza kutoa jukwaa kwa vijana kuunda sehemu yao wenyewe. Sidhani kama itabadilisha siasa kabisa au itaelekeza uchaguzi bali ninafikiri itaweza kuzaa jamii katika nia ambazo hazijawahi kuweza kutokea kabla.”

Uanahabari wa kijamii kwenye wavuti unazaa namna mpya za jamii katika ngazi za sehemu husika, kitaifa na kidunia. GV imekuwa chembe hai tepe inayonganisha jamii ya wanablogu wa Kikenya ya Ory na wanablogu wengine duniani ambao wanashiriki maadili yanayofanana.

Wakati Global Voices ina nia ya kuelekeza habari zinazoripotiwa na vyombo vya habari vya kitamaduni – ambavyo vingi vyake vinahudumia mataifa au maeneo malum – kadhalika tunajenga jukwaa kwa ajili ya mazungumzo ya kidunia, na jamii ya raia wa dunia katika mazungumzo hayo. Tunatumia wavuti si kwa ajili ya kutoroka kutoka katika ubinadamu wetu, bali kwa ajili ya kuusisitiza. Tunaamini kuwa maamuzi binafsi na vitendo vianasababisha mabadiliko. Ikiwa wavuti hatimaye utawezesha zaidi kuliko unavyotia watu utumwani kutategemea kama tutachukua wajibu kwa ajili ya mustakabali wetu na kutenda. Kujenga jamii ya tamaduni mbalimbali na lugha mbalimbali inayomakinikia miradi mahsusi inayounganishwa na seti ya maadili ya kiutu ni jitihada ndogo katika mwelekeo huo.

3 maoni

  • shaban kaluli

    wananchi tuwe makini na bunge la bajeti kwa kufuatilia matangazo ya moja kwa moja kwenye tv

  • ninaomba kushirikiana nanyi lakini sijajuwa jinsi ya kuweka makala yangu na makala ya aina gani yana takiwa nikimaanisha ya kidini,kijamii ,kielimunk

  • Dear Sir/Madam
    I am Mr kadir Are you a business man or woman? Are you in any financial stress or do you need funds to start up your own business? Do you need a loan or for any reason funding such as, a) Personal Loan, Business Expansion.b) Business Start-up and Education.c) Debt Consolidation.? I can help you with the urgent loan you need.contact us at globalserviceloana@gmail.com

jiunge na Mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.