Sudani: Watumia Mtandao Wathibitisha Tetesi za Kukatwa kwa Intaneti

Watumiaji wa mtandao wanafuatilia kwa karibu yanayoendelea ndani ya Sudani, kufuatia tetesi kwamba Serikali ya Sudani inakusudia kukata mtandao wa intaneti –hatua inayokumbushia jaribio la Misri kuwanyamazisha wanaharakati na kuthibiti mapinduzi ya Januari 25 pale ilipoondoa uwezekano wa watu kuwasiliana kwa mtandao wa intanenti mnamo Januari 27.

Kwenye mtandao wa twita, Ali Alhasani, raia wa Jordan aliripoti:

@_AHA: HABARI MPYA: Zinaripoti kwamba intaneti IMEKATWA nchini Sudan. Kama ni kweli basi Mungu awe nao kwa sababu hatutaweza kujua chochote kinachoendelea huko!

Masaa manne yaliyopita, mwandishi wa habari wa ki-Misri Salma Elwardany, ambaye anaripoti kutoka Khartoum, alitwiti:

@S_Elwardany: Habari zinadai kuwa serikali ya Sudan inaweza kukata mtandao wa intaneti

Katika kujiandaa na matarajio ya kukatiwa mtandao, huduma ya Kutwiti kwa kuongea maneno imetengenezwa. Rodrigo Davies alitwiti kuhusu suala hili:

@rodrigodavis: Mpendwa Sudani, kama Bashir atakata mtandao wa intaneti, twiti kwa kuongea maneno kwa kutumia +16504194196 au +390662207294 ‪#SudanRevolts‬ ‫#السودان_ينتفض

Mara tu baada ya tangazo hilo, watumiaji wa mtandao walianza kuambiana nani yungali mtandaoni nchini Sudan,

Sara Elhassan anaandika:

@BSonblast: @SudaneseThinker @Usiful_ME yuko Sudani na bado anatwiti

Na Israeli Elizabeth Tsurkov anaongeza:

@Elizrael: @JustAmira @SudaneseThinker Naona watu wengi bado wanatwiti kutokea Sudan nina mashaka kama ni kweli …jionee kwa @elizrael/sudanpeeps

Maandamano yalianza katika Chuo Kikuu cha Khartoum mnamo June 17, ambapo mamia ya wanafunzi walipinga hatua za kubana matumizi zinazotarajiwa kuchukuliwa na serikali. Waandamanaji walipambana na polisi na wengi wakawekwa kizuizini, hatua ambayo iliamsha hasira na maandamano zaidi katika siku zilizofuata.

Mwandishi wa habari wa shirika la utangazaji la CNN, Ben Wedeman ana maoni yafuatayo:

@bencnn: Ikiwa Misri haikuwa Tsunami ya habari masaa 24 kila siku, basi naona Sudan imenasa macho zaidi. Nchi hii ina historia ndefu ya uasi na mapinduzi.

Arab Revolution anaongeza:

@ArabRevolution: Ninavyotazama video za mapinduzi ya Sudani nakumbuka namna yalivyoanza [mapinduzi] huko Yemen. Ni watu wachache tu walitoka mitaani, lakini wakiwa na ari ya kutekeleza walichokitaka. Haya yatakuwa mapinduzi makubwa katika kipindi cha majuma machache.

Na kutokuwepo kwa habari katika vyombo vikuu vya habari kuonyesha kile kinachotokea nchini Sudani kunawakera wanaharakati. Mwanablogu wa Misri Wael Abbas anauliza [ar]:

هو ليه الجزيرة … مش بتغطي احداث السودان تماما؟
@waelabbas: Kwa nini Aljazeera haionyeshi kabisa habari za matukio yanayotokea Sudani?

Al Jazeera, ambayo ilirusha habari za moja kwa moja katika kipindi cha mapinduzi ya Misri kutokea katika kituo chake kidogo kilichokuwepo karibu na viwanja vya Tahrir mjini Cairo, ilisifika sana kwa kuzifikisha ‘cheche’ za mapinduzi katika sebule zote za nchi za kiarabu.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.