Serikali ya Nijeria yaifungia Twita baada ya mkanganyiko wa twiti ya rais iliyotishia matumizi ya nguvu kufutwa

Picha Rasmi ya Rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Naijeria, Rais Muhammadu Buhari iliyopigwa na Bayo Omoboriowo via Wikimedia Commons, Mei 29, 2015, (CC BY-SA 4.0).

Serikali ya Naijeria imetangaza siku ya Ijumaa kwamba inaufungia mtandao wa Twita nchini humo, siku kadhaa baada ya mtandao huo kufuta twiti hatari iliyoandikwa na Rais wa Naijeria Muhammadu Buhari iliyodai kwamba serikali itatumia nguvu dhidi ya kabila la Igbo.

Pamoja na kuondolewa kwa twiti hiyo, ujumbe uliendea kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, hali iliyokumbushia maumivu ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyopoteza maisha ya watu zaidi ya milioni moja. Lakini twiti hiyo ilichochea harakati kwenye mitandao ya kijamii kusimama na Wanaijeria wa kabila la Igbo.

Kwenye mfululizo wa twiti zilizochapishwa mnamo June 1, 2021, Buhari anatishia “kuwashughulikia” Wanaijeria wanaotoka kwenye sehemu ya mashariki ya nchi hiyo “kwa kutumia lugha wanayoielewa,” akirejea vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Naijeria kati ya mwaka 1967-1970 dhidi ya vuguvugu la kujitenga la Jamhuri ya Biafra, kusini mashariki mwa Naijeria. 

Twiti hiyo iliandikwa baada ya mfululizo wa mashambulio dhidi ya serikali na vyombo vya usalama kwenye eneo hilo, ambalo linalaumiwa kuwa na kikundi cha kijeshi  kinachohusishwa na Wenyeji wa Biafra (IPOB), vuguvugu la watu wanaotaka sehemu ya Biafra ijitenge. Kikundi hicho kimekanusha kuhusika na mashambulizi hayo, kwa mujibu wa Sauti ya Amerika.

“Wengi wa wale wanaoonesha utovu wa nidhamu leo walikuwa wadogo kuelewa uharibifu na upotevu wa maisha ya watu uliotokea wakati wa Mapigano ya Wenyewe kwa Wenyewe nchini Naijeria,” ilisema twiti ya Buhari ambayo sasa imefutwa: 

Picha ya twiti ya vitisho ya Rais wa Naijeria Buhari

Twiti zilizojibu mapigo kwa matamshi hayo yaliyotolewa na Buhari aliyeonekana dhahiri kuwa na hasira akiwa katika Ikulu ya nchi hiyo, makao makuu ya nchi, Abuja, kuhusu mwelekeo wa mashambulizi dhidi ya maafisa wa uchaguzi. “Ninadhani tumewapa jukwaa la kutosha. Wamesema walichokitaka, lakini sasa wanataka kuiangamiza nchi,” alisema, akionekana kuwazungumzia watu hao wanaotaka kujitenga: 

Buhari amezungumza kwa kinywa chake

Buhari, jenerali mstaafu, alikuwa jeshini wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Naijeria.

Vita hivyo vibaya vilisababisha vifo vya “zaidi ya watu milioni wa kabila la Igbo na wakazi wengine wa ukanda wa Mashariki,” kwa mujibu wa Chima J. Korieh, profesa wa Historia ya Afrika kwenye Chuo Kikuu cha Marquette nchini Marekani. “Kwa Wanaijeria wengi, vita vya kujitenga kwa jimbo la Biafra, kwa ujumla, huchukuliwa kama tukio la baya la kusahauliwa, lakini kwa watu wa Igbo waliopambana kujitenga, linabaki kuwa tukuo lililobadili maana ya maisha yao,” anasema mwandishi wa Naijeria Adaobi Tricia Nwaubani. (Dondoo: Mwandishi anatoka kabila la Igbo.)

Sera ya Twita kuhusu tabia za chuki inazuia twiti ambazo “zinahubiri ghasia na kutishia” watu kwa kigezo cha “rangi, kabila, asili ya utaifa wa mtu.” Twiti za namna hiyo, kama ya Buhari, hufutwa na kampuni hiyo au watumiaji wenyewe hulazimisha “kufuta maudhui yanayokwenda kinyume na sera.” 

Lai Mohammed, waziri wa habari wa Naijeria, alieleza kuondolewa kwa twiti ya rais huyo na kampuni hiyo ya mitandao ya kijamii kama “tukio la kushukiwa sana”: 

Twiti zenye vitisho bado zinaonekana mtandaoni

Uchunguzi uliofanywa na mtaalam wa mtandao ya kijamii wa Digital Africa Research Lab (DigiAfricaLab) unaonesha kwamba twiti ya vitisho iliyoandikwa na Buhari bado inaonekana “kwenye akaunti kadhaa” siku mbili baada ya kuwa imefutwa na Twita, “shauri ya kunukuliwa na watumiaji wengine:” 

Zaidi ya saa 30 baada ya Twita kufuta twiti ya rais wa Naijeria @MBuhari kwa kosa la kuvunja sheria, twitiiliyofutwa BADO INAONEKANA kwenye akaunti nyingi mtandaoni kwa sababu ya kunukuliwa!

Kwa kuingia mtandao “kwa kutumia akaunti tofauti” kupitia “vifaa tofauti,” DigiAfricaLab iliweza kuona zaidi ya twiti 17,000 zilizonukuliwa na watumiaji kabla kampuni hiyo ya mtandao wa kijamii haijaifuta twiti hiyo kutoka kwenye “akaunti ya @MBuhari na @NGRPresident,” zote zikiwa ni anuani za twita zilizohakikiwa zinazotumika na Rais Buhari. Zaidi ya hayo, DigiAfricaLab iliweza kubofya na kukuza twiti ya Rais Buhari iliypfutwa. 

 — mpaka tovuti ihuishwe na nakala mpya ya twiti kwenye ukurasa mkuu wa akaunti husika.”

Mwitikio wa alama habari ya #IAmIgboToo

Twiti ya vitisho ya Rais Buhari iliibua mjadala mkali kutoka kwa Wanaijeria wanaotumua mtandao wa Twita, mjadala uliogonga vichwa vya mtandao huo kwa alama habari ya #IAmIgboToo kuonesha masikitiko yao. kadhalika, watumiaji wa mtandao wa Twita nchini Naijeria kutoka kwenye makundi mbalimbali ya kikabila pia walitumia majina ya lugha ya Igbo  kama namna ya kusimama na watu wa kabila la Igbo. 

Uchambuzi uliofanywa mnamo Juni 4, 2021 na Global Voices kwa kutumia zana ya Brand Mentions  ulionesha kwamba ndani ya siku saba, alama ishara ya #IAmIgboToo ilitajwa mara 508, imetumiwa mara 319,200, imewafikia watu 457,500, na kusambazwa mara 313,100 kwenye mtandao wa Twita na Instagram.

Picha ya maneno yanayotajwa kwenye alama habari ya #IAmIgboToo

Mwanaharakati wa Haki za Binadamu Aisha Yesufu — akitumia jina la Waigbo “Somtochukwu,” likimaanisha “ungana nami kumsifu Mungu” — huku akilaani namna Rais Buhaari aliyowatisha watu wa Igbo” wakisema “kushambuliwa kwa watu wa Igbo ni kushambuliwa mimi”: 

Jina langu ni Aisha Somtochukwu Yesufu
Tishio lolote kwa watu wa Igbo ni kunitisha na mimi
Kuwashambulia watu wa Igbo ni kunishambulia mimi
Nalaani vitisho vya 1967  kutoka kwa Rais Buhari kwa watu wa Igbo
Hakuna Mnaijeria ambaye ni zaidi kuliko Mnaijeria yeyote

Msanii wa muziki wa kufoka foka na mzalishaji wa muziki Jude Abaga (M.I Abaga) alionesha shauku yake kwa nchi hii kuendelea mbele ya matamshi haya yaliyojaa chuki: 

Maelezo kwamba “Naijeria inawachukua watu wa Igbo” ni ya kishamba na yanaacha mtazamo ule ule usiobadilika

Mwanaharakari wa #KomeshaSars Rinuola [Rinu] Oduala, akitumia jina la Kigbo “Ochiaga,” ikimaanisha “lkiongozi wa vikosi vya majeshi,” alikumbuka kwa fahari mchango muhmu wa wanawake wa Kiigbo kwenye historia ya Naijeria, akirejea Maasi ya Wanawake wa Aba  Novemba 1929:

Ninakumbuka Maasi ya Wanawake wa Aba ambapo wanawake wasiopungua 25,000 waliandamana dhidi ya unyanyasaji wa kikoloni.

Ninatoka kwenye eneo hilo hilo lenye wanawake wenye hulka hiyo, wakiwa wamezaliwa na ujasiri & uvumilivu dhidi ya miaka mingi ya unyanyasaji na ukosefu wa  haki.

Jina langu ni Rinu Ochiagha Oduala #MimiNiIgbo

Blossom Ozurumba, mtafsiri wa lugha ya Igbo wa Global Voices alibainisha kwamba “vitisho huanza na kutweza utu wa mtu”: 

Ukishatweza utu wa watu inakuwa rahisi kuondoa ule wasiwasi wa kimaadili kuhusu mauaji, ubaguzi au kutesa wengine kwa sababu tu ya utambulisho wa makabila. Kama hawaonekani kuwa binadamu, ni rahisi kuhalalisha matendo ya vurugu dhidi yao.

Kuteza utu, kwa mujibu wa Ozurumba, “kunafanya iwe rahisi kuondoa hali ya kuguswa kimaadili na vitendo vya mauaji, ubaguzi, au utesaji wa watu kwa sababu tu ya makabila yao.”

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.