Liberia Kukabidhi Elimu ya Msingi kwa Mwekezaji Binafsi wa Kimarekani

Students in Bong County, Liberia, study by candlelight. These students missed school during Liberia's civil war. Public Domain photo by United States Agency for International Development (USAID).

Wanafunzi kwenye Kaunti ya Bong, Liberia, wakisoma kwa kutumia mshumaa. Wanafunzi hawa walikosa masomo wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Liberia. Picha ya Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID)4. Inaweza kutumiwa bila ruhusa.

Liberia inaelekea kuvunja rekodi ya kuwa nchi ya kwanza kufanya jambo jipya barani Afrika. Nchi hiyo ilikuwa ya kwanza barani Afrika kuongozwa na rais mwanamke baada ya Ellen Johnson-Sirleaf kuchaguliwa kuwa rais mwaka 2006.

Hivi sasa, nchi hiyo iko mbioni kutekeleza kile ambacho baadhi ya watu wanakiita jambo jingine la kwanza kuwahi kutokea barani Afrika: kukabidhi mfumo wake wote wa elimu ya awali na msingi kwa mwekezaji binafsi wa Kimarekani.

Kwa kiwango kikubwa elimu nchini Liberia iliathiriwa na Vita vya Kwanza vya Wenyewe kwa Wenyewe na Vita vya Pili vya Wenyewe kwa Wenyewe kati ya 1989 na 2003.  Inakadiriwa kwamba asilimia 50 ya wasichana na asilimia 68 ya wavulana wamehitimu elimu ya msingi au, kama sivyo, wanaweza kusoma sentensi kamili. Hali ilikuwa mbaya zaidi wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa Ebola.

Waziri wa Elimu wa Liberia George Werner alitangaza mwezi Januari 2016 kwamba elimu ya awali na msingi itakabidhiwa kwa kampuni binafsi ya Kimarekani iitwayo Bridge International Academies, kwa kipindi cha miaka mitano. Serikali ya Liberia italipa zaidi ya dola za Kimarekani milioni 65.

Kampuni hiyo ya Bridge International Academies inajieleza kama kampuni kubwa zaidi duniani katika uboreshaji wa elimu, hivi sasa inaendesha shuguli zake nchini Kenya na Uganda. Mbinu za ufundishaji zinazotumiwa na kampuni hiyo zinawalenga zaidi walimu –ambao hawalazimiki kuwa na cheti cha ualimu ambao hupatiwa mafunzo ya majuma matano — kujifunza namna ya kufundisha kwa kutumia mwongozo wa kipindi unaokuwa umewekwa kwenye vifaa maalumu mfano wa simu kubwa (tablet). Ukubwa wa darasa unaweza kufikia wanafunzi 60 kwa darasa.

Tofauti na uendeshaji wa shule za kampuni hiyo zilizoko Kenya na Uganda, ambapo wazazi wa wanafunzi hulipa ada inayofikia dola 6 kwa muhula mmoja wa masomo, wazazi nchini Liberia hawatalipa chochote kinachohitajika shuleni kutoka mifukoni mwao.

Hatua hiyo imeibua ukosoaji mkali kutoka sehemu mbalimbali duniani na hata ndani ya nchi hiyo. Wataalam wa elimu wanapanga kuishinikiza serikali ya Liberia kusitisha mpango wake huo.

Akipinga mpango huo, Kishore Sing, Mwandishi Maalum wa Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya kupata elimu, alisema kwenye taarifa yake kwa vyombo vya habari mwezi Machi:

Ni dhahiri kwamba Liberia haina raslimali za kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kutoa elimu ya msingi bure kwa kila mtoto, lakini inaweza kutafuta kiasi kikubwa cha fedha kuingia mkataba na kampuni binafsi ili kutoa elimu kwa niaba yake.

Akiandikia jarida la afrika Kusini Mail & Guardian, Christine Mungai alihoji  kwamba mbinu za ufundishaji zinaotumiwa na kampuni ya Bridge International Academies zinazuia mwalimu na mwanafunzi kubadilishana maarifa na hivyo “hazikuzi uwezo wa mwanafunzi kuchambua mambo.” Kadhalika aligusia madai ya kampuni hiyo kuwa wanafunzi wake wanafanya vizuri zaidi kuliko wenzao walio kwenye shule za serikali, akionesha kwamba matokeo hayo ya utafiti yalifadhiliwa na kampuni hiyo.

Hata hivyo, kubinafsishwa kwa elimu ya msingi kwaweza kuwa fursa nzuri kwa Liberia, ambayo hivi sasa mfumo wake ‘una matatizo mengi,” anakiri:

Kwa hivyo, mfumo wa elimu, unaotengenezwa kwa misingi ya uwajibikaji, uhakiki wa ubora wake, uchambuzi makini, na mabadiliko ya kisera yanayofanywa kwa kutumia matokeo ya utafiti -hata kama ni za watu binafsi – ni bora zaidi kuliko aina ya elimu iliyopo Liberia hivi sasa.

Akijibu habari hizo, Jan Resseger, mtaalam wa elimu ya umma nchini Marekani na mwanablogu, alihoji nia ya wawekezaji wa kampuni hiyo, ambao ni pamoja na Shirika la Fedha la Kimataifa, ambalo ni sehemu ya Makampuni ya Benki ya Dunia:

Lazima mtu asaili nia hasa ya wale wanaoitwa wawekezaji wanaosemekana kuwa nyuma ya shughuli za kampuni ya Bridge International Academies, kwa mfano Bill Gates na Mark Zuckerberg. Je, makampuni haya ya kiteknolojia ya hisani yanasaidia kweli ukuaji wa elimu ya duniani kama sehemu ya misaada yake ya kibinadamu kwa watu au lengo ni kupanua soko la dunia kwa tekenolojia ya elimu iliyotengenezwa kwa ajili ya kujitengenezea faida binafsi?

Ripoti ya Ufuatiliaji wa Elimu ya Dunia, inayochapishwa na UNESCO, ilionesha wasiwasi kwa suala hili:

Kuzifikiria shule kama sehemu tu ya kujifunza kusoma inaweza kuonekana kuwa wazo jema kwa nchi ambayo watoto wake wengi hawawezi kufikia angalau hatua hiyo. Hata hivyo, hatari yake ni kupoteza lengo halisi la elimu. Watunga sera wanahitaji kutambua kwamba ufundishaji mzuri hauwezi kufanywa na yeyote kwa kutumia mwongozo wa somo lililoandaliwa tayari na mtu mwingine

Chama cha Walimu nchini Liberia, miongoni mwa mashirika mengine ya kiraia, limetuma barua kwa Waziri wa Elimu wa Liberia George K. Werner kikielezea masikitiko yake kwamba mpango huo wa kubinafsisha elimu unaleta ‘hatari kubwa’ na ni ‘kufanya elimu iwe huduma ya kibiashara nchini Liberia.’ Wengine, wakati huo huo, wametoa maoni yao kwenye mitandao ya kijamii:

Ni jambo la kusisimua. Upuuzi.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.