Nchini Uganda, mtandao umekuwa uga wa makabiliano pale serikali inapojaribu kunyamazisha sauti ya upinzani inayozidi kukua mtandaoni.
Kwa miaka mingi, mamlaka za Uganda zimetumia mbinu tofauti kuukandamiza upinzani na kukirudisha chama tawala cha National Resistance Movement na Rais Yoweri Museveni madarakani.
Hii ni pamoja na kuzuia tovuti za vyombo vya habari, kuchuja ujumbe mfupi (SMS) na kuzima majukwaa ya mitandao ya kijamii. Wakati uchaguzi mkuu wa Uganda wa 2021 unapokaribia, viongozi wa utawala wanatarajiwa kuendeleza mbinu kama hizi.
Ufungwaji wakati wa uchaguzi wa 2016
Wakati wa uchaguzi mkuu wa 2016, viongozi wa Uganda walilazimika kuyafunga mara mbili majukwaa yote ya mitandao ya kijamii.
Ufungwaji wa kwanza ulitekelezwa mnamo Februari 18, 2016, wakati wa mkesha wa uchaguzi wa urais, na uliathiri majukwaa ya mitandao ya kijamii na huduma za kutuma pesa kwa njia ya simu. Uzuiaji huu ulidumu kwa jumla ya siku nne.
Mnamo Mei 11, 2016, majukwaa ya mitandao ya kijamii, ikiwemo Facebook, WhatsApp na Twita na huduma za kutuma pesa kwa njia ya simu zilifungwa kwa mara nyingine. Kufungwa huku kulidumu kwa siku moja na kulifanyika siku moja kabla ya Rais Museveni kuapishwa kwa muhula wake wa tano kama rais.
Museveni amekuwa madarakani tangu 1986. Upinzani dhidi ya uongozi wake unaimarika: Kulingana na kura ya maoni iliyotolewa mnamo Aprili 2019, idadi ya Waganda wengi inapinga uamuzi wa 2017 wa kuondoa kigezo cha umri wa 75 waa kugombea urais, ambacho kingeweza kumruhusu rais huyo mwenye umri wa miaka 74 kuwania tena katika uchaguzi wa 2021.
Wakati wa matukio yote ya ufungwaji mwaka 2016, serikali ya Uganda ilitaja kuwa sababu ilikuwa ni “usalama wa kitaifa” ili kudhibiti mtandao. Uvurugwaji uliagizwa na vyombo vya usalama vya Uganda na Tume ya Mawasiliano ya Uganda (UCC), ambayo inasimamia sekta ya mawasiliano, machapisho ya mtandaoni, utangazaji (wote redio na runinga), tasnia ya filamu, huduma za posta, usambazaji barua na vifurushi.
Mnamo Februari 18, 2016, MTN Uganda, mtoa huduma ya mawasiliano ya simu na mtandao, ilitoa taarifa kwenye Twita ikithibitisha kwamba “UCC, ilikuwa imeiagiza MTN kufunga huduma zote za mitandao ya kijamii na huduma za kutuma pesa kwa njia ya simu kwa sababu ya tishio la kiusalama kwa umma.” Agizo hili liliziathiri pia kampuni nyingine za simu kama vile Airtel, Smile, Vodafone, na Africel.
Siku hiyo hiyo, Rais Museveni aliwaambia waandishi wa habari kwamba aliamuru kufungwa kwa mitandao ya kijamii: “Hatua lazima zichukuliwe kwa ajili ya usalama kuzuia watu wengi kujiingiza kwenye taabu, ni kwa muda mfupi kwa sababu watu wengine hutumia njia hizo kusema uongo,” alisema.
Mnamo Machi 17, katika tamko rasmi wakati wa maamuzi ya Mahakama Kuu ambako ushindi wa Rais Museveni ulipingwa, mkurugenzi mtendaji wa UCC, Godfrey Mutabazi alielezea kwamba “alipokea maagizo kutoka kwa Inspekta Jenerali wa Polisi, Kale Kayihura, kufunga tovuti za mitandao ya kijamii na huduma za kutuma pesa kwa njia ya simu kwa sababu za kiusalama.”
Kufungwa huku kuliingilia haki na maisha ya kila siku ya Waganda wanaotumia mtandao na majukwa ya mitandao ya kijamii kupata habari, kuelezea maoni na kufanya biashara zao za kila siku. Majuma kabla ya uchaguzi wa 2016, Waganda walijitolea sana kuchapisha na kujadili kuhusu uchaguzi huo kwa kutumia kibwagizo cha #UgandaDecides na # UGDebate16. Kiwango cha Waganda cha ushiriki wa raia kwenye mtandao kilichochewa na midahalo ya rais ya kwanza kabisa kuwahi kurushwa na runinga, wa kwanza ambao ulifanyika mnamo Januari na wa pili, wiki moja baadaye.
Licha ya ufungwaji wa mitandao ya kijamii, Waganda wengi waliendelea kutuma taarifa kuhusu uchaguzi kwa kutumia anwani ya mtandao binafsi inayofahamika kama VPN. Siku ya uchaguzi, raia waliweza kushiriki yaliyokuwa yanajiri kuhusu kucheleweshwa kwa vifaa vya kupiga kura katika vituo mbali mbali, visa vya udanganyifu katika uchaguzi, na matokeo ya muda ya uchanguzi kwenye mitandao ya kijamii.
Wanaharakati wa haki za binadamu wanasema kwamba ufungwaji wa kimkakati wakati wa uchaguzi hupunguza kasi ya mawasiliano, wakati tu upatikanaji wa habari na usemi wa raia unahitajika sana.
“Kufungwa kwa mtandao kunazuia watu kuzungumzia mambo fulani yanayowaathiri, kama vile afya, mwingiliano na marafiki na pia kubadilishana maoni ya kisiasa,” Moses Owiny, afisa mkuu wa the Center for Multilateral Affairs, jukwaa huru la uchambuzi wa sera linalofanya shughuli nchini Uganda na Tanzania, aliiambia Global Voices katika mahojiano.
Kwa mujibu wa Owiny, ufungwaji hukusudia kuzuia upinzani katika siasa kwa misingi ya “hofu ya serikali kwamba maoni ya raia yanaweza kuchochea umma,” madai ambayo anaamini hayana msingi kiuhakika ila ni ya kudhaniwa.
Historia ya Uganda kufunga majukwaa ya mitandaoni na tovuti
Mnamo Aprili 14, 2011, UCC iliagiza watoa huduma za mtandao (ISPs) kufunga kwa muda ufikiaji kwa Facebook na Twitter kwa saa 24 ili kuondoa uunganishwaji na ubadilishanaji habari. Agizo hilo lilitolewa wakati wa maandamano motomoto ya “walk to work” yaliyoongozwa na upinzani kufuatia kupanda kwa bei ya mafuta na chakula. Mamlaka hiyo ya mawasiliano ilisema kwamba vyombo vya usalama viliomba ufungwaji wa matumizi ya mitandao ya kijamii ili kuzuia vurugu.
Mnamo mwaka wa 2011, uchaguzi ulikumbwa na uchujwaji wa ujumbe mfupi (SMS) wenye maneno fulani yakiwemo “Egypt”, “bullet” na “people power.”
Kuelekea uchaguzi mkuu wa 2006, UCC iliagiza watoa huduma za mtandao (ISPs) kuzuia upatikanaji wa wavuti ya Radio Katwe kwa kuchapisha habari “mbovu na za uongo’ dhidi ya chama tawala cha National Resistance Movement na mgombea wake wa urais,” kwa mujibu wa chapisho la sera ya tehama la 2015 la Collaboration on International ICT Policy for East and Southern Africa (CIPESA).
Mamlaka ya Uganda ilizuia upatikanaji wa matangazo ya kituo hicho cha redio na wavuti wa the Daily Monitor kwa kuchapisha “matokeo huru ya uchaguzi.” Majukwaa haya yalirejeshwa kwa haraka lakini tu baada ya tume ya uchaguzi kutangaza matokeo rasmi.
Uchaguzi wa 2021: Mbinu zile zile?
Tangu mwaka wa 2016, utawala umeendelea kuwakamata wanasiasa wa upinzani na waandishi wa habari.Robert Kyagulanyi, almaarufu kama “Bobi Wine,” mwimbaji na kiongozi wa chama cha upinzani cha People Power, ambaye pia ni mbunge, tayari ametangaza azma yake ya kuwania urais. Bobi Wine kwa sasa anakabiliwa na mashtaka ya jinai kwa “kumuudhi rais” na ikiwa atapatikana na hatia, hataruhusiwa kuwania.
Kwa mujibu wa Human Rights Watch, mnamo 2018 utawala uliwalilenga wabunge sita wa upinzani wakiwemo Bobi Wine na Francis Zaake, kabla ya uchaguzi mdogo wa Agosti 15 huko Arua (kaskazini mwa Uganda). Polisi na jeshi walilikamata kundi hilo pamoja na watu wengine 28 mnamo Agosti 13, 2018, na kuwashtaki kwa uhaini. Baadaye waliachiliwa kwa dhamana.
Siku hiyo hiyo, polisi pia waliwakamata waandishi wa habari wawili, Herber Zziwa na Ronald Muwanga, walipokuwa wakiripoti kuhusu uchaguzi na vurugu zilizohusiana na uchaguzi huo, ikiwemo mauaji mabaya ya kufyatuliwa risasi dereva wa Bobi Wine yaliyotekelezwa na jeshi.
Read more: #FreeBobiWine: Protests mount over torture and arrest of a young political force in Uganda
Wakati uchaguzi wa 2021 unapokaribia, kuna uwezekano mkubwa kuwa utawala wa Uganda utaendeleza ukandamizaji wa wapinzani, ikiwa ni pamoja na kufunga mitandao ya kijamii. Kwa kweli, tangu uchaguzi wa 2016, hakujakuwepo na mabadiliko katika mfumo wa kisheria ambao unaruhusu serikali kuzuia haki ya uhuru wa kujieleza na ufikiaji wa habari mtandaoni.
Kwa mujibu wa 2016 State of Internet Freedom in Africa report, Sheria ya Mawasiliano ya 2013 inaipa UCC nguvu zaidi na inafanya kazi chini ya kifungu cha 5 kinachoruhusu mdhibiti wa mawasiliano “kufuatilia, kukagua, kutoa leseni, kusimamia, na kudhibiti huduma za mawasiliano” na “kuweka viwango, kufuatilia, na kutekeleza uzingatifu unaohusu taarifa.” Kwa ombi la serikali, UCC ilitumia sehemu hii kuagiza watoa huduma za mtandao (ISPs) kuzuia ufikiaji wa mitandao ya kijamii na huduma za pesa kwa njia ya simu wakati wa uchaguzi wa 2016.
Serikali inaendelea kutumia sheria hizi kudhibiti mijadala ya umma na kunyamazisha wapinzani wa kisiasa, haswa wakati wa uchaguzi.
Owiny anatoa hoja kwamba serikali ina uwezo wa kuzima mtandao wakati wowote ule inapoonekana kuna umuhimu huo: “Pale ambapo usalama wa serikali na ule wa raia wake unaingiliana, na pale usalama wa serikali unapotishiwa, usalama wa serikali na uponaji wake utapewa kipaumbele.”
Asasi zisizo za kiserikali na watetezi wa haki za binadamu wamekuwa wakijiandaa nchini Uganda ili ufungaji kama ule uliofanyika mwaka wa 2016 hautokei tena.
Asasi kadhaa ziliandika barua ya pamoja kwa Jumuiya ya Afrika na mashirika ya kikanda zikiyaomba kulaani uamuzi wa utawala wa Uganda wa kufungia ufikiaji wa mtandao wakati wa uchaguzi wa 2016.
Shirika la Unwanted Witness Uganda liliipeleka serikali ya Uganda mahakamani, pamoja na watoa huduma za mtandao (ISPs) na mdhibiti wa mawasiliano (UCC), katika kesi iliyowasilishwa mnamo Septemba 2016. Shirika hilo lilionyesha kwamba hatua ya ufungwaji wa mtandao iliyopangwa na serikali ilikiuka haki za raia wa Uganda za uhuru wa kusema na kujieleza kama inavyoelezwa kwenye kanuni za kifungu cha 29 (1) cha katiba ya 1995. Hata hivyo, jaji alitoa uamuzi kwamba “upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha ukiukwaji wowote” uliotokana na ufungwaji huo, Unwanted Witness ililiambia shirika la Global Voices.
Kufanikisha kutokatishwa kwa ufikiaji wa mtandao – hasa wakati wa uchaguzi ujao – kutahitaji utetezi zaidi.
Owiny alipendekeza hitaji la wanaharakati wa haki za dijitili kuongeza mazungumzo kati ya serikali na sekta binafsi kuwasilisha athari mbaya za ufungwaji kwa sababu sekta binafsi inatiwa hofu na serikali.
Uganda ilikuwa miongoni mwa nchi za kwanza barani Afrika kutunga sheria ya haki ya raia kupata habari za umma, inayojulikana kama Access to Information Act (ATIA), mnamo 2005. Sheria hiyo inaahidi kutoa “ufanisi, urahisi, uwazi na uwajibikaji” ambao “utawezesha umma kupata kwa urahisi na kushiriki katika maamuzi ambayo yanawaathiri kama raia wa nchi. “
Je! Serikali itatimiza jukumu lake la kukuza haki ya kupata habari? Na je! Itatimiza ahadi zake?
Makala haya ni sehemu ya mfululizo wa machapisho yanayochunguza kuingiliwa kwa haki za dijitali kupitia mbinu kama vile ufungwaji wa mtandao wa intaneti na upotoshaji taarifa wakati wa matukio muhimu ya kisiasa katika nchi saba za Afrika: Algeria, eEthiopia, Msumbiji, Nigeria, Tunisia, Uganda, na Zimbabwe. Mradi huu unafadhiliwa na Mfuko wa Africa Digital Rights Fund wa The Collaboration on International ICT Policy for East and Southern Africa (CIPESA).