Mtalii wa Kifaransa ameuwawa na watu wapatao 20 wamejeruhiwa wakati bomu lilipolipuka nje ya msikiti wa Al Hussein uliopo katika eneo la utalii la Khan Al Khalili mjini Kairo mapema leo.
Na wakati dunia ilipokuwa inaanza kufahamu ni kipi kilichokuwa kinatokea, wanablogu wa Misri waliingia kazini haraka, wakipashana habari za yanayotukia, taarifa, uchambuzi na hofu zao.
Yote yalianza wakati Zenobia alipotundika ujumbe katika ukurasa wa Twita akiripoti kuwa “Kumetokea mlipuko wa aina fulani kwenye mgahawa uliopo Al Azhar.” Dakika chache baadaye Arabawy alifuatia na ujumbe mwingine uliothibitisha: “Mlipuko katika mtaa wa el-mashhad el-Husseini mjini Kairo.”
Moftasa ndiye alikuwa wa kwanza kuuhisi uhusiano wa milipuko na sheria mpya ya kuzuia-ugaidi, ambayo itajadiliwa katika siku chache zijazo kwenye bunge la Misri. Rasimu ya sheria hiyo imekumbana na vipingamizi vikubwa.
Hakuna lililothibitishwa mpaka sasa, na uvumi unaenea; hata hivyo, Zeinobia alijaribu kukusanya habari kama zinavyotokea kutoka vyanzo tofauti vya magazeti na idhaa za televisheni katika muhtasari.
Mwanablogu Arabist, ambaye alikuwa Karibu na eneo na kuusikia mlipuko huo yeye mwenyewe, aliandika:
Nimesikia taarifa za mabomu yanayolipuka katika mji mkongwe wa Kairo Karibu na Khan al-Khalili, sehemu maarufu kwa watalii. Nitawapasha kadri habari zitakapopatikana.
Habari mpya: Al Jazeera inaripoti
vifo 11, Wamisri watatu, Wajerumani watatu, Mfaransa mmoja,16 wamejeruhiwa, Mfaransa mmoja amefariki, haya na mengineyo bado hayajathibitishwa.Habari mpya 2: Tayari wanaharakati wanasema kuwa tukio hili limetukia Karibu sana na mwezi ujao ambapo Sheria ya Dharura itajadiliwa Bungeni…
Habari mpya 3: Wanne wamefariki (Wajerumani na Wafaransa) 12 wamejeruhiwa, wa mataifa mbalimbali.
Halafu moftasa alibandika kiungo cha picha kutoka kwenye eneo la mlipuko kwenye Twita.
Wakati Msfour, mfanyakazi wa Kimarekani anayeishi Kairo, alikuwa wa kwanza kuwataka wanablogu wanaotumia Twita kutumia kielelezo cha #cairobomb, Arabawy ndiye alikuwa wa kwanza kuwataka wanablogu watumie kielelezo jumuishi cha delicious: El-HusseinExplosion ili kukusanya viunganishi vyote chini ya anwani pepe moja.
Wanablogu Yassary Masry [Ar], Carl, Msfour, Maree, Rob, SandMonkey pamoja na Grey wool Knickers walikuwa ni miongoni mwa wanablogu wa kwanza kuandika kuhusu tukio hilo, ama kuwafariji marafiki na familia au kujadili uhusiano wa milipuko ya mabomu na sheria ya kuzuia ugaidi. Grey wool Knickers aliandika ujumbe mfupi unaohusianisha matukio ya mwisho yaliyotokea Misri, akijaribu kuyaunganisha na milipuko ya hivi karibuni:
Kama watu kadhaa wanavyoona, matukio haya yametokea katika wakati wa kushuku, tukizingatia kwamba Sheria ya Dharura (iliyokuwepo tangu mwaka 1967 wakati wa vita vya Waarabu-na-Waisraeli, vilivyositishwea kwa muda wakati wa utawala wa Rais Sadat) ilitaka kuanzishwa tena. Serikali ya Rais Mubarak imekuwa ikiahidi kwa miaka mingi kuanzisha sheria ya kuzuia ugaidi ambayo ingechukua nafasi ya sheria za kijeshi, ambayo ingewapa raia angalau kinga kidogo kwenye katiba ya Misri. Utawala wa sasa unao uwezo wa kurejesha Sheria ya Dharura na kutenda inavyotaka, kama wasomaji watakavyogundua katika kutekwa kwa Philip Rizk na Diaa Gad, kati yaw engine wengi. Huku kukiwa na matarajio ya mabadiliko katika serikali za Marekani na Israeli – pamoja na makundi ya upinzani yenye sauti na yaliyo mitandao ya ndani na ile inayovuka mipaka na kuingia Gaza – inaonekana kuwa utawala unaozeeka wa Mubarak unaanza kuingiwa na kihoro na kujikuta una machaguo machache ya kuendeleza mshiko wake madarakani isipokuwa kwa kutumia mikakati ya kuongeza hali ya vuguvugu. Nafikiri kuachiwa kwa mfungwa wa kisiasa Ayman Nour hivi karibuni kunaweza kuwa ni ushahidi wa mchechetu unaozikumba ngazi za juu za utawala huu wa kiimla. Ili kupata habari kama zinavyotukia, angalia ukurasa huu wa delicious.
Mpaka wakati makala hii ilipokuwa ikiandikwa imethibitishwa kwamba msichana wa Kifaransa mwenye umri wa miaka 21 ameuwawa, na watu wengine wapatao 20 wa mataifa mbalimbali wamejeruhiwa. Hata hivyo, bado ni mapema mno kurukia hitimisho la ni nani aliyehusika na milipuko.
Picha zinaweza kupatikana katika blogu ya AbdelFatah na wasomaji wanaweza kuwafuatilia wanablogu wa Misri kwenye twita hapa.
2 maoni
president acheiye ma daraka
Interesting and made me think