Guadeloupe: Hali Tete Yazua Ghasia

Baada ya wiki za maandamano ya amani katika Idara za Ng'ambo za Ufaransa za Guadeloupe na Martinique, mambo yaligeuka na kuwa ghasia siku ya jumatatu, polisi na waandamanaji walipambana katika jiji kubwa la Guadeloupe, Pointe-a-Pitre. Wafanyakazi wanapinga ukosefu wa ajira unaoongezeka pamoja na kupanda kwa bei za bidhaa muhimu, ambazo nyingi zake huagizwa kutoka Ufaransa.

Katika tovuti ya uandishi wa kiraia, Agoravox, Illiouchine, metropolitanin [raia wa Ufaransa aliyeko Ufaransa bara], anaelezea hali ilivyokuwa katika Guadeloupe mwishoni mwa juma na utulivu uliofuatia baada ya ghasia za usiku wa Jumatatu.

Hali ya hewa ilikuwa nzuri asubuhi hii, jua, hapakuwa na upepo, kadhalika hapakuwa na mawingu angani. Kilele cha Soufrière [volkeno iliyopo kwenye mbuga za taifa za Guadeloupe], kilikuwa kinaonekana wazi kabisa. Uliweza kuuona moshi unavyopaa moja kwa moja kuelekea angani kutokea kwenye matobo yaliyoko juu ya volkeno hiyo.

Jana usiku hali ilibadilika. Maeneo yanayoizunguka PAP [Pointe-à-Pitre, jiji kubwa katika Guadeloupe] yalikuwa ndiyo kiini cha ghasia: paliwaka moto, na maduka yaliporwa. Maduka ya walaji hayakuguswa, ni maduka ya vifaa vya michezo na spea za magari ndiyo yalidhurika. Kila sehemu, palikuwa na vizingiti asubuhi hii. Kiranja aliendelea kuwa mtulivu na akasema kuwa ataendelea kusafisha barabara. Hivi sasa, Saint Claude imerudia hali ya kawaida, maduka yamefunguliwa, na watu wanaendelea na shughuli zao.

La Guadeloupe en colère anaelezea matukio ya Jumatatu:

Jana asubuhi, watu waliogoma walisimika vizuizi kadhaa barabarani katika sehemu muhimu.
… vikosi kadhaa vya polisi, vilivyotumwa kisiwani humo mwanzoni mwa mgogoro, viliendelea na kazi ya kuviondoa vizuizi hivyo. Mambo yasiyoepukika yalitokea. Huku wakikabiliana na pingamizi kutoka kwa waandamanaji, vikosi vya usalama havikusita kutumia nguvu. Waandamanaji kadhaa walichukuliwa kwa ajili ya kuhojiwa, kiasi cha 50, ambao wote wataachiwa leo baada ya kushikiliwa na polisi kwa muda.

Nimeudhika na jinsi hali ilivyoharibika, ambapo ghasia zinatawala mazungumzo yameshindwa… Ni makosa ya nani? Dola? Umma? Waajiri? Kila mmoja ana makosa kwa sababu kila mmoja anafahamu matokeo!

Ilikuwa vigumu kuamka. Nilistuka niliposikia kwamba duka la magazeti, kisiwa hadimu cha utamaduni, lilichomwa moto. Nasikia hofu inaanza kunichukua. Niliamua kwenda kazini; kwa hakika [mimi] nina dhamira kubwa au hamasa. Wanyapara waliwasiliana nasi na kutuambia turejee nyumbani, wakihofu kwamba hali ilikuwa ni tete mno.

Nikaondoka… huku takataka zinazoungua zikiipamba mitaa…
Kwa mara ya kwanza ninajiuliza tunaenda wapi…

Katika safu ya maoni, f parfait anaandika:

Bila ya kuyahalalisha yote yaliyotukia, ninapata matumaini katika ukweli kwamba jamii ya Waguadeloupe haijakuwepo hata kwa miaka 400, na watu wa Guadeloupe (ni lini utumwa ulikomeshwa?). Sisi ni jamii ambayo bado inajiunda. Ni muda gani Ufaransa ilitumia kufikia hapo ilipo leo?…

Caro akitoa maoni katika makala moja ya Rue89, anafafanua ni nini chimbuko la mgogoro huu:

Kosa kubwa, kwa maoni yangu, lilikuwa ni kujaribu kusuluhisha [vuguvugu] katika Guiana ya Kifaransa mnamo mwezi Disemba (kwa sababu malalamiko ya kwanza yalitokea katika Guiana ya Kifaransa), bila ya kufanya lolote kwa ajili ya Guadeloupe au Martinique, ambako kila mmoja alikuwa anafahamu kuwa walikuwa wanajitayarisha kwa ajili ya mgomo.

Serikali ikaachia hali iendelee kuharibika, wakati wanazifahamu kero za wananchi, ukosefu wa ajira unaoongezeka, na kwamba bidhaa muhimu zinazoagizwa kutoka taifa mama, zilikuwa zinazidi kuwa ghali.

Idara ya Ng'ambo inapokea fedha nyingi, siyo tu kutoka kwa taifa mama, bali pia kutoka nchi nyingine za Ulaya (kwani ni sehemu ya Ulaya…), Lakini fedha hizi haziwasaidii watu, ambao wanazidi kuwa masikini…

Kama hawataki kuziona Idara zote za Ng'ambo zikilipuka (Guiana ya Kifaransa itakuwa tayari kufanya mgomo baada ya tamasha la kanivali, kadhalika mambo yanatukia pia huko Reunion), ni kwa maslahi ya serikali kutafuta suluhisho haraka na kufungua mifuko yao ya fedha katika njia ambayo itawanufaisha watu, na sio waajiri. Lakini hivyo ni kinyume na falsafa za mamwinyi.

Haya yataishia vipi? Tunaweza kuhofu. Tunahitaji kuungwa mkono na umma wote wa Ufaransa bara, kuonyesha mshikamano. Kinachotokea huko kinatudhuru na sisi pia.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.