Wakati vita vikiendelea huko Gaza, taarifa zilizotolewa mwanzoni mwa mwezi kuhusu usafirishwaji wa shehena kubwa ya silaha kutoka Marekani kuelekea Israeli kupitia bandari ya Astakos huko Ugiriki zimezua kelele kutoka kwa wanablogu wa Kigiriki. Wanablogu hao walitumia huduma ya Twita kuchunguza swala hilo na kuitia shinikizo serikali ya Ugiriki kusimamisha usafirishwaji wa silaha hizo.
Usafirishaji wa shehena hiyo ulisitishwa, wakati serikali ya Ugiriki ilipobanwa na vyama vya upinzani pamoja na Shirika la Msamaha Duniani lilipokuwa likitaka vikwazo vya uingizwaji wa silaha nchini Israeli vipitishwe.
Awali, vyanzo kutoka serikalini vilipingana na habari iliyotolewa tarehe 9 Januari na shirika la habari la Reuters. Lakini watumiaji wa huduma ya Twita waliipata habari hiyo na kuipeleleza baada ya Indy.gr - tawi mojawapo la Indymedia Athens - kutoa tafsiri ya makala hiyo katika lugha ya Kigiriki.
Wazo la kuandaa vikwazo bandarini lilipendekezwa na likaenezwa kwa “kutuma tena na tena jumbe za Twita”:
itsomp: http://is.gd/f8Wa Je tunaweza kuandaa vikwazo kwenye bandari ya Astakos? Vikwazo kwa meli za Marekani na Israeli pekee…
Wengine walituma jumbe za twita moja kwa moja kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Ugiriki, waziri ambaye ana timu yenye akaunti katika huduma ya twita:
Dora Bakoyannis, Nini kinachoendelea kuhusu shehena inayosafirishwa Astakos? Hatutaki Ugiriki ihusishwe na mauaji yanayotokea Gaza.
Wakivunja utaratibu waliokuwa wakiufuata hapo awali wa kutojibishana kwa kutumia huduma ya twita, timu ya waziri [wa mambo ya nje] nayo ilijibu moja kwa moja:
… majibu kuhusu Astakos, http://tinyurl.com/9ts6xw
Kiungo hicho kilisababisha wizara itoe majibu rasmi kuwa suala la upitishwaji wa shehena hiyo ya silaha kwenye bandari ya Astakos au bandari nyingine yoyote nchini Ugiriki siyo “mada muhimu” kadhalika wizara hiyo pia ilikana kilichoripotiwa na vyombo vya habari.
Hata hivyo, tayari bloga Odysseas alikuwa ameshabaini mahali yalipo maombi ya upitishwaji wa shehena hiyo kwenye tovuti ya serikali ya Marekani:
Katika kiungo kinachofuata utaiona barua ya Jeshi la Marekani inayohusu usafirishwaji wa silaha kutokea bandari ya Astakos kuelekea bandari ya Ashdod, nchini Israel. Shehena hiyo ipo na inasubiri mkandarasi wa kuisafirisha
Pia watumiaji wa twita waliendelea kutia shinikizo, bila kujali maelezo yanayopinga ukweli huo kutoka kwa serikali:
Dora Bakoyannis, je vipi kuhusu tovuti inayotafuta mkandarasi?
Siku iliyofuata, vyombo vya habari viliripoti kuwa upitishwaji wa shehena hiyo umesitishwa. Hilo pia lilitangazwa kwa kutumia huduma ya twita mara moja:
Myrto_fenek: Usafirishwaji wa wa silaha kupitia bandari ya Astakos umesitishwa kutokana na mgogoro wa Gaza!
Bloga magicasland.com alitoa muhtasari wa matokeo:
Habari ya Shirika la habari la Ugiriki, APE inasema kwamba usafirishwaji wa makontena 325 ya silaha kutokea bandari ya Astakos kuelekea bandari ya Ashdod umesitishwa. […] Hapana shaka kwamba shehena hiyo itasafirishwa, isipokuwa siyo hivi sasa na si kwa kutokea hapa.
Bloga coolplatanos alichunguza zaidi na kubaini kwamba kuna maombi mengine zaidi ya upitishwaji wa silaha, na akahakikisha kwamba maombi yale ya awali yalikuwa yameshasitishwa:
… pia kulikuwa na maombi mengine awali ya haya, yaliyofanywa tarehe 6 Disemba, 2008 (Yalichapishwa kwa mara ya kwanza tarehe 4 Disemba), na Jeshi la Marekani. Hili ni ombi jingine la usafirishwaji wa silaha, kwa ajili ya shehena kubwa zaidi, kwani chombo chenye uwezo wa chini wa kubeba tani 989 kilitakiwa.
Haidhuru, leo tarehe 13 Januari [saa 03:00 kwa saa za mashariki], maombi ya chombo chenye uwezo wa tani 325 yalibadilishwa na kusomeka kuwa “yamesitishwa kwa wakati huu”.
Niangalia maombi hayo kwa kutumia zana ya utafiti ya Google kwenye mtandao wa Intaneti.