Bahrain: Raha na Karaha za Kusoma Ng'ambo

Ingawa Bahrain ina idadi kadhaa ya vyuo vikuu, vya umma na binafsi, raia wengi wa nchi hiyo hupata fursa ya kwenda ng'ambo kwa masomo ya shahada ya kwanza na hata zile za juu, mara nyingi kwa kutegemea ufadhili. Moja ya matatizo ya kwanza wanayokumbana nayo huko ughaibuni ni kwamba watu wachache tu hufahamu ni wapi Bahrain ilipo. Katika makala hii tunafuatilia uzoefu wa wanablogu watatu ambao ndiyo kwanza wamekwenda ng'ambo kwa masomo: kule Japan, Uingereza na Marekani na mwanablogu wa nne ambaye anasoma India kwa kipindi fulani hivi sasa.

Cradle of Humanity amekwenda masomoni huko Cleveland, Ohio (Moja ya jimbo la Marekani, na anajihisi kukanganyikiwa na hali ya mambo huko:

Mara nyingine huogopa pale watu wanaponiuliza juu ya kule ninakotoka. Si zaidi ya asilimia 10 ya wale wanaosikia nikitamka “Bahrain” kama jibu la kule nitokako wanaelewa au kuwa na picha kichwani juu ya mahali nchi hii ilipo, lakini hicho siyo hasa kinachonisababishia simanzi. Kwa wale wanaofahamu kwamba Bahrain ipo katika Ghuba ya Ajemi, kuna kitu ambacho huwaingia vichwani – utajiri. Mara nyingine baadhi yao huuliza, lakini hawa ni wale ambao nadhani hunitia simanzi zaidi. Ndani ya miezi miwili iliyopita nimepata marafiki wengi sana, hasa Wahindi kwa kuzingatia idadi ya wanafunzi walio katika Kozi ninayochukua. Licha ya ukweli kwamba wengi wao katika hawa ni Wahindi wa hali ya juu, wanaomiliki biashara nyingi na wao wenyewe ni matajiri – wanapenda sana kunieleza kwamba kwa vyovyote mimi pia lazima niwe mtu tajiri. Mara nyingine nilipoeleza kuhusu ninakotoka wapo wanaoamini kwamba sisi ni matajiri kupita kiasi, lakini utajiri ambao hatukuustahili; wakati ambapo wao waliufanyia kazi utajiri wao. Zaidi sana ni kwamba mara nyingi wanachanganya kati ya Bahrain na Dubai.

- Usafiri wa umma hapa si mzuri sana, lakini kumiliki gari pia ni ghali mno, vinginevyo ningekuwa nimeshajipatia moja
– La mtumba au jipya?
– La mtumba, mie nipo hapa kwa kipindi kifupi tu.
– Si afadhali ununue jipya, hilo ni bora zaidi.
– Lakini hilo litakuwa ghali sana.
– Wewe si unatoka Bahrain, unaweza kununua gari!

- Unamaanisha wewe si tajiri?
– Kwa kusema ukweli mimi si tajiri.
– Haiwezekani, kule Dubai kila mmoja ni tajiri.
– Kuhusu Dubai, sijui, lakini kule Bahrain si kila mtu ni tajiri.

Yagoob, ambaye amewasili huko Nagoya, yeye anakabiliana na tatizo la msingi zaidi – lugha:

Kwa kusema ukweli, tofauti ya tamaduni imenistusha mno! Yaani nimekutana na watu wachache mno wanaozungumza Kiingereza. Najihisi kama mtu wa zama za mawe aliye katika karne ya 21, maana natumia njia za kijima kabisa ili kuwasiliana, huku nikitumia ishara za mikono na kuzungumza taratibu kwa sauti ya juu katika Kiingereza. […] Chumba changu cha kulala bwenini ama kwa hakika ni cha Kijapani, ni kidogo na kila kitu kimewekwa tayari kukabili matetemeko ya ardhi, yaani ni kama kuishi katika kopo la dagaa wa kusindika. Karibu kila kitu kilicho chumbani mwangu kimewekewa maelekezo, lakini yote kwa Kijapani kwa hiyo sijui yanatumikaje mpaka sasa! […] Njia ya treni za chini kwa chini inanikumbusha ile ya kule Landani tofauti tu ni kwamba hii ni safi zaidi na mtu kama mimi nakuwa nimejitokeza mno kama dole gumba lililovimba (bila shaka mahali popote mwarabu mrefu, mnene mwenye vinyweleo na jasho jingi angeonekana zaidi). […] Yaelekea watu wa hapa Nagoya hawajawahi kukutana na yeyote kutoka Bahrain, walau hicho ndicho wanachonieleza watu wanaofanya kazi katika bweni langu, hata hivyo nashangazwa na ukweli kwamba wanajua kule ilipo nchi hiyo (pengine ni kwa sababu ya mapambano makali katika viwanja vya kandanda miaka ya hivi karibuni) na nilipozungumza na mmoja wa majirani zangu wa Kichina, ‘Andy’, alisema, “Ooh, kumbe wewe unatoka Asia Magharibi!” na nafikiri yuko sahihi … hasa ukizingatia kwamba sasa nipo huku Mashariki ya Mbali.

MuJtAbA AlMoAmEn anasoma kule India, na anatuambia ni nini kinachomfanya apende kuwa huko:

Inawezekana kwamba kuwa mbali na nyumbani kuna ubaya wake, lakini hakuna shaka kwamba kuna upande mzuri pia. Nimewahi hapo kabla kujadili faida na hasara za kuwa mbali na nyumbani; sina lengo la kujirudia, na kwa hiyo leo nitaandika kuhusu kitu tofauti. Nataka kuandika kuhusu tafakari, utulivu, uwezo wa kusoma na muda wangu huru ninaoweza kuutumia kwa malengo mazuri.
Niwapo Bahrain, kati ya ndugu na marafiki, huwa sipati muda wa kusoma magazeti, yawe ya palepale nchini, ya Kiarabu au hata ya kimataifa. Pia sipati muda wa kusoma vitabu kama vile kuhusu maisha ya watu binafsi, hadithi, au hata kuhusu mada za kujiendeleza kiakili.
Hapa India, kuna muda tele wa kujitafakari. Najisikia kuwa na utulivu wa kiakili na kwa hiyo naweza kufikiri sana – najikuta naweza kupata suluhu kwa karibu kila tatizo au kikwazo kinachonikabili, na kitamu zaidi ni kwamba napata suluhisho zaidi ya moja kwa tatizo fulani. Nakuwa sitegemei suluhisho moja tu, kwa hiyon naweza kupima masuluhisho
mbalimbali niliyo nayo, na kama hii ina maana yoyote, basi walau ni ushahidi wa utulivu wa kiakili na kiroho nilio nao kwa sasa.

Bride Zone ndiyo kwanza amewasili Uingereza, na tayari mwanadada huyu anakumbuka nyumbani:

Nashindwa kukana jinsi gani ilivyo vigumu kuwa mbali na nyumbani. Dunia ni Dunia, sayari ya tatu kutoka kwenye jua katika mfumo huu wa jua. Sote tulijifunza jambo hilo na tunalichukulia kuwa ni ukweli wa kisayansi. Lakini ukweli ni kwamba Dunia yetu siyo ileile endapo utaondoka na kwenda mahali pengine. Nchi ile nilikokulia na kuishi maisha yangu
yote, pamoja na uzuri na ubaya wake, na ambayo imewabeba ndugu na marafiki zangu kwa kweli ni kipenzi changu kuliko nchi na ardhi nyingine zote Duniani. Licha ya uzuri wa nchi ninayoishi hivi sasa – haina thamani hata ya chembe ya mchanga ikilinganishwa na nchi yangu ninayoipenda sana.

Hapa Uingereza, hali ya hewa ni ya kupendeza mno. Nimeyaona majira ya mapukutiko ambayo sikuwahi kamwe kuyaona maishani mwangu. Tulipokuwa shule tulijifunza kwamba kuna majira fulani ya mapukutiko ambapo miti ilipukutisha majani, nilikuwa sijawahi kuliona jambo hilo isipokuwa hapa. Na wakati ambapo sisi kule nyumbani tuna uhaba wa
mvua, hapa inanyesha sana na kunifanya kutamani maisha zaidi, maisha yanayohuishwa na mvua, na kufanya chemchem ambayo bado inaendelea kuwepo.

Hivi ninapata maruweruwe? Sioni uhusiano wowote uliopo kati ya maneno niliyoandika kwenye kurasa hizi zaidi ya maneno ambayo yamekuwa yakiisongasonga akili yangu na ambayo nimeyefasiri katika kidirisha hiki kidogo ninachotumia kuitazama dunia. Tafadhali nisameheni rafiki zangu. Sitaki kuzungumzia kingine chochote kile isipokuwa upendo na hamu ya kuwa katika ardhi na taifa langu.

1 maoni

  • najifunza kutengeneza blogs kama ulivyoona hapo ukifugua na marfekebisho yanaruhusiwa ila matusi no na peruzi penye mianya ya kupenyesha wawekezaji na watangazaji wa biashara zao

jiunge na Mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.