Ndege ya Malaysia ya MH17, iliyokuwa ikisafiri kutoka Amsterdam kwenda Kuala Lumpur, imeanguka mashariki mwa Ukraine jioni ya Alhamisi, ikiwaua abiria 298 pamoja na wafanyakazi waliokuwepo ndani.
Taarifa nyingi zinaonyesha kwamba ndege hiyo ilitunguliwa na silaha umbali wa kilimeta 50 kutoka kwenye mpaka wa Urusi na Ukraine. Serikali y Ukraine inawatuhumu wapinzani wanaoungwa mkono na Urusi kutumia silaha kali kuitungua ndege hiyo lakini viongozi wa waasi wanakana madai hayo.
Picha ya mchoro inaonesha njia ya ndege hiyo na eneo ilikoangukia ndege ya MH17:
Infographic: Crashsite Map incl. MH17 Flight Path – pic.twitter.com/JkPwUJAv8u
— Florian Witulski (@vaitor) July 18, 2014
Picha ya mchoro: Ramani ikionesha eneo ilikoanguka ndege ikiw ni pamoja na njia ya ndege MH17
Waziri Mkuu wa Malaysia Najib Razak aliwahakikishia wananchi wake kwamba wale waliohusika kuitungua ndege hiyo watapelekwa kwenye mkono wa sheria:
Leo ni siku mbaya, katika mwaka ambao tayari ni mbaya, kwa Malaysia.
Kama itajulikana kuwa ndege hiyo ilitunguliwa kwa hakika, tunasisitiza kwamba waliohusika wanakabiliana na mkono wa sheria.
Abiria wa ndege hiyo na wafanyakazi walitoka katika nchi mbalimbali.
Lakini leo, bila kujali uraia, wote tuko pamoja kuomboleza.
Alifafanua kwamba njia ya ndege hiyo angani, hata kama ilikuwa inapita juu ya eneo lenye mgogoro, ilitangazwa kuwa salama na Shirika la Kimataifa la Safari za Anga.
Kuanguka kwa ndege MH17 kumekuja katika kipindi kifupi ambacho bado dunia inakumbuka kupotea kwa Ndege ya shirika la Malaysia Boeing 777-200 mwaka huu. Mnamo Machi 8, ndege ya Malaysia MH370 iliyokuwa na watu 237 ndani yake ilipotea saa moja tu baada ya kupaa kwenye uwanja wa Kuala Lumpur wakati ikisafiri kuelekea Beijing. Ndege ya MH370 na abiria wake bado hawajulikani walipo.
Binti wa mfanyakazi wa ndege hiyo MH370 alitwiti kuwafariji ndugu na marafiki wa abiria wa ndege ya MH17:
As the family member of the crew MH370, and on behalf of all them, we pray for MH17. Stay strong dear families. #PrayForMH17
— Maira E. (@Gorgxous_) July 17, 2014
Nikiwa mwanafamilia wa mfanyakazi wa ndege MH370, na kwa niaba ya wote, ninawaombea abiria wa ndege MH17. Muwe na moyo mkuu rafiki zangu.
Josie Fernandez wa shirika la Kimataifa la Uwazi Malaysia alitoa wito wa uchunguzi wa kina wa ajali hiyo:
Kilichotokea hakikubaliki – Malaysia ni nchi pekee ambapo shirika hilo hilo, aina hiyo hiyo ya ndege zimehusika kwenye majanga yanayopoteza maisha ya watu wengi ndani miezi michache. Ndege MH370 haijapatikana.
Malaysia lazima iombe kuchukuliwa kwa hatua za Kimataifa kwa janga hili lisilokubalika. Ndege hii ilikuwa ya abiria. Hatuko vitani na taifa lolote.
Akiandikia gazeti la The Ant Daily, Alyaa Alhadjri alilieleza tukio hilo la kutunguliwa kwa ndege ya MH17 kama ‘mauaji ya halaiki’:
Kwa nini abiria wa ndege ya kibiashara waruhusiwe kupita kwenye eneo lenye mgogoro ambapo ndege zimekuwa zikitunguliwa na walitahadharishwa kusafisha anga.
Kwa sababu yoyote iliyosababisha kuanguka kwa ndege ya Shirika la Ndege la Malaysia Boeing 777 kwa mara ya pili ndani ya siku, na kupoteza watu 537 katika majanga mawili ya anga, haisaidii kuinua imani ya wasafiri kwa shirika hilo la ndege.
Wakati Malaysia ikiomboleza kufuatia ajali nyingine ya ndege, inaonekana kuwa raia wengi wataendelea kuishinikiza serikali kueleza hali hiyo ya ‘sintofahamu’ iliyosababisha kupotea kwa kwa ndege MH370.