Je, Ziara ya Obama Barani Afrika ni Neema au Hasara?

Rais wa Marekani Barack Obama amemaliza ziara yake ya siku sita katika nchi tatu za Kiafrika, Senegali, Afrika Kusini na Tanzania, mnamo Julai 2, 2013. Maoni ya watu duniani kote kuhusiana na umuhimu na matokeo ya ziara hiyo, yameonyesha kugawanyika mno.
Wakati wa ziara yake, Obama alitangaza mradi mpya, “Umeme kwa Afrika”, kwa lengo la kukuza matumizi ya umeme mara dufu katika nchi zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara. Kupitia mradi huu, Marekani inaahidi kutoa Dola za Kimarekani bilioni saba wakati makampuni ya sekta binafsi yanatoa zaidi ya bilioni tisa kwa mradi huo.

Kwa mujibu wa blogu ya Ikulu ya Marekani, karibu asilimia 70 ya Waafrika hawajafikiwa na huduma ya umeme.

Image of President Barack Obama on a billboard in Dar Es Salaam. Photo courtesy of Sandy Temu.

Picha ya Rais Barack Obama katika bango kubwa barabarani kumkaribisha jijini Dar Es Salaam. Picha ya mtumiaji wa Instagram Sandy Temu.

Akitoa maoni yake kuhusu mradi huo wa umeme, Bright Simmons wa mtandao wa African Argumentalipongeza wazo hili jipya la ushirikiano wa kimkakati baina ya Marekani na bara la Afrika:

Kama mmoja wa watu waliolalamika sana siku za nyuma kuhusu kilichoonekana kuwa kukosekana kwa mawazo mapya ya “ushirikiano wa kimkakati na Afrika” kutoka Ikulu ya Obama, ninauona mpango wa nishati kuwa na mwelekeo sahihi.

Jambo lenyewe lililochaguliwa -changamoto ya umeme barani Afrika- linao umuhimu mkubwa. Benki ya Dunia kwa mfano inasema kwamba nchi zote za Kusini mwa Jangwa la Sahara, ukiiacha Afrika Kusini, kwa pamoja hazizalishi umeme wenye mkondo mkubwa kuliko nchi moja tu ya Argentina. Ukiijumuisha na Afrika Kusini, kiasi cha umeme kinachozalishwa kinafikia kile cha Uhispania.

Ni jambo la kupongezwa kwamba Ikulu ya Marekani inaahidi mpaka Dola za Marekani bilioni 7 kama msaada wa nyongeza kutoka kwenye mashirika yake yenye mrengo wa kusaidia nchi za nje -EXIM na OPIC – kwa sababu hii.

Nina uhakika kwamba Ikulu ya Marekani inaelewa kwamba hata kama kiasi hiki chote kitatolewa katika kipindi cha mwaka mmoja, na kuna uwezekano kwamba kitatolewa kwa kipindi cha miaka 3 mpaka 5, hakitaweza kutosheleza mahitaji ya kiasi cha dola bilioni 23 zinazohitajika kwa mwaka kuwekeza katika nishati ya umeme barani kote.

Daniel McLaughling alijibu makala hiyo akihoji kwamba kumaliza ukiritimba katika huduma ya umeme ndilo haswa suluhisho linaloweza kuleta matokeo yanayoeleweka:

Kama hawa jamaa wanamaanisha kwa dhati kutatua tatizo la umeme barani Afrika, ni lazima wapiganie suluhisho pekee linaloweza kuleta matokeo halisi: kuachana na ukiritimba wa huduma ya umeme. Inanishangaza kwamba, pamoja na mazungumzo yote kuhusu kuongeza uzalishaji wa umeme, hakuna anayetaka kukiri kuona kuwa inawezekana kabisa kuwa ukiritimba wa serikali na vitendo vya ufisadi ni tatizo, na kwamba mabilioni yanayokwenda serikalini yanakuza ufisadi tu, yakisaidia walengwa kwa kiasi kidogo sana. Fungueni masoko kwa ushindani na biashara za faida na mtaona uwekezaji mkubwa na matokeo yake huduma hiyo itaongezeka kuwafikia watu wengi zaidi.

Joel B. Pollak alikuwa na maoni kuwa Mradi wa “Nishati kwa Afrika” hautazalisha umeme mwingi kama inavyoahidiwa:

[…] Mradi wa “Umeme kwa Afrika” hautazalisha umeme kwa kiasi kingi kama inavyoahidiwa, labda sana utatunisha tu mifuko ya watu wenye uhusiano na wanasiasa wa pande zote mbili, Marekani na Afrika. Wakati huo huo, China, ambayo haionekani kujali kama Waafrika wanaendesha magari na kuishi katika nyumba bora zenye viyoyozi, itaendelea kuwekeza barani Afrika kwa namna ambayo itakuza kweli uchumi wa Afrika, ikiishinda Marekani katika mipango yenye mustakabali bora wa kiuchumi barani Afrika.

Siddhartha Mitter alibaini kwamba “uwekezaji katika miundo mbinu ni jambo linalopaswa kuwa jema isipokuwa ikithibitika vinginevyo – hasa Afrika”:

Kwa sasa, uwezo na uzalishaji wa nishati barani kote ni karibu sawa na ule wa Ujerumani na Kanada. Ukiondoa Afrika Kusini na Misri, unabakiwa na GW 63 zinazotoa kWh bilioni 260, zaidi kidogo ya Australia au Irani. Katika mukhtadha huu, kama awamu ya kwanza ya mradi huu wa “Umeme kwa Afrika” itafanikiwa kufikia malengo yake ya kuongeza GW 10 za uwezo wa uzalishaj na kuwaunganisha wateja milioni 20 wa nyumbani na wa kibishara, itakuwa ni ukuaji mkubwa ambao hata hivyo haitakuwa mara dufu ambalo, kwa mjibu wa mkakati wa Ikulu ya Marekani kwa mradi huo, ndilo lengo kuu la mradi. Kwa hakika, mkakati huo huo unakadiria kwamba inagharimu dola za Marekani bilioni 300 kufikia kiwango cha kila mtu kupata huduma ya umeme barani kote ifikapo mwaka 2030.

Pamoja na shamra shamra nyingi [sw] zilizoonyeshwa na raia wa nchi hizo tatu, blogu ya Shadow Government ilionyesha ziara hiyo haikuwa na faida yoyote kubwa:

Lakini pamekuwa na udhaifu katika ziara hiyo: kwa mfano, matamshi yake (Obama) akiwa Afrika Kusini wakati wa mkutano na wanahabari akiwa na Rais Jacob Zuma. Rais huyo alitoa maoni ambayo ninayachukulia kuwa maoni yasiyofikiriwa ipasavyo, labda yalitegemewa kuishia kuwa kichekesho, kuhusu vyombo vya habari. Aliwaita wanahabari wa Marekani kama “waandishi wangu,” na kuwazuia kuuliza maswali mengi. Kwa kawaida, huenda, hili lisingekuwa jambo kubwa. Lakini kwa sababu alikuwa anatembelea nchi tatu za Afrika ambapo vyombo vya habari vinaonekana “kutokuwa huru,” ninadhani si tu matamshi yale ni namna mbaya bali ni hatari kwa serikali yake inayojinadi kupigania demokrasia. Ni kweli sitarajii rais aitumie ziara yake kama fursa ya kuwakosoa wenyeji wake moja kwa moja. Lakini ningetarajia kwamba wakati huu ambapo yeye, mwenyewe, anatazamwa kwa jicho la wasiwasi namna anavyowachukulia wanahabari (masuala ya kupeleleza simu na yale ya James Rosen wa Fox News), asingeweza kulipuuza hilo.

Kumekucha alimwita  Obama “Obama mkatili” kwa sababu ya kutokuzuru Kenya, nchi aliyozaliwa baba yake:

Wakati huu Obama anapotua Dar es Salaam na kucheza Bongo ‘Ohangla’ Flava [Bongo Flava ni jina la muziki wa Kitanzania wa Hip Hop na R&B], tunaweza kujihesabu kuwa tumeshamkosa na kubaki tukimwona kama fahari yetu ya taifa iliyokosa maana.

Mtu mwenye dharau namna gani kumwona anakesha mlango wa pili kwa jirani bila kujali maumivu anayowasababishia watu wake mwenyewe wanaomheshimu kupindukia. AIBU.

Sahau uchungu wote uliosikika kwa watu wakisema hatuhitaji kutembelewa na Obama. Ni kweli, matokeo ya kiuchumi kwa ziara hiyo yangeonekana baada ya muda, lakini je, ni kweli Nairobi haikosi kitu!

Obama kusingizia kesi za ICC ni kutuumiza kulikozidi kipimo hasa baada ya Kibaki kutangaza mapumziko ya kufurahia ushindi wake katika uchaguzi mwaka 2008. Zaidi, Watanzania wangeweza kumwaibisha kwa kumpa jina la mtaa kumtambua.

Video ya YouTube hapa chini iliwekwa na Ikulu ya Marekani ikimwonyesha Obama akighani kwa kufoka foka katika Kituo cha UKIMWI cha Desmond Tutu:

Akichambua mchango wa jumla wa Obama katika maendeleo ya Afrika, Tolu alimwona Obama kama mtu “apuuziaye mambo kwa namna chanya” anapomfananisha na mtangulizi wake Bush. Alieleza:

Serikali ya Bush imeaacha nyayo barani kote zaidi ya kutoa misaada. Serikali yake ilikuwa na nafasi muhimu katika kusainiwa kwa makubaliano ya amani yaliyomaliza miongo kadhaa ya vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudani, ilionyesha kutaka kumaliza vita katika eneo la Kongo, na ilisaidia kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Liberia, ikisaidia kuhakikisha Charles Taylor anaachia madaraka, na kisha akikamatwa na kushitakiwa. (Taylor mwenyewe amekuwa akishangaa kwa nini Bush mwenyewe hashitakiwi kwa “uhalifu” wake).

Katika historia hii ya Marekani, Obama anaonekana kama anayepuuzia mambo kwa mtazamo chanya. Kimoja tu alichokifanya na kikaonekana ni kuongezeka kwa vikosi vyake vya kijeshi barani Afrika, akiongeza vituo vya kijeshi, kuingiza vikosi vingi vya kijeshi kulinda amani. Alipochaguliwa kwa mara ya kwanza kulikuwa na shangwe barani kote, na huenda kwa matarajio yasiyo halisi kwamba angepigania maslahi ya Afrika katika uso wa kimataifa. Na kwa kweli katika ziara yake ya kwanza nchini Ghana, alitangaza kuwa alikuwa na “damu ya AFrika ndani yake”. Tangu wakati huo umbali wake na bara hili umekuwa bayana mno, ukisababisha shutma kwamba ameisaliti asili yake.

Lakini hii ni haki? Je, Obama ana jukumu maalumu kwa bara hili, kwa sababu ya asili yake? Huenda sivyo. Labda msisitizo kwa Obama kama rais mwenye asili ya Afrika unakosa mantiki. Kwa kuwa si kwa sababu za ushirikiano kwamba Rais wa Marekani anapaswa kulisikiliza bara la Afrika. Kuna sababu zaidi za kibinafsi, za kiuchumi na kisiasa vile vile.

Akiwa mtetezi wa haki za wanawake wa ki-Afrika Kusini, Jennifer Thorpe alibaini kwamba mazingira anayoiishi yanaathiri sana maisha ya wanawake kwa kiasi kikubwa. Kwa hiyo anaitazama “rekodi” ya Obama kwa utunzaji wa mazingira:

Tunajua Marekani ina “rekodi” mbaya kimazingira -mfano sahihi wa namna sheria zinazolinda mazingira hazina uzuri wowote kama zinavyoyaharibu mazingira hayo. Hivi karibuni Obama alibadili mtazamo wake, akisema angesitisha miradi yenye hatari kubwa kwa mazingira kama bomba la Keystone kama zingeonyesha athari mbaya za kimazingira.

Nchini Afrika Kusini, katiba inatoa haki kwa watu wote kuishi katika mazingira yasiyo na athari za kiafya. Lakini bado tunaona mara nyingi tathmini za athari za mazingira zinahakikisha kuwa makampuni yanafikia angalau kiwango cha chini kabisa cha utunzaji wa mazingira na sio kuhakikisha kuwa yanatunza mazingira na ardhi tunayoimiliki sote. Ninatarajia kwamba Rais Obama anapotathimini madhara ya Keystone kwa mazingira, anafanya hivyo kwa mtazamo mpana, na sio kwa mtazamo mwembamba wa viwango na mazoea. Ninadhani swali lapaswa kuwa rahisi -je uoto wa asili, uzuri, na ardhi itaboreshwa na mradi wa Keystone? Kama mtu aliyekulia Hawaai, najua anajua jibu la swali hili moyoni mwake.

Kwenye mtandao wa twita, Andrew Harding wa BBC (@BBCAndrewH) aliona haya:

@BBCAndrewH: #obama – Afrika haiwezi kuwa chanzo cha bidhaa ghafi kwa mtu mwingine.

Mr. Mabotja (@MelosoDrop_Line) alijibu twiti ya @BBCAndrewH kwa kusema:

@MelosoDrop_Line: @BBCAndrewH #Obama hajawahi kuonyesha kwamba Afrika ni duka la bidhaa ghafi…ameonyesha mabadiliko ya mtazamo wa jinsi hii

Dayo Olopade (@madayo) aliandika:

@madayo: Zaiara ya #ObamabaraniAfrika inaonekana kwa kile inachokifanya na kile isichokifanya. Utawala wa sheria unaziacha mbali nchi nyingi ambazo zingestahili.

Haru Mutasa (@harumutasa) anaonyesha kile ambacho baadhi ya Waafrika wanauliza:

@harumutasa: #obamabaraniafrika. Baadhi ya Waafrika wanauliza, “kipi kilichofanywa na rais huyu wa Marekani kwa ajili ya Afrika ambacho ni tofauti na marais wengine waliopita?”

Ashley Koen (@a_koen) alikuwa na wasiwasi na wananchi wasiona hatia waliofukuzwa katika jitihada za “kusafisha mji” -ni shughuli ya kawaida katika nchi nyingi za Afrika wakati mkuu wa nchi ya kigeni, hasa kutoka Ulaya na Marekani anapokuja, kwa wazururaji wa mitaani kuondolewa:

@a_koen: Je, biashara zilizoondolewa na wananchi wasio na hatia waliotupwa jela kwa kisingizio cha kusafisha mji wataendelea na maisha yao? #ObamabaraniAfrika

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.