Palestina: Gaza Haitafuti Aspirini Kwa Ajili Ya Kidonda Chake

Wapalestina wachache na wanaharakati wakigeni bado wanaweza kutuma ripoti za kile kinachoendelea kwenye ukanda wa Gaza kwa kutumia umeme wa jenereta inapobidi. Zifuatazo ni jumbe za blogu katika masaa 24 yaliyopita.

Profesa Abdelwahed, ambaye anafundisha Kiingereza Chuo Kikuu cha Al-Azhar anaandika katika Moments of Gaza:

Leo yalikuwa mashambulizi ya nchi kavu. […] Raia wengi walifariki kwenye mashambulizi ya mabomu katika maeneo ya ukingoni mwa mji wa Gaza. Umeme na maji bado ni matatizo makubwa kwa wakazi wote wa Gaza. Bado ninatumia jenereta kuweza kuandika jumbe hizi! Simu za mikononi zimezimika na zile za majumbani zimeganda au hazisikiki vyema na wakati mwingine, husikika! Shambulio la anga karibu na hapa dakika chache zilizopita; hatujui lilitokea wapi lakini lilitisha. Walipiga jengo lililo karibu! Ni majengo matatu kutoka hapa nilipo; kuna majeruhi! Ndege za Israeli zinatupa mabomu ya radi au pengine ni miangaza inayotumiwa kwa madhumuni ya kijeshi. Israeli iliingilia idhaa ya setilaiti ya Al-Aqsa kwa mara kadhaa. Walitangaza habari zinazoipinga Hamas. Nitarejea tena kama nitaweza!

Natalie Abu Shakra, mwanaharakati wa Kilebanoni, ambaye pia anablogu katika Moments of Gaza:

Wanatumia silaha mpya… zinatisha sana… wakati zikipita angani… utazisikia ziko karibu sana na wewe… zinakuja, zinakuja kuniua, sasa hivi… hivi ndivyo unavyofikiri… inatisha mno… nakubali kwamba sijali tena… nimeshazoea zile silaha za zamani… na sasa inanibidi nizizowee na hizi pia… siwezi kukuelezea kwa maneno ukali wa vitisho hivi… ni kama kombora linaloelekezwa kwako… na mlio wake… mlio wa ndege angani ikikuelekea… ikiongeza sauti kadri inavyokukaribia zaidi… ikesha inapita juu ya vichwa vyetu… sote tumelala chini…

Laila El-Haddad, ambaye wazazi wake wako mjini Gaza, anablogu katika Raising Yousuf and Noor:

Tumesikia kuhusi vipeperushi ambavyo majeshi ya Israeli yanauchafua mji wa Gaza navyo – wakiwaambia watu kuwa Hamas ndio wa kulaumiwa kwa matatizo yao, na sio ndege za kijeshi za F-16 na mabomu mengine. Na hivi sasa wameanza kuwapigia watu simu kwa kutumia mashine za sauti kana kwamba ni Hilary Clinton, kwa muda wa masaa yote usiku na mchana. Baba yangu kapokea simu kadhaa – pamoja na ile wakati tulipokwa tunamaliza mahojiano na CNN, tulikuwa tukitumia Skype. Alijaribu kuiweka simu kwenye kipaza sauti ili nami niisikie. Tafasiri ya haraka haraka ni kuwa: “Ujumbe wa dharura: Onyo kwa raia wote wa Gaza. Hamas inawatumieni kama ngao. Msiwasikilize. Hamas wamewakimbia na wamejificha kwenye maficho yao. Achaneni nao…”

Aliweka simu chini kwa hasira, hakutaka kusikiliza ujumbe wote. Jeshi pia limekuwa likiwapigia simu watu kuwafahamisha kuwa nyumba zao zitashambuliwa. Watu wameacha kupokea simu zao, na hawapokei simu zenye namba wasizozifahamu kutokana na kuogopa.

Sharon ni mwanaharakati anayeblogu katika blogu ya Tales to Tell, na kama wanaharakati wengine wa kimataifa mjini Gaza, anafanya awezalo ili kuwasaidia wafanyakazi wa afya wa dharura:

1.30: Magari ya wagonjwa yameitwa. Tunashindwa kulipita shimo kubwa barabarani ambamo kuna gari lilikwishanasa ndani yake. Tulichukua njia ndefu ya mzunguko, tukamuokota mtu aliyevalia mavazi ya kitamaduni, wa makamo ndani ya miaka ya 60 hivi, kutoka katika linaloonekana ni shamba lake la ukoo. Anatokwa damu usoni na mwenye hofu kubwa. Njiani kuelekea hospitali ya Karmel Adwan mlipuko mmoja karibu kabisa na gari la wagonjwa ukalitetemesha gari. Lazima nilishtuka kiasi, kwa sababu dereva aliniuliza “je umesikia?”. Ninaanza kufahamu kuwa Wapalestina hupendelea sana kuuliza maswali yenye majibu yaliyo wazi, kama vile “unauonaje mji Gaza hivi sasa?”
[…]
4.55: Tunaondoka Al Shifa kurejea kwenye kituo cha Jabalia. Kuna kahawa. Mo anatengeza kahawa na mkate ambavyo si kawaida. Kuna ahueni kwenye idadi ya simu. Hassan ananiuliza kuhusu kitabu changu, “Tiba Asilia”; Ninamueleza kuwa ni kitabu kinachohusu safari ya mtaalamu wa mahusiano ya viumbe na mazingira kutoka kwenye ugonjwa wa mawazo. “watu huugua ugonjwa wa mawazo kwenye nchi za magharibi?” Aliuliza kwa mshangao. Ninaelewa isivyoweza kuyumkinika kusikika hivi sasa, nasema watu wengi hujikuta wamejitega katika maisha ya kazi na ununuaji wa vitu tu, bila ya kuwa na maana katika maisha yao – dini, au ndoto ya ukombozi wa nchi yako, au jambo kama hilo, watu wengi hupotea. “Kwa kweli Israeli inataka kutufanya tuwe hivyo hivi sasa”, alisema. “kwa mfano, saa nyingine jambo kubwa ambalo hulifikiria ni jinsi ya kupata kilo ya gesi, nilijenga jiko kwa ajili ya familia yangu na nilijisikia kana kwamba nilifanya jambo la kustaajabisha.”

Katika ujumbe mwingine anatuambia:

Tulimuuliza mtumishi wa mapokezi wa shirika la Hilali Nyekundu la Jabalia ni simu ngapi za dharura wanazozipokea kutoka sehemu ambazo Waisraeli hawawaruhusu kwenda. Maeneo hayo ni yale ambayo uratibu wake lazima ufanywe na majeshi ya uvamizi kupitia shirika la Msalaba Mwekundu. Alisema kuwa hawaruhusiwi kuhudumia asilimia takriban 80 ya simu zote zinazotokea kaskazini, amabpo ni sehemu za Beit Lahia, Beit Hanoun, na Jabalia. Naweza kurudia tena? Asilia 80. Wanane kati ya watu kumi wanaoomba msaada huzuiliwa kupokea msaada huo.

Mwanaharakati kutoka Kanada, Eva Bartlet, anblogu katika In Gaza:

Idadi ya walioteketezwa na kujeruhiwa ni kubwa mno hivi sasa – 521 na 3,000 kufikia asbuhi hii, kwa saa za Gaza – kuketi pembeni ya maiti au mtu anayefariki inakuwa ni jambo la kawaida. Doa la damu kwenye machela ya gari la wagonjwa linasogeea karibu ya koti langu, na mganga ananionya kwamba koti langu linaweza kuchafuka. Kwani ninajali?Doa lile haliwezi kunikera kama ambavyo ningekereka, au ambavyo nilikereka wiki moja iliyopita. Mauti yamejaa hewani, kwenye mitaa ya Gaza, na siwezi kusisitiza zaidi kwamba siongei kwa kutia chumvi. Nimerudi mjini Gaza kwa muda mchache, baada ya mchana na usiku wa kazi na wauguzi, nitajaribu kutoa muhtasari, ingawa kuna mengi ya kueleza, habari nyingi zinazojitokeza, na ni vigumu kuwafikia wananchi, hata wale walioko kilometa moja tu kutoka hapa. Kabla ya kunishusha wauguzi walikwenda kwenye vituo mbalimbali vya mafuta, wakitafuta mafuta kwa ajili ya gari la wagonjwa. Walipita vituo viwili bila kubahatika. Na wengine walipofika kwenye kituo cha mwisho walibahatika kujaza mafuta. Uhaba wa mafuta umefikia hali mbaya. Kadhalika uhaba wa mikate, ambao unaendelea, na foleni ni ndefu kuliko. Ujumbe wa maandishi kwenye simu ya mkononi unaniambia ( katika kipindi hiki inanibidi nitegemee habari kutoka kwenye simu ya mkononi kama inawezekana kupokea) kwamba Umoja wa Mataifa unasema kuwa watu 13,000wamepoteza makazi yao, na kwamba asilimia 20 ya waliokufa ni wanawake na watoto, asilimia 70 hawana maji salama ya kunywa. Kuna taarifa nyingi zinazoweza kumlevya mtu na ugonjwa wa kutojali, lakini siwezi kuwaambia yote hivi sasa.

Safa Joudeh anaandika kwenye blogu ya Lamentations – Gaza:

Israeli imetuingilia majumbani, inapigana katika mitaa yetu na unaonyesha unyama wake dhidi kwa nguvu zote. Je tujibu vipi? Makundi yote ya Wapalestinayameungana na yanampinga adui, kwa kutumia nguvu zao zote za kijeshi kwa pamoja. Japokuwa nguvu hizohaziwezi kulingana na nguvu zilizoshinikizwa na Israeli, zimetufanya tuwe na hakika zaidi kwamba Wapalestina watapigana mpaka mwisho kulinda kile kilicho chao. Imetuonyesha kwamba mapambano ya upinzani, kujitoa muhanga na mapenzi ni sehemu ya Wapalestina ambayo haitaweza kubadilika pamoja na dhiki zote zinazotusibu. Imetutia mwamko adili katika hisia zetu, mwamko ambao umetufikia katika wakati tunaouhitaji zaidi. […] Ni vigumu kukumbukawakati ambapo mahitaji ya msingi kama vile chakula, maji, vuguvugu la mapendo na mwanga wa juahavikuwa anasa. Katika kipindi hiki ni haja za kibinaadamu opekee ambazo zinafanya kazi, haja ya kuwalinda wale uwapendao, haja ya kuhakikisha unayo malazi na maamuzi ya haraka ya aidha kukimbia au kupigana. Tumekuwa tukikimbia kwa muda mrefu sana, Gaza ndiyo kwetu na ndiyo ngome yetu ya mwisho baada ya kupoteza makazi yetu kule panapoitwa Israeli hivi sasa. Haya yote yalitokea miaka 60 tu iliyopita. Jingine lipi wanalolitaka? Hatuna pengine pa kwenda. Huu ndio wakati ambao kila mbinu ya upinzani ni ruksa kutumika. Wamepuuza kila kila sheria ya kimataifa iliyopo. Kwa hiyo huu ndio wakati wa kupigana.

Rafah Kid anatoa rai:

Tafadhali… kabla ya kila mmoja kufa mjini Gaza… labda jaribuni kuelewa kuwa Hamas ni dalili… na sio chanzo… chanzo ni kukaliwa kimabavu… uhaba wa makazi uliotokana na watu kuhamishwa kwa nguvu kutoka kwenye ardhi yao… hicho ndio chanzo… Hamas ni dalili… na Marekani haizipendi serikali ambazo haikuziteua. Hakuna umeme… hakuna mawasiliano ya simu kwenda nje. Giza na mvua ya moto inanyesha. Watoto wanapiga mayowe.

Mutasharrid (mtu asiye na makazi) yupo huko Khan Younis, na ana hasira:

Niliulizwa jana kama misaada inafika Gaza au ni “habari tu ya kwenye magazeti”. Nilikataa kujibu kwani jawabu liko wazi, liko wazi kama ngurumo ya ndege za kijeshi za F-16 zinavyonguruma hivi sasa;usijali, misaada inayoingia Gaza, labda kwa kiwango kikubwa wakati wa siku zile za mwanzo, lakini ilisitishwa siku mbili zilizopita kwa madai ya operesheni ya kijeshi ya nchi kavu, hata hivyo, hilo halikubadili chochote! Yaani, ni vipi vyombo vya habari vimefanikiwa kuwasilisha shauri hili kama shauri moja la mtu mwenye njaa aliyezingirwa, anayetafuta misaada ya kibinaadamu na chakula kisichomfaa hata mbwa?! Nilipomuuliza raki yangu alinijibu “Waarabu ni mfano wa watu wanaompiga mbwa huku wakimrushia mnofu wa nyama!”

Gaza haitafuti aspirini kutibu jeraha lake, rafiki zangu, Gaza haitafuti bandeji kwa ajili kuziba mtiririko wa damu. Kitu kinachoiumiza Gaza, na hasa kitu kinachoiua Gaza zaidi ya makombora ni sauti yake: sauti ya kila mtu anayevalia suti na tai anayeizungumzia Gaza. Utatatamani uwapayukie kwenye nyuso zao, kabla ya ndege, “Nyamaza! Sauti yako inajeruhi na ina makali zaidi ya ukimya wako, kwa hivyo kaa kimya… Tuonee huruma, kaa kimya kwa kitambo kidogo…”

Mwanablogu Exiled anasema kwa ufupi:

Nakwenda mapumzikoni mpaka mwisho wa mauaji haya ya kinyama
Tuombeeni

Blogu yenye jina la Madhara kwa raia wakati wa mapambano mjini Gaza na Kusini mwa Israeli imetengenezwa na asaasi za haki za kibinaadamu za Kiisraeli ili kuorodhesha matukio ambayo hayaandikwi na vyombo vikubwa vya habari.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.