Rwanda: Watumiaji wa Twita Wajadili Mpango wa Rais Kagame wa Kugombea Awamu ya Tatu

Rais wa Rwanda Paul Kagame hana matatizo na mjadala unaoendelea nchini mwake kuhusu ikiwa katiba ya nchi irekebishwe ili kumruhusu kugombea awamu ya tatu ama la. Akiongea kwenye mkutano na waandishi wa habari jijini Kampala, Uganda, ambako alikuwa mgeni rasmi kwenye tukio moja la vijana mjini humo, alidai kwamba raia wa Rwanda wanao uhuru wa kusema hawamhitaji tena, lakini vilevile wana uhuru wa kusema kuwa wanamtaka.

Kiongozi huyu wa Rwanda anasifiwa kwa kumaliza mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 yaliyoangamiza zaidi ya watu 800,000. Katika miaka ya hivi karibuni, mashirika ya haki za binadamu yameonyesha kusikitishwa na rekodi inayoendelea kushuka ya haki za binadamu nchini humo.

Rais wa Rwanda Paul Kagame. Picha imetolewa na David Shankbone chini ya Creative Commons (CC BY 2.0)

Rais wa Rwanda Paul Kagame. Picha imetolewa na David Shankbone chini ya Creative Commons (CC BY 2.0)

Wanaharakati wa Rwanda wanaofanya kampeni kwa ajili ya demokrasia “walisikitishwa sana ” na tangazo hili. Wanaharakati wanaamini kwamba Rais Kagame anatafuta awamu ya tatu kama mbinu ya kujikinga dhidi mashtaka yanayoweza kumkabili siku za usoni. Kwa mfano, wanaonyesha ripoti iliyotolewa hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa (United Nations Mapping report) inayomtuhumu kwa makosa ya uhalifu wa kivita dhidi ya jamii ya kabila la wa-Hutu. Taarifa hiyo hiyo inasisitiza kwamba uhalifu huo unaweza kufikia kiwango cha mauaji ya kimbari kama yatathibitishwa na mahakama ya sheria.
Wachambuzi pia wana wasiwasi kuwa uamuzi huu wa kutafuta awamu nyingine unaweza kuhatarisha usalama katika ukanda wa Maziwa Makuu kwa kuwalazimu wapinzani wa Rwanda kutokuwa na namna nyingine zaidi ya kubeba silaha.
Mjadala wa ukomo wa kipindi cha urais nchini Rwanda unaongozwa na waziri wa mambo ya ndani, Sheikh Musa Fazil Harerimana. Sheikh Fazil pia anafanya kampeni ya kutambuliwa kisheria kwa ndoa za mitala, ambazo kwa sasa haziruhusiwi. Rais Kagame anaonekana kukubaliana na Sheikh Fazil::

Huyu Sheikh ana haki ya kujieleza na inakuwa kama watu wananitarajia niende kwa huyu bwana na kumwambia “Nyamaza. Usizungumzie hili tena” Hapana. Hiyo siyo kazi yangu.

Kwenye Twita, mwandishi wa habari wa Uganda Timothy Kalyegira aliukejeli uamuzi huu kwa maneno ya mzaha:

@TimKalyegira: Maelfu ya wa-Nyarwanda wenye kutiririkwa na machozi hivi karibuni wataanza kuviambia vyombo vya habari vya kimataifa namna gani watajisikia kusalitiwa kama Kagame hatagombea kwa awamu ya tatu.

Mwandishi wa Uingereza Ian Birell vivyo hivyo alionyesha kutokufurahishwa:

@ianbirell: Watu wako huru kusema wananihitaji kuwa rais kwa mara nyingine, asema Kagame. Hawako huru, na kwa kweli ndivyo ilivyo, kusema aondoke…

Lakini maoni ya Ian Birell ndani ya muda mfupi yalivuta ghadhabu ya balozi wa Rwanda nchini Uingereza, Erneste Rwamucyo, aliyemtuhumu kwa kuwa na mtazamo wa tawala za kimagharibi:

@ErnestRwamucyo: Mtazamo huu wa tawala za kimagharibi na “ mtazamo wa kujifanya kujua kila kitu” kuhusu Afrika na viongozi wa Afrika si mzuri. Watu wana haki ya kuheshimiwa.

Maneno ambayo Bw. Birell aliyajibu:

@ianbirell: Hakuna kitu kinachofanana na uelekezaji wa kimagharibi kuhusu kuunga mkono haki za binadamu na kupinga tawala kandamizi na za kimabavu

Kwa kadiri mjadala ulivyoendelea kupamba moto, majibizano makali yakiwahusisha waandishi kadhaa wa habari wa ki-Ganda yalijitokeza. Mambo yalianza pale Bob Muheebwa alipouliza ikiwa kulikuwa na waandishi wengine wa ki-Ganda nje ya Andrew Mwenda na Alan Kasuja waliopenda kumhoji Rais Kagame. Waandishi walishangaa kwa nini Mwenda na Kasuja kamwe hawamkosoi Rais Kagame kwenye makala zao.

Jibu la George Bankole halikuwa la moja kwa moja. Kwa kuonekana wazi kuwazungumzia waandishi hao wawili, Mwenda na Kasuja, alisema:

@Snottyganda: @tijo5 Cos wote wamenunuliwa kwa pesa @mugumya@TimKalyegira@Gilespies@AndrewMwenda@kasujja

Giles Muhame, mhariri mtendaji wa gazeti la Uganda liitwalo Rolling Stone, alionekana kukubali:

@Gilespies: @Snottyganda Niongeze kipi tena hapo? @tijo5@mugumya@TimKalyegira@AndrewMwenda@kasujja

Ndivyo alivyofanya pia mwandishi Timothy Kalyegira:

@TimKalyegira: @Snottyganda@tijo5@mugumya@AndrewMwenda@kasujja Wengine wamenunuliwa kwa sifa tu za kuwa na mahusiano ya kirafiki na wakuu wa nchi.

Andrew Mwenda aliendelea kuwa kimya kwa suala hili, lakini Allan Kasujja baadae akakanusha madai hayo:

@kasujja: @TimKalyegira @tijo5 @mugumya @AndrewMwenda Ninashangazwa na namna hoja zenu zilivyokuwa rahisi. Hivi haiwezekani nikasukumwa na haki

Kwa mara nyingine, Timothy Kalyegira akajibu:

@TimKalyegira: @kasujja Inaweza kuwa ni haki. Inafikirisha kwa wengine wetu, mbio hizi za waandishi wa ki-Ganda kuimba sifa za Kagame.

Rwanda hivi sasa inao ukomo wa vipindi viwili vya kikatiba kwa urais. Kila kipindi kina jumla ya miaka saba, ambacho ni kipindi kirefu kuliko vyote barani Afrika. Rais Kageme aliingia madarakani rasmi mwaka 2000 ingawa wengi wanaamini alikuwa madarakani kwa namna fulani tangu wakati wa mauaji ya kimbari yaliyoikumba nchi hiyo mwaka 1994.

1 maoni

jiunge na Mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.