Angola, Brazil: Mshituko na Utengano wa Kitamaduni


Kinyago cha mtumwa mweusi kilichochongwa na Luiz Paulino da Cunha. Picha kwa hisani ya Asasi ya Watoto Walio Hatarini.

Angola na Brazil zina uhusiano maalum baina yao, kutokana na matumizi ya lugha moja na pamoja na historia yao ya kutawaliwa huko nyuma – nchi hizi mbili zilikuwa sehemu ya himaya ya Wareno – na utamaduni wa pamoja unaotoka na historia ya asili moja. Tangu mwaka 2000, biashara kati ya mataifa haya mawili ilianza kukuwa na sasa inachanua. Kwa mujibu wa Chama cha Makampuni ya KiBrazili nchini Angola (AEBRAN), biashara kati ya mataifa mawili haya imekuwa kwa mara sita zaidi tangu mwaka 2002.

Kutokana na kuongezeka huko kwa biashara, uwepo wa makampuni ya Brazili nchini Angola pia kumeongezeka. Kumepelekea, pia ongezeko la uhamiaji kutoka Brazili kwenda Angola kwa kadri ya asilimia 70 kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita. Inakadiriwa kuwa kuna Wabrazili 5,000 waliosajiliwa nchini Angola haswa wanaojishughulisha na masuala ya ujenzi, uchimbaji madini na biashara za mazao ya kilimo. Maendeleo haya mapya katika historia ya Angola, nchi iliyozoea kuwa na uhamiaji kuelekea ng'ambo nyingine ya Atlantiki, yanapelekea kwenye mtikisiko wa kiutamaduni usioweza kuepukika kwa wote, Wabrazili na Waangola pia.

Hapa chini kuna habari zilizopachikwa katika kurasa za blogu mbili zikionyesha mitazamo tofauti baina ya watu wawili kwa kuibua masuala muhimu kama uhamiaji, ubaguzi wa rangi, ukabila na heshima miongoni mwa watu. Zaidi ya yote, wanabainisha mahusiano ya namna mbalimbali na yenye mchanganyiko – kwa kuwianisha yale yanayofanana na yanayotofautiana – miongoni mwa watoto hao waliotenganishwa na bahari wakati wa makuzi yao.


Kinyago cha mtumwa mweusi kilichochongwa na Luiz Paulino da Cunha. Picha kwa hisani ya Asasi ya Watoto Walio Hatarini.

Migas [pt], Mbrazili anayeishi Luanda, anasema yafuatayo:

Nimekuwa nikiuangalia uchaguzi wa Septemba kwa mtazamo chanya. Nina matumaini kwamba matukio ya vurumai yaliyowahi kutokea huko nyuma hayatatokea tena. Kila mmoja anakubaliana kuwa taifa linahitaji amani ili kuweza kufuatilia makuzi ya uchumi, maendeleo, hali bora ya maisha. Labda maisha bora ni lengo lililokwishasahaulika. Hata hivyo, tukio linakaribia. Septemba 5 ni siku iliyochaguliwa na kila mmoja anasubiri kwa hamu awe raia wa Angola au wa nje.

Ninaishi katika eneo ambalo mimi peke yangu ni mgeni kutoka nje ya nchi. wengine wote ni watu weusi, waliopo katika tabaka ambalo siwezi kujitambulisha nalo. Siyo matajiri na wala siyo masikini. Lakini hawako kwenye tabaka la kati pia. Naweza kusema ni masikini zaidi kuliko matajiri, kwa mujibu wa viwango vyangu. Hata hivyo, ni matajiri kiasi kuweza kuwa na hifadhi za maji, majenereta, magari na vyakula katika meza zao. Katika moja ya wikiendi zilizopita, kulikuwa na sherehe katika kaya mojawapo. Ilikuwa ni hafla ya kuadhimisha kuzaliwa. Ninajuta kushinda nyumbani siku hiyo.

Hafla hiyo iliendelea mpaka mapambazuko na mcheza santuri (DJ) alichagua miziki kabambe. Nilijijutia kwa sababu nilikuwa nimekwishaamua kubaki nyumbani na kulala mapema. Baada ya kurejea nyumbani nikitokea dukani majira ya saa nne hivi usiku, nikaona gari moja likiwa limeegesha katika sehemu yangu ya maegesho. Sikuwaambia waondoe gari lao, lakini nikatafuta “suluhisho la haraka” (katika desturi nzuri ya kaskazini) ili kwamba [magari] yaendelee kuwepo pale. [gari] langu na lile la mgeni. Mgeni, ambaye ni wazi alikuwa amelewa, aliniacha nikisubiri na akarejea kwenye hafla, kwa madai ya kutafuta funguo za gari. Dakika chache baadaye, alisahau ombi langu na alikuwa akisakata muziki wa dansi na watu wengine.

Nilimudu kukabiliana na suala lile angalau kidogo, lakini ni lazima nikiri sikupenda tabia yao. Habari hii inabainisha hofu zangu. Sina shaka kwamba uchaguzi utaleta kiwango kikubwa cha ulevi, hafla kadhaa na tabia za hovyo. Na hilo linanitia hofu miye. Kama mpaka sasa sijapata kuhisi kukosa raha kwa kuishi kwenye maeneo ambayo nyumba yangu pekee ndiyo makazi ya mtu mweupe, niligundua usiku ule kwamba hafla zinazochangamshwa na pombe zinaweza kuleta matukio ya usumbufu, hata katika sehemu tunazojihisi vyema.


Mtoto wa miaka 12 Naomi Leonardo de Queiros, Picha kwa hisani ya Asasi ya Watoto Walio Hatarini.

Hapa chini kuna mtizamo tofauti, kuhusu hafla nyingine na taswira nzima ya uhamiaji huu mpya na Gil Gonçalves [pt], raia wa Angola:

Jijini Luanda, Kampuni za Brazil zinajihusisha na ubeberu wa Marekani. Brazil ni koloni la Marekani. Wengi, kwa kweli raia wengi wa Brazili wameshawasili na wanazidi kuwasili Luanda kama samaki wa kopo.

Kule Movicel, kuna kampuni ya mawasiliano ambako wanashikilia imara idara ya masoko, wanawaleta kaka na dada zao kama vile ni wataalamu wenye ujuzi wa juu wa masuala ya teknolojia. Watu wa Luanda ndiyo wanawafundisha jinsi ya kufanya kazi, kwa sababu masikini watu hao wamefika hapa wakiwa hawajui kusoma. Nchini Brazili inaonekana kama vile hakuna Vyuo Vikuu au kama vipo basi havifanyi kazi. Wanapata mishahara katika maalfu ya dola za kimarekani na wana haki ya kupata maalfu marupurupu ya anasa. Na wa-Luanda wanalipwa dola kiduchu. Mfumo wa kikoloni lazima udumishwe.

Wanaume na wanawake wa Kibrazili wamevamia hoteli, iko kwa ajili ya miliki yao tu. Wanavuta sana (sigara), wanfanana na volkeno inayolipuka wakati wote. Kila mara wanaangusha pati kwenye kiwambaza. Kama watu wasio na elimu ya masuala ya kijamii wanapiga wanaporomosha miziki miovu inayowakosesha usingizi watwana wa Luanda. Hawajui, wanajifanya hawajui , kwamba jijini Luanda uchafuzi wa mazingira kwa kupiga kelele ni kinyume cha sheria na ni kosa la jinai., Wageni wasioheshimu sheria za nchi walizofikia wanastahili kutimuliwa. Lakini kwa kuwa [hoteli] inamilikiwa nao na baadhi ya marafiki zao kutoka Luanda…

Cha kushangaza katika yote haya ni kwamba Wabrazil… wote ni weupe. Wako wapi wanaume weusi? Wananawake weusi? Je wamekimbia kutoka Zumbi quilombo? Hivi walipelekwa katika makambi ya ya maangamizi ya Nazi? Au wamejificha katika misitu ya Amazoni? Au wameangamizwa? Je hivi hawatakiwi au ni haramu? Au wanapamba maonyesho ya wanyama mwitu? Au wametupwa baharini?

Kwanini pasiwe na ujasiri wa kusema hadharani kwamba hakuna Wabrazili weusi huko Brazili!

Picha inayoelezea kisa hiki zinatoka katika mtandao wa picha wa Symbols and Symbolism Flickr photo set kwa hisani Asasi ya Watoto Wanaoishi katika Mazingira Hatari na unatumiwa chini ya leseni ya mfumo Huru wa Haki Miliki. Zinaonyesha picha za historia ya miaka 300 ya utumwa nchini Brazil na athari zake ndani ya nchi hiyo, kama vile urithi wa Candomblé. Hapa chini ni maelezo ya picha hiyo:

Mtu mweusi aling'olewa kutoka katika ardhi yake na kuuzwa kama bidhaa, utumwani. Aliwasili nchini Brazili kama mtumwa, kifaa; kutoka katika ardhi yake alitoka kama mtu huru. Wakati wa safari, safari ya utumwani, alipoteza utu wake, lakini utamaduni wake, historia yake, nchi yake, na uzoefu wake alikuja navyo.

Miaka 300 ya historia ya utumwa wa mtu mweusi nchini Brazili imeacha athari kubwa ndani ya nchi hiyo. Candomblé ni mojawapo ya athari hizo, dini iliyojawa na siri nyingi, ishara za matambiko yanayofahamika tu kwa wanaopitipia matambiko hayo lakini pia ni ni sehemu muhimu ya utamaduni wa Brazili. Hakuna idadi kamili kuhusiana na watu wangapi wanaabudu Candomblé. Serikali inakadiria, kihafidhina, kwamba kuna vituo zaidi ya 300,000 vya kuabudia imani za Wabrazili wenye asili ya Afrika, ambavyo vinajumuisha Candomblé. Wanaoshiriki katika imani hizo wanadhaniwa kufikia angalau theluthi moja ya watu wote wa Brazili wanaokaribia milioni 170. Wengi wanaabudu katika Ukatoliki na Candomblé.

Bahia, jimbo ambalo lina asilimia kubwa zaidi ya watu weusi, ndiyo makao makuu ya dini hii, ambayo inafuata kwa karibu asili yake ya Kiafrika na hasa tamaduni za Kiyoruba za Nigeria na za Kibantu za Angola na Kongo. Tamaduni za Kiyoruba zinazojumuisha majina yanayotumika sana ya Orisha (miungu ya mahekalu ya Kiafrika), bado inatawala sana. Hivi sasa Candomblé inatambulika rasmi na inalindwa na serikali ya Brazil. Hata hivyo, enzi za utumwa na miongo mingine iliyofuata baada ya kukomeshwa kwa biashara hiyo ya watu nchini Brazil mwaka 1888, ibada za Candomblé zilipigwa marufuku na serikali na kanisa Katoliki, na wafuasi wake waliadhibiwa vikali.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.