Jinsi Mauaji ya Mwanamuziki Hachalu Hundessa Yalivyochochea Uvunjifu wa Amani Huko Ethiopia: Sehemu Ya I

Hachalu Hundessa akifanyiwa mahojiano na OMN kupitia Firaabeek Entertainment / CC BY 3.0.

Dondoo ya Mhariri: Huu ni uchambuzi wenye sehemu mbili juu ya Hachalu Hundessa, mwanamuziki maarufu wa Oromo ambaye mauaji yake yaliamsha vurugu za itikadi za kidini na kikabila kwa sababu ya taarifa zisizo sahihi zilizotolewa katika mitandao ya kijamii. Soma Sehemu ya pili hapa  

Mwanamuziki mkubwa wa Kiethopia Hachalu Hundessa alipata umaarufu kwa kutumia ubunifu na kipaji chake kuutambulisha umma kuhusu watu wa Oromo. Aliuawa katika viunga vya mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, tarehe 29 Juni mwaka huu.

Usiku ule mnamo saa tatu na nusu, wakati Hachalu akishuka kwenye gari lake, mwanaume aliyejulikana kwa jina la Tilahun Yami alitembea kuelekea gari yake na kumpiga risasi  kifuani mwake. Alikimbizwa katika hospitali ya karibu ambapo ilithibitishwa rasmi kwamba amefariki. Iligundulika baadaye kwamba risasi iliharibu vibaya sana viungo vyake vya ndani.

Mkuu wa polisi wa Addis Ababa  aliripoti kwamba watuhumiwa wawili wamekamatwa. Baada ya siku chache mamlaka za serikali ziliwahukumu wauaji hao pamoja na washirika wao wawili.

Katika kuuawa kwake, nchi imeingia katika wakati mgumu wa kutuliza ghasia zilizofuata. Ukweli ni kwamba mauaji ya Hachalu hayajawekwa wazi vizuri na pia matokeo yake, uvumi ulianza kuenea baada ya wanasiasa na wanaharakati  kuweka msisitizo mkubwa kuhusu mgogoro uliopo baina ya viongozi wakuu wa Oromo na Amahara ambayo ni makabila makubwa kabisa nchini Ethiopia.

Siku ya maziko yake, waombolezaji walifurika katika mitaa ya Addis Ababa na miji mingine inayozunguka jimbo la Oromo. Asubuhi iliyofuata Kituo cha runinga ya setilaiti cha Oromia Media Network (OMN), ambapo ndipo Hachalu alifanya mahojiano yake ya mwisho walirusha matangazo mubashara kupitia runinga na pia mitandao na kuonesha wakati jeneza lake likisafirishwa kutoka Addis Ababa kwenda nyumbani kwao huko mjini Ambo.

Matangazo hayo yaliyokwenda polepole sana yaligeuka kuwa uwanja wa mapambano baina ya mamlaka za serikali na viongozi wa upinzani, kukiwa na mabishano ya wapi hasa akazikwe Hachalu  na OMN ilibidi wakatize matangazo yake; inasemekana walilazimishwa kurejea Addis Ababa. Watu kumi waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa huko Addis Ababa.

Mgongano huo ulipelekea kukamatwa kwa baadhi ya viongozi wa upinzani akiwepo Jawar Mohammed ambaye ni kiongozi wa  OMN  na pia kiongozi wa upinzani Bekele Gerba ambapo walishtakiwa kwa kuchochea vurugu.

Utata uliibuka zaidi baada ya mamlaka za serikali kuuchukua tena mwili wa Hachalu na kuupeleka mjini kwao Ambo kwa njia ya helkopta, ambapo pia pande mbili ziliendelea kugombana na kuinyima familia ya marehemu fursa ya kumpa ndugu yao maziko stahiki.

Baada ya hapo vurugu na mapigano yalifuata. Mapigano hayo yalichukua siku tatu yaliyararua baadhi ya maeneo ya miji ya Oromo na Addis Ababa na uharibifu halisi ni: vifo vya watu 239  na mamia wamejeruhiwa, zaidi ya watu 7,000 wamekamatwa kwa kusababisha vurugu na uharibifu wa mali  zenye thamani ya mamilioni ya birr, fedha ya Kiethopia.

Hapo Juni 30, serikali ilijaribu kuzima mtandao ili kuzuia kuenea kwa uhamasishaji wa kufanya vurugu unaofanyika katika mitandao ya kijamii na kudumu kwa wiki tatu.

Watu kadhaa walipigwa risasi na mamlaka za usalama lakini baadhi ya vyanzo vya habari ikiwamo Sauti ya Amerika na Addis Standard viliripoti kuwa vikundi vya watu wenye hasira kutoka kabila la Oromo walishambulia watu wa makundi mbalimbali ikiwepo miji na mitaa inayokaliwa na watu wa imani tofauti tofauti, iliyo Kusini Mashariki mwa mji wa Oromo, wakilenga hasa familia za watu wasio Waoromo na wasio Waislam katika ukanda huo.

Vurugu zaidi zilikuwa katika ukanda wenye mchanganyiko wa watu wa Amahara-Oromo na dini inaweza ikawa imecheza nafasi kubwa kwa sababu ya uelewa uliopo kwamba: jamii ya Waoromo wa Kusini Mashariki inatambulishwa kwa mchangayiko wa dini ya Kiislamu na watumiaji wa lugha ya Afan-Oromo. Mkulima mmoja wa maeneo hayo alisema kwamba “tulifikiri Hachalu ni Muoromo” baada ya kuangalia matangazo yaliyorushwa moja kwa moja yakionesha shughuli za maziko ya Hachalu yaliyofuata desturi za Kanisa la Kiothodoksi la Tewahedo Ethiopia.

Kulingana na ripoti, wahanga wengi wa vurugu hizo walikuwa ni Wakristo wa ki-Amhara, Wakristo wa ki-Oromo na watu wa Gurage.  Shuhuda mmoja alisema kuwa makundi hayo yaliharibu na kuchoma moto mali na kufanya mauaji  kwa kuwakata vichwa na miguu wahanga.

Utabiri wa Mahojiano

Wakati taarifa kuhusu mauaji ya Hachalu ziliposikika tu, chanzo cha habari za Waoromo wa diaspora zilihusisha kifo chake na  mahojiano ya mwisho aliyoyafanya Hachalu na kituo cha runinga cha OMN yakiongozwa na Guyo Wariyo, na yalirushwa wiki moja kabla Hachalu hajauawa.

Wakati wa mahojiano Gayo alirudia rudia kumuuliza Hachalu maswali ya mtego kuhusu yeye kukiunga mkono chama tawala na pia mara kwa mara alimkatiza alipokuwa akijibu.

Hachalu alikataa kuunga chama tawala mkono lakini pia alikosoa  migogoro na utengano katika vyama vya siasa vya Oromo, akionesha uhuru wa mawazo kama mwanamuziki – hali ambayo ilimfanya kuwa mlengwa wa mashambulizi ya watu mtandaoni mpaka siku aliyouawa.

Hata hivyo, Guyo alimuuliza Hachalu kuhusu unyanyasaji wa kihistoria uliofanywa kwa watu wa Oromo na mfalme Menelik II aliyeijenga Ethiopia ya sasa.

Hachalu aliwashangaza wasikilizaji wengi aliposema kuwa farasi aliyepandwa na Menelik katika sanamu iliyopo huko Addis Ababa alikuwa mali ya mkulima wa ki-Oromo aliyeitwa Sida Debelle, na Menelik alimuiba farasi huyo.

Majibu hayo yalivutia maoni ya kumsifia  na pia ya kumkosoa kutoka kwa watu mbalimbali huko Facebook na Twitter.

Wakati Hachalu alikiuawa wiki moja baadaye watu wengi wa jamii ya Oromo wanaokaa nje ya nchi walihisi kwamba kitendo cha Hachalu kuikosoa sanamu ya Menelik II kiliwakasirisha wanaoiunga mkono Ethiopia ya kifalme na kusababisha kuuawa kwake.

Katika mitandao ya kijamii wananchi waling'ang'ana na kile Hachalu alichokisema dhidi ya Menelik, na hili lilisababisha kuenea kwa uvumi wenye taarifa nyingi za uongo. Sehemu nyingine ya mahojiano imebeba taarifa za mambo yanayohusu utengano na migogoro ndani ya jamii ya Waoromo.

Katika mahojiano yote Guyo alimchimba sana Hachalu kuhusu mabadiliko ya kisiasa yanayoendelea nchini na kuhusu vuguvugu la kuipinga serikali kwa kuuliza swali kuhusu Waziri Mkuu Abiy Ahmed, ambaye ni Muoromo na kwamba kama serikali imeweza kutimiza matakwa ya watu wa Oromo tangu aingie madarakani mwaka 2018.

Hachalu alirudia kusema kuwa hajihusishi na siasa za ovyo za Oromo lakini aliwakosoa wote wanaohukumu uzalendo wa Abiy.

Aliilinda nafasi yake dhidi ya viongozi wakuu wa upinzani walioungana na Tigray People's Liberation Front (TPLF), ambacho kilishawahi kuwa na ukaribu na  chama kikuu chenye historia kubwa cha Ethiopian People's Revolutionary Front (the EPRDF). TPLF iligeuka kuwa chama cha upinzani baada ya Abiy kuibomoa EPRDF.

Hachalu pia alizungumza kuhusu vurugu za kisiasa zinazoendelea katika mkoa wa Oromo akilaumu pande zote yaani mamlaka za serikali na wanamgambo wa kikundi cha wanamgambo wa mrengo wa kulia Oromo Liberation Front (OLF) ambapo pia (hufahamika kama OLF-Shane).

Kufuatia mauaji ya Hachalu, serikali iliweza kuchukua mkanda wa mahojiano yenye urefu wa dakika 71 na  kuyarusha kwa umma.  Mkanda huo unajumuisha ujumbe wa vitisho vya kuuawa alivyotumiwa Hachalu kutoka pande za Magharibi mwa Oromo, ambapo ndipo vikosi vya wanamgambo wa OLF-Shane wanafanyia shughuli zao.  Hachalu alisema aliamini kuwa asingeshambuliwa mitandaoni kama angewasifia OLF-Shane.

Alizungumzia moja kwa moja mgogoro baina yake na Getachew Assefa, Afisa Usalama Mkuu wa Ethiopia katika kipindi TPLF ikiwa madarakani.

Guyo, aliyeyatangaza mahojiano hayo katika ukurasa wake wa Facebook kwa kuyaita “lazima uyaone” siku chache kabla ya kurushwa kwake hewani, amekamatwa na polisi tangu wakati huo na serikali inafanya upelelezi wa mkanda wa dakika 71 za mahojiano hayo ili kupata vielelezo vitakavyosaidia kupata ufumbuzi wa chanzo cha mauaji ya Hachalu.

Soma zaidi kuhusu madhara yaliyotokana na mauaji ya Hachalu Hundessa katika sehemu ya II. 

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.