Ghana: Nani atanufaika na mafuta?

Wakati Kampuni ya mafuta ya Uingereza Tullow Oil ilipotangaza uvumbuzi wake wa kiasi cha mapipa milioni 600 ya mafuta nchini Ghana mwaka 2007, ulimwengu wa wanablogu uliitikia kwa maoni yanayotofautina juu ya matumaini na hali ya kuchelea. Baada ya miaka miwili tangu kuvumbuliwa, nchi hiyo imeanza kujiandaa kwa uzalishaji wa mafuta, lakini majadiliano ya hivi karibuni yanazunguka kwenye maswali: “Nani atanufaika na na nini kinaweza kuwa matokeo ya maamuzi yanayofanywa na watawala wa Ghana leo?”

Charles Crawford, kwenye Blogoir, alitoa maoni kwenye kipande kilichoandikwa na Craig Murray akiainisha sababu na athari za kupatikana kwa mafuta nchini Ghana. Aliandika haya kwenye makala hiyo ya Murray:

Katika wakati mmoja, mapato lazima yaelekezwe kwenye miundo mbinu ya vijijini, kuongeza bei za mazao ya mashambani na kuendeleza viwanda vya kusindika mazao, katika kipimo ambacho hakikuwahi kujaribiwa kabla. Ghana tayari ina tatizo kubwa la namna ya kuwafanya vijana waendelee kulima. Fikiria namna hali hii itakavyokuwa mbaya zaidi mafuta yatakapoanza kumiminika.

Kwa nini vijana wabaki mashambani sasa ambapo nchi inaelekea kuwa tajiri? Ghana, kama mpinzani wa Naijeria, imekuwa sehemu mpya yenye teknolojia kubwa katika aina ya Kisingapore badala ya kuwa nchi ya Kiafrika yenye kutegemea mauzo ya kilimo zaidi?

Je, si suala la kujipatia hazina kubwa namna hii inayoipa nchi nafasi ya kuangalia chaguzi tofauti, na siyo tu njia za kusimika masuluhisho yanayotoka juu kuja chini katika misingi ya mawazo ya kizamani?

Maoni yaliwekwa kujibu kauli hiyo ya mwanablogu mwenye jina la Craig Murray yalisomeka:

Kwa sababu William Cobbett alikuwa sahihi!

Maoni ya Crawford kuhusu vijana wanaoendelea kujishughulisha na shughuliza mashambani, pamoja na njia inayoonekana ya nchi kuelekea kwenye utajiri, yamekuwa kwenye vichwa vya Waghana. Mwanablogu Ghana Pundit aliweka kipande kilichotoka kwenye Shirika la Habari la Ghana (GNA) kilichozungumzia suala hilo hilo:

Dr. Edward Omane Buamah, Naibu waziri wa Mazingira, Sayansi na Teknolojia, ameona kwamba upatikananji wa mafuta na gesi kwenye Mkoa wa Magharibi, kumefanya tatizo la ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana kwenye eneo hilo kuwa suala kubwa.

Akizungumza katika kongamano maalumu kuhusu Tathmini ya Athari za Mazingira kwa ajili ya awamu ya kwanza ya kuendeleza Maeneo yenye mafuta ya Jubilee, lililoandaliwa na Mwakilishi wa mkoa huo wa Baraza la Machifu katika Sekondi, alisema eneo hilo halijafaidika na raslimali kama bahari, dhahabu na vito vingine, magogo na madini mengine.

Dr. Buamah alisema kwa hiyo ilikuwa ni jambo linalotegemewa kwa vijana kutegemea unafuu wa nafasi za ajira baada ya kupatikana mafuta ya Ghana.

Alisema ajira za moja kwa moja kutoka kwenye visima vya kuchimba mafuta zinahitaji kiwango cha juu cha ujuzi, uwezo na sifa za kitaaluma, hivyo kuhitaji vijana kujiendeleza zaidi ili kuweza kufaidika kikamilifu na nafasi nyingi za kazi, ambazo zitatokana na machimbo hayo.

Mwanablogu Ghana Pundit aliweka makala nyingine ambayo iligusia eneo jingine la kutilia maanani:

Kupatikana kwa mafuta Ghana kama hakutashughulikiwa kwa umakini kunaweza kusababisha ghasia zinazofanana na kile kinachotokea Naijeria kwenye eneo la Delta ya Naija lenye vurugu kubwa.

Mwanasheria anayeheshimika na mhadhiri kwenye Chuo Kikuu cha Ghana, Kitivo cha Sheria, Dr. Raymond Atuguba ameonyesha kwa umakini jinsi wanamgambo wa eneno la Delta ya Naija, wanaojulikana kwa ukorofi wa kulipua mabomba ya mafuta, kuteka watu nyara na kudai dhamana kubwa na kusababisha vurugu kwenye eneo lenye utajiri wa mafuta nchini Naijeria wameanza kuingia Ghana kwa makundi.

Dr. Atuguba katika mahojiano yake kwenye kipindi cha Citi Breakfast Jumatano alisema kiini cha maslahi ya wanajeshi hao nchini Ghana ni kuwafundisha kuwa walinzi wa maslahi yao wananchi wa Mkoa wa Magharibi wa Ghana, ambako kwenye ufukwe wake, nchi itakuwa ikichimba mafuta.

Ingizo jipya la makala kwenye blogu rasmi ya kampeni ya Rais Atta Mills lilisema:

Rais John Evans Atta Mills siku ya Alhamisi aliikumbusha kampuni ya Kosmos Energy, moja ya makampuni yanayohusika na upatikananji wa mafuta ya taifa kwenye maeneo ya Jubilee ya Cape Three Points, kuwa werevu wa kijamii, kisheria na wajibu kibiashara ili kwamba watu wa mahali hapo waweze kuwa sehemu ya mchakato na kupata faida.

Aliisihi kampuni hiyo kuwatumia wataalamu wa Ghana wanaopatikana na vile vile kuwakinga watu na changamoto zinazoweza kutokea kutokana na uchimbaji wa mafuta.

Maoni, katika kujibu makala hiyo, ya Ofori Amooako Elijah yanasomeka:

Uchimbaji wa mafuta ni lazima uwanufaishe zaidi watu wa Ghana hususan, ni lazima iwe hatua katika kutengeneza ajira.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.