Arabeyes: Rais wa Mauritania Aliyepinduliwa Katika mapinduzi ya Kijeshi


MAKAMANDA wa jeshi wamemuondoa madarakani Rais Sidi Ould Cheikh Abdallahi, rais wa kwanza kuchaguliwa katika uchaguzi huru katika miongo miwili, katika mapinduzi ya kijeshi yaliyofanywa Jumatano iliyopita baada ya mtafaruku wa kisiasa uliotokana na rais huyo kuwatimua kazi majenerali wanne wa ngazi za juu wa jeshi. Makamanda wa jeshi walitangaza kuundwa kwa Baraza jipya la taifa na kiongozi wake, Jenerali Mohamed Ould Abdel Aziz (mmoja kati ya majenerali wanne wa jeshi waliotimuliwa), kwenye radio na vituo vya televisheni vya serikali. Jenerali Abdel Aziz ni miongoni mwa walioshiriki mapinduzi ya kijeshi nchini Mauritania mwaka 2005.

Bloga kutoka Algeria The Moor next Door amekuwa akiblogu habari hii kwa kina anaripoti:

Ninapozungumza na Wa-Mauritania wanaojua, baadhi yao walihisi kutokea kwa mapinduzi wakati wa kiangazi kama ilivyotokea, wakati wa kipupwe au isingeweza kutokea kabisa. Hisia zangu mara zote zilikuwa zikinielekeza kwamba mapinduzi haya yangefanyika majira ya kiangazi (Sijawahi kuandika bayana juu ya hili, lakini nimelielezea hili katika majadiliano na sikutaka kuchangia lolote kuhusiana na sakata hili. (1) kwa sababu Western Sahara Info. taarifa za kutoka Sahara Magharibi zilielezea kinaganaga na hakukuwa na haja ya kushindana ikiwa wewe ni mmoja wa mabloga wawili au watatu unakuwa miongonimwa wanaofuatilia sakata hili kwa karibu sana. (2) nilitaka kuhakikisha kwamba kama ‘ningetabiri’ jambo hili nisingekosea; Ningeweza kutabiri kuwa ‘Mwishoni mwa miezi ya Mei, Juni, Julai na Agosti Serikali ya Rais Sidi, isingelikuwapo tena’ na ningekuwa nimekosea; mimi si mtabiri wa hali ya hewa, na (3) sijawahi kukutana na raia wa Mmauritania ambaye lolote jema la kumzungumza kuhusu Sidi, ukiachilia mbali uzuri wa wajihi wake.) Mojawapo ya mashinikizo yaliyomfanya Rais Sidi afanye alivyofanya ni kuwapo tishio la kuundwa tume huru ya kuchunguza mapesa ya mfuko wa maendeleo wa mkewe, tume ambayo ingemuweka hata yeye mwenyewe pabaya zaidi. Tume hiyo pia ingeufanya utawala wa Rais Sidi kituko kutokana na matumizi mabaya ya fedha za umma. Kwa mfano, nimeambiwa kuwa, safari zake za ndege za nje ziliigharimu serikali zaidi ya dola za Marekani mbili bilioni, kwa kukodisha ndege za kifahari yeye na familia yake na ujumbe wake pamoja na anasa zingine zisizokuwa za lazima. Kwa hakika alikuwa katika wakati mgumu: Ama angelazimika kujiuzulu (kwa mujibu wa Olmert) katika aibu kubwa au angelazimika kuvunja bunge na hivyo kuunda serikali yake upya, hali ambayo ingempeleka katika mapinduzi kama haya tuliyoyoyashuhudia, ambayo angalau imeficha aibu yake kisiasa. Alibanwa pande zote na alikuwa hana pa kutokea zaidi ya kukumbana na hatima yake.

Western Sahara Info amekuwa akiblogu mgogoro huu tokea ulipoanza, na leo ametuletea habari za mapinduzi hayo ya kijeshi kama zinavyotokea dakika kwa dakika, pamoja na muhtasari wa unyambuzi:

Uchambuzi wa harakaharaka, ambao naweza kuujutia: balaa kwa demokrasia ya Mauritania, kwa upande mmoja, (demokrasia) ambayo haikuwa na nafasi, lakini muhimu zaidi ni kuwa (mapinduzi haya) yamerudisha nyuma nafasi iliyokuwepo kwa maendeleo ya kisiasa. Ingawa, Rais Abdellahi na washirika wake si malaika, lakini Majenerali Ghazouani na Abdelaziz wanawakilisha kundi baya la kinyonyaji katika utawala wa Mauritania, kwa kukataa kuruhusu utawala wa kiraia kutulia madarakani kwa kuwatishia kung'oa kabisa utawala wa kiraia hatimaye. Kama mapinduzi ya mwisho ya kijeshi yaliyotokea Agosti 2005, yangalieleweka na Jumuiya ya Kimataifa baada ya kung'olewa kwa Rais Ould Tayaa, na hatimaye kupelekea mabadiliko makubwa, mapinduzi haya ya juzi yalikuwa tofauti saana. Kilichotokea mwaka 2005 ilikuwa kwamba madikteta wa kijeshi walioegemea katika ukabila waling'atuliwa na nafasi ilijitokeza ikasimika badala yake utawala wa kiraia uliokuwa na muundo wa nusu-mabavu ambao uliruhusu desturi nyingi za kidemokrasia kwa muda mwingi zaidi, (utawala huo) ulishughulikia zaidi muwafaka wa kitaifa, urejeshwaji wa wakimbizi na maendeleo ya kiuchumi; ingawa siyo hema, lakini ilikuwa bora. Mabadiliko haya hivi sasa yanageuzwa. Wapinduaji – japokuwa wengine ni miongoni mwa wale waliofanya mwaka 2005 – – ni lazima walaumiwe na matokeo ya mapinduzi yabatilishwe kama inawezekana; Mauritania ilikuwa na fursa ya pekee kuweza kuvunja mzunguko huu usiokwisha, na sasa (fursa hiyo ya pekee) inaponyoka.

Blogu ya Roads To Iraq, katikaujumbe wenye kichwa cha habari “Wamarekani walipanga mapinduzi nchini Mauritania,” inaripoti habari hiyo vile vile:

Mambo yanabadilika kwa kasi sana nchini Mauritania, imeanza na mapinduzi asubuhi hii, kwa kutoa “taarifa nambari moja” katika kituo cha televisheni cha Mauritania, Mkuu wa kituo hicho cha televisheni
alibadilishwa sababu alikataa kushirikiana na mkuu wa jeshi aliyeandaa mapinduzi na kumtangaza mtawala mpya wa kijeshi.

Huko Misri, Bella [Ar]anasema kilichotokea Mauritania kimedhihirisha kuwa Waarabu hawakupangwa kwa demokrasia.

Inaonekana demokrasia haikuumbwa kwa watu kama sisi – ambao hatuwezi kupumua nje ya tawala za kijeshi.

Baada ya kutupa historia fupi ya demokrasia changa ya Mauritania Bella anaandika:

Kwa njia hii, Mauritania, ambayo ilikuwa ianze kuvuna matunda ya demokrasia katika msukumo wa kiasisi ambao eneo lote la mataifa ya jirani yalikuwa yanaungalia kwa shauku, mambo yamerejea kule yalikotoka kiasili, na wanajeshi wakaingilia kati na mapinduzi kutokea.

Bloga wa Kuwaiti Wild Il Deera anahoji maswali machache kuhusiana na mapinduzi haya. Anauliza:

Jumuiya ya Kiarabu ina msimamo gani kuhusu viongozi wa mapinduzi haya?
Hivi huyu kiongozi wa Mauritania hakuchaguliwa na watu wake?
Hivi inawezekanaje kundi la kisiasa, kama Jumuiya ya Kiarabu, ambayo inataka kuheshimiwa katika jamii ya Kiarabu na katika ulingo wa kimataifa ikaruhusu mapinduzi kama haya kufanyika katika moja ya mataifa wanachama wake?

Bloga maarufu nchini Morocco Larbi [Fr] alipachika kiungo cha makala ya ya habari, kisemacho:

Unaweza kusema: Afrika ni bara lililolaaniwa!

Habari yake hiyo imepata maoni mengi. Citoyen anatoa maoni kwamba:

Ni kweli mapinduzi hayatabiriki Afrika… Nashangaa, ingawa, kama kwa mara nyingine tena, Mashirika ya Moroko yamekatizwa kama yalivyokuwa mwezi Ogasti 2005?

Mwishoni KABOBfest, ambaye huwa anaingiza vichekesho katika kila hali, anatoa maoni yenye mzaha:

Wakati utamaduni wa mapinduzi katika mataifa mengi ni utamaduni uliopitwa na wakati (kama vile Syria hakujapata kutokea mapinduzi kwa miongo kadhaa sasa) Baadhi ya mataifa yanapendelea mitindo ya kizamani, rejea pale ambapo ianonekana palikuwa na mapinduzi kama juma moja lililopita sehemu fulani hapa duniani. Wakati Mauritania siyo Fiji, wanadumisha utamaduni usio na maana wa mapinduzi katika dunia ya Waarabu.

Blogu ya Arabdemocracy pia anayo taarifa ya maombolezo ya iliyokuwa demokrasia changa.

Picha ya hapo juu ni ya Sidi Mohamed Ould Cheikh Abdallahi iliyopigwa na Marcello Casal Jr./Abr (Septemba 2007)

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.