Misri: Sisi sote ni Laila


Sisi sote ni Laila, ndivyo wanavyosikika kusema kwa sauti moja wanablogu wa kike wa Misri. Hivi, huyu Laila ni nani na kwa nini wasichana na wanawake wa kiMisri wanapenda kufananishwa naye? Hebu endelea kusoma ili uone ni kwa namna gani wanablogu wa Misri wanavyojihangaisha ili kuvunjilia mbali vikwazo vya jinsia na kufanya sauti zao zisikike.

Vuguvugu hili lilianza mnamo mwezi Septemba, 2006, wakati ambapo kikundi cha wanablogu kiliamua kwamba ilikuwa imefika wakati kwa wao kuzungumza na kushirikisha hisia na uzoefu wao, na yale yanayogusa wanawake wengine, hasa chini ya mfumo usio na haki.

Sakata zima lilianza kama ifuatavyo:

Wazo hili la ‘Sisi sote ni Laila’ lilianza na Laila, mwanamke aliyekuwa akieleza mambo na hisia zake za ndani kwa mwanamke mwingine aliyeitwa Laila. Mara idadi ya kina Laila iliongezeka kutoka wale wawili hadi watatu, watano na hatimaye zaidi ya hamsini, ambao kwa pamoja waligundua kwamba licha ya tofauti zao katika mazingira, mawazo na vipa umbele, walikuwa wote ni akina Laila. Laila ni shujaa mwanamke wa Mlango Ulio Wazi, hadithi iliyotungwa na Latifa Al Zayat, ambayo baadaye ilitumika kutengeneza filamu ambamo Faten Hamana ndiye aliyekuwa mwigizaji mkuu. Laila ni msichana yeyote wa kileo wa Misri, ambaye anakabiliana na mazingira tofauti katika jamii ambayo inatukuza sana wanaume na kuwadharau wanawake. Hakuna anayejali kuhusu ndoto za msichana huyu wala mawazo yake na hasa nini kile ambacho angependa kuwa maishani. Licha ya vikwazo vyote hivi, Laila, ambaye alinyanyaswa tangu utoto wake, bado aliweza kuendeleza imani yake kwake mwenyewe, na hasa msimamo wake kwamba wanawake walikuwa sawa na wanaume – iwe nyumbani, kazini, shuleni au katika jamii nzima kwa ujumla.

Tulimchagua Laila kwa sababu anawakilisha hali ya Mmisri, ambapo anaonyesha hali halisi tunayopitia na chokochoko zilizojijenga katika jamii ya WaMisri, utamaduni na msimamo wake dhidi ya wanawake katika historia nzima. Hii haimaanishi kwamba wanablogu kutoka katika nchi nyingine za KiArabu hawawezi kushiriki katika sakata hili, la hasha, maana utamaduni huu unaomkandamiza Laila upo pia katika nchi hizo.

Lengo letu kuu leo ni kumpa Laila fursa ya kusema na kuwasikia wengine wakimzungumzia, ili atambue kwamba hayupo peke yake katika kukabiliana na ukosefu wa haki ambao mara nyingi yeye hujikuta akiupitia. Lengo letu ni kuwa na sauti inayoeleza mateso yetu kwa kuwa tumekinaishwa kuona wengine wakitusemea. Lengo letu la juu ni kukushirikisha kiini muhimu cha uwepo wetu, sehemu ile iliyojificha vema ndani ya dada yako, mkeo na mfanyakazi mwenzio … sehemu ile ambayo wewe mara nyingine unaichangia kwa kujua au kutojua.

Tangia hapo mjadala huu umeendelea huku kila mwaka kukiwa na mafanikio zaidi – wanablogu wengi wa kike wakifunua nyoyo zao na kueleza kinagaubaga yale yanayowasibu, na kwa namna ya kushangaza wakipata pia mwega kutoka kwa wanaume.

Mwaka uliofuata, Sisi Sote ni Laila, aliandika:

Mwaka mmoja umepita tangu Sisi Sote ni Laila ya kwanza .. wazo lilikuwa ni kupata idadi kubwa ya wanablogu wanawake wakiandika kuhusu matatizo wanayokabiliana nayo, ili kutoa fursa ya kujadili jambo hili katika ulingo ulio wazi, ambao unatoa kiwango fulani cha uhuru na kujitambua. Lengo lilikuwa ni kujifunua na kushirikishana na vilevile kujiondoa kutoka katika upweke wakati wa kukabili matatizo haya. Kusudio lingine lilikuwa ni kutumia kuaminika kwetu katika ulimwengu wa blogu kueleza matatizo tunayokumbana nayo, hasa kuonyesha jinsia nyingine waone matatizo yetu kama sisi wenyewe tunavyoyaelewa na kuyaeleza. Ilikuwa ni fursa nzuri kwetu kuelewana na kuona jinsi kila mmoja wetu anavyojaribu kujikwamua dhidi ya unyanyasaji unaoelekezwa kwetu, hata kama ni kwa kiwango kidogo, ambao unajumuisha yeye mwenyewe na nyumba yake.

Matokeo yake yalikuwa ni muundo tofauti wa uchangiaji ili kuadhimisha siku hiyo, ambapo hata wanaume nao walichangia katika mazungumzo.

Mtandao wa Sisi Sote ni Laila unaeleza:

Licha ya mafanikio ya siku hiyo, bado tulikosolewa katika mambo kadhaa, kubwa zaidi likiwa ni kuwapuuzia wanaume, na kutobainisha vema mada za kujadili. Mwaka huu tutajaribisha kusahihisha makosa hayo. Safari hii, tulichagua kuisherehekea siku hii kwa mtindo tofauti, kwa kuuliza maswali fulani bainifu, yaliyochaguliwa kwa umakini mkubwa kabisa na marafiki wachache, ambayo yanalenga hasa hadhi ya wasichana na wanawake wa ki-Misri, kwa namna ya pekee, na Wa-Misri kwa ujumla. Lengo ni kuendeleza majadiliano yaliyochipuka kutoka kwenye mijadala ili tupate kujielewa wenyewe zaidi na wale wanaotuzunguka.

Maadhimisho ya mwaka huu ya Sisi Sote ni Laila yatafanyika katika blogu mbalimbali mnamo Oktoba 19. Hebu keti mkao wa kula kwa yale atakayojiri siku hiyo.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.