Mashirika ya Kimataifa Yataka Kuachiliwa Huru kwa Mwanaharakati wa Haki za Ardhi Nchini Cambodia Tep Vanny

Watu wanaomuunga mkono Tep Vanny wanataka aachiliwe huru. Picha kutoka LICADHO, kikundi cha haki za binadamu Cambodia.

Angalau Asasi za kiraia 65 (CSOs) na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) kutoka duniani kote yametia saini tamko la pamoja likiitaka serikali ya Cambodia kumwachia huru mwanaharakati wa haki za ardhi Tep Vanny, ambaye amekuwa kizuizini kwa miezi 12.

Tep Vanny ni mwanaharakati wa haki za binadamu maarufu ambaye amekuwa akifanya kampeni kwa niaba ya wakulima wadogo na wamiliki wa ardhi waliondolewa katika maeneo yao nchini Cambodia. Alikamatwa Agosti 2016 kwa kuongoza maandamano ya ‘Jumatatu Nyeusi’ yaliyoandaliwa kwa ajili ya kudai kuachiliwa huru kwa wanaharakati wa haki za binadamu watano wanaotuhumiwa kwa kuingilia kesi ya serikali inayowahusu viongozi wa upinzani.

Mahakama ilimuhukumu Tep Vanny kwa kosa la “kutukana viongozi wa umma” kifungo cha siku sita gerezani. Lakini akiwa kifungoni serikali ilifufua kesi yake ya 2013 alipoongoza maandamano mbele ya nyumba ya waziri mkuu akipinga kuondolewa kwa wakazi wa ziwa Boeung Kak. Mradi wa serikali wa kuendeleza eneo la ziwa Boeung Kak, lililo katika mji wa Phnom Penh, umewahamisha maelfu ya wakazi waliokuwa wanaishi katika eneo hilo.

Hapo Februari 23, 2017, Tep Vanny alikutwa na hatia kwa kufanya “kosa kwa kukusudia la kuchochea hali hiyo” wakati wa maandamano ya 2013 na amehukumiwa kifungo cha miaka miwili na miezi sita gerezani.

Hapo Agosti 8, 2017, mahakama ilithibitisha uamuzi wa kumtia hatiani Tep Vanny. Pia iliripotiwa kuwa Tep Vanny anaweza kukutana na shtaka la tatu kwa kufufuliwa kwa kesi nyingine inayohusiana na maandamano ya jamii ya Ziwa Boeung Kak hapo 2011.

Kuongezeka kwa muda wa Tep Vanny kuwa kizuizini kunaonwa na baadhi ya wanaharakati kama sehemu ya mpango wa serikali kunyamazisha wapinzani na kueneza hofu miongoni mwa watu kuelekea uchaguzi mkuu hapo 2018. Chama tawala cha Cambodia kimekuwa madarakani kwa miongo mitatu sasa, lakini kilipoteza idadi kubwa ya viti katika uchaguzi wa 2013.

Tamko la pamoja lililosainiwa na asasi za kiraia na mashirika yasiyo ya kiserikali (CSOs naNGOs) limeonya kuwa kizuizi cha Tep Vanny “kimechangia hali ya hofu kwa wanaharakati wa haki za binadamu Cambodia yote.” Pia limesisitiza kuwa upinzani na harakati za amani zisifanywe kuwa ni uhalifu:

Kama matokeo ya kufungwa kwake, Tep Vanny anazuiwa kufanya kazi yake ya amani na ya thamani kama mwanamke mpigania haki za binadamu. Maandamano ya amani na matamko ya upinzani sio uhalifu, na wapigania haki za binadamu wasifungwe kwa kutumia haki zao za binadamu.

Jukwaa la Haki za Binadamu na Maendeleo la Asia limekumbusha kuwa mashtaka ya Tep Vanny yamekiuka taratibu za kimataifa:

Mashtaka yaliyotengenezwa dhidi ya Tep Vanny na kizuizi holela ni majaribio yaliyochochewa kisiasa kunyamazisha na kumzuia harakati zake kama mpigania haki za binadamu. Kesi yenyewe haikufikia vigezo vya kimataifa vya mashtaka ya haki.

Pamoja na vikundi vya haki za binadamu vya nyumbani, wanaharakati na wakazi wa ziwa Boeung Kak wamekuwa wakiomba ofisi za mashirika ya Umoja wa Mataifa na balozi mbalimbali nchini Cambodia kuishurutisha serikali imwachie huru Tep Vanny.

Watumiaji wa mitandao ya jamii nchini Cambodia pia wamehamasishwa kuweka picha za alama ya kampeni katika kurasa zao mtandaoni. .

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.