Pakistani: Musharraf Aondoka Jengoni

Imepita miaka nane, siku mia tatu na ushee tangu mapinduzi yasiyo ya kumwaga damu yaliyoongozwa na Jenerali wa Jeshi la Pakistani yalipofanyika na hivyo kumpokonya madaraka kiongozi fisadi Nawaz Sharif. Wakati huo kulikuwa na matumaini ya kesho mpya, ilikuwa ni mwendo wa madaha kuelekea kwenye dira iliyofifia iliyopachikwa jina la ‘mwamko wa wastani wenye kuongozwa na fikra pevu’ na ama kwa hakika hatua muhimu katika kuiondolea jamii gonjwa lililogeuka kuwa janga, yaani, rushwa. Wakati huo raia wa Pakistani walisherehekea, lakini haikupita muda mrefu kabla watu hawajang’amua kuwa walikuwa tena kwenye janga wasilotaka, na kwa bahati mbaya ujaji huo polepole uligeuka kuwa utawala wa kidikteta usiotakikana. Baada ya miezi mingi ya utawala wa mabavu, hivi majuzi kulitokea tukio la kumaliza utawala uliodumu muda wa miaka tisa kasoro siku sitini, na hapa Pakistani inafungua ukurasa mpya.

Ilionekana kama siku nyingine nchini Pakistani lakini mara iligeuka kuwa inayojijaza munkari na mara minong’ono ilianza kusambaa miongoni mwa raia wakati habari zilipoanza kusambaa. Watu hao waligubikwa na mnong’ono mmoja baada ya mwingine kutoka katika taarifa zilizorushwa na vituo vya televisheni kwenda kwenye ujumbe mfupi wa maneno na hata barua pepe; ilikuwa kana kwamba majaaliwa ilikuwa yaamuliwe na kila mmoja wao. Gazeti tando moja linalokwenda kwa jina la linatupa muhtasari makini kuhusu msukumo wa minong’ono hiyo katika sentenso moja: ‘Simu inaita – Mushy anaondolewa madarakani kwa manufaa ya umma … tazama GEO (kituo kimoja cha televisheni) … SASA hivi’ Wapo waliotuaminisha kwamba huyu jamaa anayekwenda zake angejaribu kujitetea ili abaki madarakani, wapo waliotabiri kwamba huenda angerejesha mfumo wa mahakama kama njia yake pekee ya kujinusuru na kulipiza kisasi; kinyume chake hali imegeuka kuwa hotuba ya kuagia, akiachia mambo mbele ya watu wake wa karibu waliokuwa wakilengwalengwa na machozi, hali ambayo tunahabarishwa kupitia kwamba ‘akiwa amevaa uso usio na tabasamu Musharraf, huku akipepewa na bendera za Pakistani nyuma yake na picha ya ‘mwanzilishi’ wa taifa hili aliishia kusema “Naweka hatma yangu mikononi mwa umma.”

Pervez Musharraf – Picha kwa hisani ya: Mtiririko wa picha za Flickr wa Mkutano wa Uchumi Duniani zilizo chini ya haki miliki huria kwa umma.

Kuaga huku kulikotawaliwa na machozi kulikofanya na Musharraf mnamo tarehe 18 Agosti mwaka huu kulikuja zikiwa zimepita siku nne tu tangu Taifa liadhimishe sherehe za miaka 61 ya Uhuru. Ni katika hali ya tahadhari kubwa kwamba Pakistani inaadhimisha mwisho huu wa miaka tisa ya utawala wa familia hii. Hotuba yake ya mwisho ilijaa hasa kurejelea historia na hii ni kama ilivyonukuliwa na The Pakistani Spectator, yaani hasa kuelezea ni kwa namna gani alitumikia nchi na watu wake.

Wanablogu wa KiPakistani walipokea taarifa hizi kwa hisia tofauti, wapo waliomshabikia kwa miluzi yenye kuashiria kwamba alikuwa ‘a Jolly Good Fellow’ (mtu mwema na mchangamfu), wakati huohuo washabiki wake waaminifu hawakukawia kumpigia mbija za kumpongeza, hata hivyo wapo waliochukua hali hii kwa tahadhari huku wakisherehekea kumalizika kwa utawala wa kidikteta. Katika namna ya kukejeli, Yeah That Too alishirikisha maneno machache, Ammar kwa upande wake aliandika kuhusu namna ‘Mpambano mpya wa manyau’ unavyokaribia kuanza, Chowrangi anazungumizia mustakabali wa nchi ya Pakistani baada ya Musharraf, Psychotic Discourses anatupatia mwanga juu ya muundo mpya wa ‘Utawala wa Kishetani’ (Demon-cracy), wakati ambapo MB anatuchanganya zaidi kwa kuzungumizia hali hii kama moja ya mizunguko ya kisarakasi.

Swali kubwa kwa sasa linabaki kuwa endapo Musharraf anaruhusiwa kutafuta ukimbizi nje ya Pakistani au endapo atafikishwa mbele ya sheria ili kujibu tuhuma mbalimbali zinazomkabili. Ama kwa hakika ni changamoto kubwa kwa Taifa la Pakistani na ambayo inaweza kuwa na matokeo mengi.

Mtu anabaki kujiuliza, hivi nini kinafuata, hasa katika kipindi hiki ambapo kuna wanasiasa wenye matumaini ya kunyakua cheo hicho cha juu zaidi katika taifa hili, ambapo hata hivyo jukumu la kuiondoa nchi katika mkanganyiko huu mkubwa liko zaidi mabegani mwa Asif Zardari na Nawaz Sharif, ambapo wote wawili ni wanasiasa ambao hawakuchaguliwa lakini ambao wengi wanawawekea matumaini makubwa ya kuiondoa nchi hii kutoka katika lindi la vurugu ambamo imo kwa sasa.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.