Huru Mchana, Usiku Kifungoni: Mwanaharakati wa Kimisri Azungumzia Masharti ya Kufunguliwa Kwake

Shawkan akiufurahia mchana kabla hajafungiwa tena wakati wa usiku. Picha imepigwa na Wael Abbas na kubandikwa katika ukurasa wa Mwanahabari za Picha huko Twitter.

Mwanahabari za picha wa Misri Mahmoud Abu Zeid, ambaye pia hufahamika kama Shawkan, alitumukia miaka mitano gerezani kwa kutimiza wajibu wake tu kama mwanahabari. 

Aliwekwa kizuizini Agosti 2013 alipokuwa akipiga picha mtawanyiko wa kikao cha Rabaa El Adaweya ambapo waungaji mkono wa Rais wa zamani wa Misri Mohamed Morsi walikusanyika wakipinga mapinduzi ya kijeshi ambapo uongozi wake uliishia Julai 3 mwaka huo huo. Vyombo vya ulinzi vya Misri vilipowatawanya watu hao, waliuwawa watu karibu 817 kujeruhi wengi wao na hii ni kulingana na Shirika la Haki za Binadamu.

Shawkan, aliyekuwa akifanya kazi na Demotix wakati wa kukamatwa kwake, alitumia karibu miaka minne akiwa mahabusu kabla ya kuanza kusikilizwa kwa kesi yake akiwa na watuhumiwa wengine 739 wa shauri lililokuja kujulikana kama “Kesi ya Mtawanyo wa Rabaa,” kuanza. Septemba 2018, Mahakama ya Jinai ya Cairo ilimkuta na hatia ya kosa la mauaji na kujihusisha na kikundi cha Kiislam Cha Muslim Brotherhood, na miezi michache baadaye aliachiliwa huru kutoka gerezani.

Wanaomuunga mkono Shawkan walifurahishwa kwa kumuona akiungana na wapendwa wake alipoachiliwa Machi 4. Lakini mwandishi huyo ni kuwa hayupo huru moja kwa moja. Kila siku jioni saa 12 anatakiwa kuripoti katika kituo cha polisi cha karibu naye na hulala hapo usiku wote kisha huruhusiwa tena kuondoka saa 12 asubuhi inayofuata. Shawkan anapaswa kufanya hivi kila siku kwa miaka mitano baada ya kuachiliwa kwake.

“Ninataka kuwa huru ili niweze kuyarudia maisha yangu ya kawaida,” Shawkan aliiambia Sauti ya Ujerumani-Deutsche Welle Baada ya kuachiliwa kwake  katika kipindi chake cha uangalizi.

Uko Twitter na Instagram, mwanahabari huyo amekuwa akitafakari na kushirikisha kuhusu maisha yake chini ya sheria hizi zinazombana na masaa yake ya uhuru kuanzia saa 12 asubuhi mpaka saa 12 jioni.

Machi 31, aliandika kuhusu yeye kutembelea mapiramidi huko Giza.

Mapiramidi yako kwa nyuma.
Matembezi katika eneo la karibu na kituo cha uangalizi (kituo cha polisi ambapo anatakiwa kulala usiku) kwa sababu ya (ukosefu Wa) muda.

Aprili 6 akitumia hashitagi ya نص_حرية# (“Nusu Uhuru”) alibandika picha huko Instagram, aliyopiga akiwa kwenye pikipiki. Alielezea kuwa ili kufika katika kituo cha polisi kwa wakati kila usiku husafiri kwa pikipiki ili kuwahi foleni barabarani .

Habari ya Shawkan sio mpya kwa Wamisri. Mwanablogu maarufu na mwanaharakati wa Misri Alaa Abd El Fattah, ambaye aliachiliwa huru kutoka gerezani Machi 28 naye yupo katika uangalizi na kwa muda wa namna hiyo hiyo. Alaa alitumia miaka 5 gerezani kwa kudharau zuio la maandamano na kama Shawkan anatakiwa kulala katika kituo cha polisi kila siku kwa kipindi cha miaka mitano.

”Uhuru kwa Alaa”. Tangu “aachiliwe huru” Alaa amekuwa akizungumzia kuhusu taratibu za uangalizi wake. Picha na Kampeni ya Uhuru kwa Alaa.

Alaa naye amekuwa akitafakari kuhusu maisha yake chini ya uangalizi huo.

“Ninafurahi kuiona furaha yenu juu ya kufunguliwa kwangu, lakini siko huru kwa kweli,” Alaa aliandika huko Facebook siku kadhaa baada ya kuachiliwa kwake. “Kila siku ninakutana na udhalilishaji unaoitwa uangalizi wa polisi.”

Katika bandiko jingine aliandika: “Sijui namna nzuri ya kuelezea hisia za kumuona Khaled (mwanae wa kiume) akijifunza kuogelea kwa mara ya kwanza. Lakini pia sijui jinsi ya kuuelezea ukatili wa kumuacha katikati ya mafunzo yake ili niwahi kwenye ukaguzi”

Dada yake Alaa, Mona Seif, ambaye pia ni mwanaharakati wa Haki za Binadamu, alifananisha masharti ya kifungo cha kaka yake kila siku usiku kama vile “Bughudha ya faragha”.

Alaa hutakiwa kujipeleka kwenye Kituo cha polisi cha Dokki kila siku saa 12 jioni na humwachilia huru kila siku saa 12 asubuhi.

Anaporipoti kituoni, humtenga na wengine katika kibanda kidogo cha mbao kilicho ndani ya kituo cha polisi na humfungia humo kwa masaa 12.

Hizi taratibu mbaya kabisa kuliko zile alizovumilia akiwa gerezani kwa miaka mitano. Alaa kwa sasa anatumia nusu siku yake kifungoni katika kituo cha polisi na anaitazama miaka hiyo mitano ya jinamizi hili

Alaa ametambua kuwa kuna hatari ya kuongezewa muda wa kifungo gerezani ikiwa ataendelea kuzizungumzia taratibu hizo. Katika usiku wa Aprili 9, maafisa wa usalama walimtishia kumrudisha gerezani ikiwa ataendelea kuzungumzia taratibu za kipindi chake cha uangalizi.

Ahmed Maher, mwanaharakati za kisiasa aliyekuwa na harakati za vijana Aprili 6, alitumikia miaka mitatu gerezani kwa kufanya maandamano haramu. Aliachiliwa huru  Januari 2017 na aliwekwa chini ya uangalizi wa polisi kwa kipindi sawa na kile alichokaa gerezani. Huko Twitter, alielezea taratibu za wakati huo:

Chini ya uangalizi wa polisi, tulipokuwa tunalala palikuwa pachafu kuliko gerezani na kulikuwa na uholela uliopitiliza ingawa kulingana na sheria, hawakuwa na haki ya kutufungia kwenye vituo vya polisi au kutunyima watoto wetu, kazi zetu, masomo na maisha yetu ya kawaida. Kulingana na sheria, uangalizi unatakiwa uwe wa Kistaarabu na wa kkibinadamu lakini ni wazi kuwa msingi wake ni kiu ya kuumiza na kudhalilisha

Kitendo hiki cha kuwafungia wafungwa wa zamani wakati wa usiku ni kutumia madaraka vibaya. Kulingana na Mchambuzi wa sheria na taasisi binafsi ya Haki za Binadamu, wale wote waliowekwa chini ya uangalizi wa polisi wanapaswa wawe wanatumia usiku majumbani mwao. Wale pekee ambao hawana sehemu ya kuishi karibu na kituo cha polisi ndio wanaotakiwa kulala kituoni chini ya Uangalizi maalum.

Yasmin Omar na Mai El-Sadaby wa Taasisi ya Sera za mashariki ya kati Tahri waliandika:

Baada ya mtu kuhukumiwa kwa kipindi cha uangalizi kilichoamuliwa na jaji wakati wa hukumu, sheria huwasaidia waliohukumiwa kutengeneza makazi ambapo atatumia kwa muda wa kutumikia kipindi chake cha uangalizi. Hata hivyo, kwa kuongezea mamlaka hupewa nafasi ya kuchagua eneo la uangaliIzi ikiwa makazi hayatatolewa pia kuangalia kama eneo lililochaguliwa na mtuhumiwa linafaa kwa uangalizi wa polisi au lah. Busara hii imekuwa ikitumika kuondoa haki ya mtuhumiwa kumaliza muda wake wa uangalizi katika maeneo yaliyotajwa, haki ambayo amepewa chini ya sheria na badala yake huwalazimu watu wenye makazi yao sehemu polisi wanaweza kufanya ufuatiliaji wao kutumia muda wao kwenye vituo vya polisi .

Lakini mwisho wa kila siku WaMisri wengi wanalazimishwa kurudi kwenye vyumba vidogo vya selo za polisi, mbali na wawapendao na ulimwengu wote: wako nje ya magereza lakini hawako huru kwa kweli. Wengi wao ni wanaharakati, waandamanaji na wanahabari ambao kosa lao pekee lilikuwa ni kutumia haki yao ya msingi ya uhuru wa kujieleza, kukusanyika na kuandamana.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.