Timu ya Rais wa Zambia, Michael Sata ilipotoa picha hizo zinazosemekana kuwa ni za kikao cha baraza la Mawaziri kwa vyombo vya habari vya nchi hiyo na kuzichapisha kwenye ukurasa wa Facebook, lengo lilikuwa kumaliza madai kwamba kiongozi huyo ni mgonjwa na hajawa akifanya kazi.
Badala yake, picha hizo zilikuwa mithili ya mafuta yaliyoongezwa kwenye moto unaowaka, kiasi kwamba baadhi hata wanathubutu kuhoji uhalisi wa mkutano huo kwa sababu hapakuwa na kipande cha rekodi ya sauti na video kuthibitisha madai hayo.
Mambo yalianza wakati Sata alipoondoka nchini kimya kimya mnamo Juni 20, 2014. Tovuti ya Zambian Watchdog ilitoboa siri hiyo, ikiripoti kuwa rais alikuwa amewasili nchini Israel na alikuwa amelazwa hospitali. Msemaji mkuu wa serikali alilazimika kuthibitisha safari hiyo, lakini alisema Sata alikuwa mapumzikono nchini Israel.
Usiri unaozunguka safari hiyo uligeuka kuwa kosa kubwa lililosababisha maneno yasiyothibitishwa ambayo kwa haraka yalisambaa kwenye vijiwe vya mazungumzo. Siku kadhaa baada ya safari ya Sata, ulinzi na itifaki ya kirais na bendera ya rais yenye nembo ya taifa, vyote ambavyo vilipaswa kuondolewa wakati rais asipokuwepo, viliendelea kuwepo ikulu ya rais kwenye wilaya ya kati ya jiji hilo.
Takribani mwezi mmoja baadae, wa-Zambia hawakuwa wanajua lolote kuhusu ikiwa rais wao, ambaye kwa miezi iliyopita alionekana kuwa mdhaifu, alikuwa amerudi ama la. Zambia Reports na mwanasheria aliye mwanasiasa pia Sakwiba Sikota alihoji bandiko la mwisho kwenye mtandao wa Facebook wa rais kuwa limekuwepo tangu tarehe 6 Juni –inatia shaka kwa sababu ukurasa huo umekuwa ukihuishwa mara kwa mara.
Zambia Reports iliandikwa kuhusu kukosekana habari mara kwa mara kwenye ukurasa huo wa rais:
Inaonekana kila mmoja ametelekeza posti zake na hatimizi wajibu. Si jambo la kawaida kwamba bada ya ‘kuufurikisha’ ukurasa wa facebook kwa habari za karibu kila saa tena kila siku kwenye ukurasa wa Rais wa Facebook, hapajakuwepo na habari zozote tangu Juni 6
Kuhusu kukosekana kwa mabandiko kwenye ukurasa wa Facebook wa Sata, Sikota anabaini kwa hali ya masihara:
Kuna mambo kwenye maisha ambayo ni matamu sana kiasi kwamba huwezi kuyachoka. Nadhani sote tunakumbuka tulivyoonja asali kwa mara ya kwanza na mengineyo mazuri. Moja ya jambo tamu na zuri ni chakula cha mara kwa mara tulichokuwa tukilishwa na kukizoea ni kile cha mhe rais Michael Sata, mtu wa watu na mpenda watu. Nani anaweza kusema kasahau zile habari motomoto na za kibinafsi zilizokuwa kwenye ukurasa wa Facebook wa Mheshimiwa?Nyingi zilikuwa ni kama ile iliyotufahamisha kuhusu kila anakokwenda, iliyowekwa April 4 mwaka huu iliyosomeka, “Habari za asubuhi marafiki, nimeanza safari ya kurudi baada ya mkutano wenye mafanikio wa ushirikiano kati ya Umoja wa Ulaya na Afrika uliofanyika Brussels, Ubeligiji. Nimeshaondoka Brussels kuja Lusaka kupitia Amsterdam. Kaeni vyema na furahieni mwisho mwema wa wiki. MCS [Michael Chilufya Sata] -04/04/14″
Siku mbili baadae, picha zinazosemekana kuwa za kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika Julai 14 zilziotumwa kwenye vyombo vya habari na kuchapishwa kwenye mtandao wa Facebook ziligeuka kuwa mradi wa nchi nzima. Kituo cha runinga cha, Muvi, na hata BBC walionesha mashaka na kikao hicho.
Mwanablogu Chola Mukanga, kwenye blogu yake ya Zambian Economist aligoma kuzitumia picha hizo, akisema:
Kwa bahati mbaya, blogu ya Zambian Economist haijaweza kuthibitisha uhalisi wa picha hizo tatu, ambazo tunaelewa ziko kwenye tovuti nyingine. Ni kwamba hatuna rekodi ya sauti wala video zinazothibitisha picha hizo. Kwa hiyo itakuwa ni kutokuwa makini kwetu kuonesha picha hizo na kuzipachika alama ‘rasmi’ kwa sababu hiyo inaweza kuupotosha umma.
Kwenye mtandao wa Twita, raia walipima uzito wa kukosekana kwa Sata:
So it seems despite publication of pics of “Pres Sata chairing a cabinet meeting” yesterday #Zambia is still asking #whereisthepresident?
— Laura Miti (@LauraMiti) July 15, 2014
Kwa hiyo inaonekana pamoja na kuchapishwa kwa picha za Rais Sata akiongoza kikao jana #Zambia bado inauliza yuko wapi rais?
Mtumiaji mwinine alishangaa kwa nini alipokuwa nje ya nchi hapakuwa na habari zilizokuwa zinakuja:
To what extent should the Presidency be shrouded in mystery? #Zambia http://t.co/nvm5yv5ntN
— Tchiyiwe T Chihana (@AfriWoman) July 12, 2014
Kwa kiwango gani rais anapaswa kuzungukwa na usiri?
Hasira ni hatia:
@AfriWoman This government is taking voters for granted. Sata and his cabal are accountable to the people of Zambia not other way round.
— David Mwanambuyu (@mbuyujr) July 12, 2014
Serikali hii inawachukulia wapiga kura kirahisi. Sata na baraza lake wanawajibika kwa watu wa Zambia na si kinyume chake
Kuhusu kutokuwepo kwa Sata, mwanaharakati Brebner Changala aliiomba Mahakama Kuu kulilazimisha Baraza la Mawaziri kuunda jopo la madaktari kuchunguza afya ya Sata na kubaini ikiwa anafaa kuendelea na kazi kama Mkuu wa Nchi. Ombi hilo lilitupiliwa mbali lakini Changala alirudisha tena ombi hilo hilo Mahakamani.
Siku chache baadae kabla ya kinachodaiwa kuwa kikao hicho, jarida la Afrika Kusini la Business Day lilionyesha mtiririko wa safari za siri za Sata nje ya nchi, ambazo ziliitwa na ofisi ya Rais na maafisa wengine wa serikali kuwa ni likizo la kikazi. Kwa kupitia kwa haraka ukosoaji wa habari hiyo kwenye mitandao ya kijamii, inaonekana kuwa kilichokuwa kikisemwa na maafisa hao wa serikali kilikuwa kinafanya kazi.