Bloga wa Ki-Mauritania Akwepa Adhabu ya Kifo, Lakini Amebaki Kifungoni

Ould Mkhaitir alihukumiwa kifo mwaka 2014 kutokana na maoni aliyoyatoa katika kipande cha habari kilichochapishwa mtandaoni.

Pamoja na hukumu yake ya kifo kubadilishwa  zaidi ya mwaka mmoja uliopita, mwanablogu wa Mauritania Mohamed Cheikh Ould Mkhaitir bado yuko gerezani

Ould Mkhaitir alihukumiwa kifo mwaka 2014 baada ya kutoa maoni katika makala iliyochapishwa katika tovuti ya gazeti la Aqlame. Katika makala hiyo yenye kichwa cha habari “Dini, Udini na Wafanyabishara”, Ould Mkhaitir alikosoa majukumu ya mfumo wa dini nchini Mauritania na alitumia hadithi za maisha ya Mtume Muhammad kuthibitisha maoni yake. Makala halisi iliondolewa katika tovuti hiyo na Aqlame lakini bado ipo katika mitandao

Mahakama ilimkuta na kosa la “kuisaliti dini” na alihukumiwa kifo chini ya Kifungu cha sheria 306 na Hukumu ya Kifo ya Mauritania.

Hapo April 2016, mahakama ya rufaa iliendelea kukazia hukumu hiyo na kuihamishia kesi yake katika mahakama kuu ambapo nayo iliirudisha  kesi hiyo katika mahakama ya rufani kwa sababu ya “kukiukwa kwa taratibu”. Hapo Novemba 2017  hukumu yake ya kifo ilibatilishwa na kupunguzwa hadi kifungo cha miaka miwili gerezani na faini  katika mahakama ya rufaa. Hata hivyo, pamoja na kuwa alishakaa gerezani zaidi ya miaka miwili, mamlaka husika hazikumwacha huru Ould Mkhaitir. Karibu miezi 18 baada ya uamuzi wa mahakama ya rufaa kumwachilia huru, ameendelea kuwa kizuizini.

Hapo Aprili 24, 2019 Waziri wa sheria wa Mauritania alisema kwamba Mkhaitir alikuwa katika  “kizuizi cha muda mfupi” na ndio maana “ni mahakama kuu pekee inayoweza kutoa uamuzi wa majaaliwa yake”.

Kifungu cha sheria namba 306 cha hukumu ya kifo, mwanzoni kilikuwa kinasema kuwa ikiwa aliyehukumiwa “atatubu” kabla ya kunyongwa kwake, mahakama kuu ya Mauritania inaweza kubadili hukumu ya kifo kuwa kifungo cha miezi mitatu mpaka miaka miwili gerezani pamoja na faini.

Lakini hapo Aprili 2018, Bunge la Mauritania lilipitisha sheria kuwa hukumu ya kifo ni lazima kwa yeyote atakayekutwa na makosa ya “kutoa kauli za dhihaka”  na matendo ambayo ni “ya kudhalilisha vitu vitakatifu”.

“Kutungwa kwa sheria hii kunahusishwa na kesi ya Mkhaïtir kwa sababu ni miezi michache tu baada ya Mahakama kuu kuamuru Mkhaïtir kuachiliwa huru,”  Shirika la Uangalizi wa Haki za Binadamu walisema haya hapo Novemba 2018.

Ni makosa makubwa kukosoa ukabila na mfumo wa udini nchini Mauritania, na vimetengenezwa vitisho vingi vya kisiasa na kisheria dhidi ya wanahabari na wanaharakati katika miaka ya hivi karibuni. Mwaka 1981, Mauritania ilikuwa nchi ya mwisho kabisa duniani kukomesha biashara ya utumwa na ilifanya utumwa kuwa jinai tu, mwaka 2007. Lakini kuanzia wakati huo wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na wafanyakazi wa Haki za Binadamu wamekusanya nyaraka zinazothibitisha kuwa watu weusi wa kabila la Waharatine bado wako katika utumwa wakiishi maisha magumu ya kutumikishwa kwa lazima, na pia hukumbana na ubaguzi wa kidini.

Serikali ya Mauritania hukataa kuendelea kuwepo kwa utumwa katika nchi na watu wengi kama vile Ould Mkhaitir, ambao huzungumza wazi kuhusu matendo ya ubaguzi dhidi ya Waharatine wamekuwa wakishtakiwa na kufungwa. Septemba iliyopita mamlaka  zilimfunga mwanaharakati Abdallahi Salem Ould Yali, kwa kutuma ujumbe katika kundi la WhatsApp wenye  uchochezi na kueneza chuki za kikabila na kuharibu  usalama wa jamii yake.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.