Afrika Kusini: Kikaragosi Kiliochoathirika na VVU Kwenye Kipindi cha Sesame Chaelimisha Kuhusu Ukimwi


Wakati kipindi cha watoto cha Mtaa wa Sesame (Sesame Street) kikisherehekea maadhimisho ya miaka 40 mwezi huu, kwa kizindua msimu wake mpya leo, kikaragosi kizuri kinachovutia cha Muppet katika toleo la Afrika Kusini kinaendelea kusaidia kupambana na kuelimisha kuhusu VVU/UKIMWI.

Wakati kipindi cha Sesame Street kinatazamwa katika zaidi ya nchi 140, kila toleo huzungumzia masuala yanayotokea kwenye jamii husika na kwa kumtumia vikaragosi tofauti. Kami mwenye rangi ya Njano-dhahabu alionekana kwa mara ya kwanza kwenye kipindi mwenza cha Sisame Street cha Afrika Kusini kinachoitwa Takalani Sesame, mwaka 2002 kujibu matatizo ya nchi yanayohusiana na UKIMWI. Kama kikaragosi cha kwanza duniani chenye VVU, kinasaidia kuwaelimisha watoto kuhusu ugonjwa na kushughulikia masuala yanayohusiana na kuwa mwathirika wa UKIMWI. Jina la Kami linatoka kwenye neno la kiSetswana “Kamogelo”, lenye maana ya “kukubalika.” Sunshinestar110, anayeblogu kwenye U dont Like My Opinion…That’s Fine! anazungumzia zaidi kuhusu Kami:

“Kami ni mwathirika wa VVU mwenye afya, yatima wa miaka mitano mwenye bashasha ambaye ana aibu kidogo lakini huchangamka akijongelewa kwa njia ya kirafiki, pia anajua mengi kuhusu Virusi vya UKIMWI, alimpoteza mama yake kwa ugonjwa huo. Kami alipozinduliwa, akiwa na nywele zake za kahawia na pia alivaa fulana, na kutembea kwenye mtaa wa Susame na kujiuliza huku akihofu kama wenyeji watataka kucheza nae. Hakuwa na haja ya kuogopa kwa sababu vikaragosi vingine vilimpokea kwa bashasha”

Kami aliletwa kuwasaidia watoto wengi wa Afrika Kusini wanaotaabika na janga la VVU/UKIMWI. Inaaminika kuwa Afrika Kusini ina idadi kubwa zaidi ya watu walio na VVU duniani – inakadiriwa kuwa watu milioni 5.7 Kwa makadirio, kati ya walioathirikia, 280,000 ni watoto wa umri wa miaka chini ya 14 na kuna yatima milioni 1.4 nchini kutokana na UKIMWI. Zaidi ya madhara ya kimwili ya kuwa na VVU, vilevile kuna unyanyapaa na miiko inayotokana na kuwa na ugonjwa, ambayo husababisha ugumu kwa watu kupata matibabu stahiki na msaada. Takalani Sesame, ambayo inajumuisha lugha zote rasmi 11 za Afrika Kusini, inajaribu kuwasaidia watoto kuyatazama masuala haya kwa ujasiri kupitia Kami.

Hata hivyo, kulikuwa na mkanganyiko wakati Kami alipoanza kuonyeshwa, hasa hasa nchini Marekani, ambapo wengi walikasirishwa na kuwa kipindi cha watoto kinanamchezesha mhusika mwenye VVU. Haven on Earth anafafanua mjadala huo:

“Ingawa ilitaarifiwa kuwa ujio wa Kami kwenye kipindi cha Sesame Street nchini Afrika Kusini ulikuwa unakaribishwa.(Nina wakati mgumu kukubaliana na ukweli huu kwa sababu kiwango kikubwa cha kukataa bado kipo), kulikuwa na mkanganyiko ulio wazi hapa Marekani. Ninakumbuka kusoma kuhusu suala hili (hii ni sababu ya mimi kufurahia kukutana na kipindi kikirushwa kutokea Afrika Kusini – nisingelifikiria kukitafuta). Iliondokea kuwa kundi la wabunge wa Congress wa chama cha Republican walituma barua kwa Rais wa Shirika la Utangazaji la Umma (PBS) linalorusha kipindi cha Sesame Street. Barua ilidai kwamba mipango ya kuleta mhusika kama huyo ambaye ni mwathirika wa UKIMWI nchini Marekani haikuwa sahihi, kwa kuzingatia umri wa watazamaji. Walipendekeza kwamba hatua hiyo ingeathiri ufadhili wa umma kwa Shirika hilo (PBS).”

Kami hajawahi kuonekana kwenye kipindi cha Sesame Stree cha Marekani, ingawa amedhihirisha kuwa mhusika aliyefanikiwa sana kwenye kipindi cha Takalani Sesame na zaidi. Mwaka 2003, UNICEF ilimteua kuwa “Shujaa wa Watoto” duniani. Katika video hii, anaungana na Rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton kutoa ujumbe kuhusu VVU/UKIMWI. Jamie, anayeblogu kwenye No day but Today…, anajadili mafanikio mengine ya Kami:

“Kwa sababu watoto wengi wa Afrika Kusini wanamfahamu mtu fulani mwenye UKIMWI, mhusika huyo amekuwa shujaa wa taifa, anayependwa na watu wa nchi hiyo. Kami ameonekana kwenye Umoja wa Mataifa na Benki ya Dunia na alihojiwa na Katie Couric. Ameteuliwa kuwa balozi wa UNICEF wa watoto na ameonekana kwenye vipande vya onyesho la Takalami pembeni mwa Desmond Tutu na Nelson Mandela.”

Pamoja na mafanikio ya Kami, wanablogu wengine bado wanaamini kuwa si mhusika sahihi kwa toleo la Kimarekani la Sesame Street. Emily Meyer, anayeblogu kwa ajili ya darasa lake la heshima, anasema:

“Ingawa ni muhimu kwa Wamerekani kufahamu kuhusu VVU/UKIMWI na hatari ya ugonjwa wenyewe, nadhani kuwafundisha watoto katika umri wa miaka miwili na mitatu ni kwenda mbali sana. Watoto wadogo kiasi hiki hawataweza kuelewa kuhusu VVU na hawataelewa madhara yake. Kama Kami alitakiwa aletwe Marekani kama njia kueneza elimu na kudhibiti UKIMWI, sidhani kama matokeo yaliyokusudiwa yangetokea…Watoto nchini Marekani hawalazimishwi kuhusika na masuala ya UKIMWI katika umri huo mdogo. Nadhani wakati sahihi kwa watoto nchini Marekani kujifunza kuhusu hatari ya virusi vya UKIMWI ni wanapokuwa wakubwa, kadri ya miaka kumi ama kumi na moja au wakati mwanafunzi anapoanza kujihusisha na vitendo vya mapenzi kimwili”

Bado, wanablogu wengi, kama huyu hapa anayeandika kwenye Muppets and History, anamwona Kami kama mfano mwingine wa namna Sesame Street inavyosukuma mipaka. Wengine wanaonyesha upendo wao kwa kikaragosi huyo na ujumbe anaowaletea watoto. Na wengine wanadhani anatakiwa atumike kwenye matoleo mengine ya Sesame Street. Katika blogu yake binafsi, Steisha Pintado anasema:

“Anawaonyesha watoto kwamba ni sawa kumkumbatia mtu mwenye virusi vya UKIMWI, na anaeleza nini cha kufanya anapokuwa na kidonda kwenye kidole chake au kama umejikata mwenyewe. Anaifundisha hadhira ya watoto wadogo kuhusu kukabiliana na kuumwa na kupotelewa….Ingawa ngono huwa haitajwi kamwe katika kuzungumzia hali ya Kami, watu wengine wamesema kuwa kuwepo kwa mhusika mwenye virusi vya UKIMWI lisingekuwa jambo sahihi kwa hadhira ya watazamaji wadogo. Mbunge mmoja hata alidai kuwa Warsha ya Sesame ingepoteza msaada wa kifedha kutoka serikalini kama ingerusha kipindi chenye mhusika huyo kwenye nchi yetu. Inashangaza kusikia maneno haya. Wazazi wanatumia muda mfupi (na unaopungua kila siku) na watoto wao, na wanaruhusu runinga kuwaelimisha zaidi na zaidi. Ni wazi wazazi wengi hawawafundishi watoto wao namna ya kuyakabili masuala nyeti ya uelewa na kukubalika. Wazazi tayari wamewaruhusu Warsha ya Sesame kuingiza suala la kukubalika kwa wale wenye ulemavu na kuugua, na pia kwa wale wenye rangi na dini tofauti. Je, hii ina tofauti gani?

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.