Mwishoni mwa mwezi Septemba, Barbara Hogan, aliteuliwa na Rais wa mpito Kgalema Motlanthe kuwa waziri mpya wa afya wa Afrika ya Kusini, akichukua nafasi ya mtangulizi wake mwenye utata mwingi, Manto Tshabalala-Msimang. Wanaharakati wa masuala ya UKIMWI na raia wengi wa Afrika ya Kusini wana matumaini makubwa kwamba hatua hii huenda ikaashiria mabadiliko ya sera za serikali kuhusu suala la VVU na UKIMWI.
Hogan, mwanamama mwanaharakati mkongwe dhidi ya ubaguzi wa rangi na mwanachama wa muda mrefu wa ANC, yaani African National Congress, hapo awali alikuwa mwenyekiti wa kamati ya kusimamia masuala ya fedha. Tangu kuteuliwa kwake kuwa waziri wa afya, amebadili mwelekeo wa serikali iliyopita kuhusu VVU na UKIMWI na kuapa
kutoa kipaumbele kwa masuala ya UKIMWI. Jambo hili limezua mshawasha miongoni mwa raia wa Afrika ya Kusini, ambapo wengi wao wanaamini kwamba Hogan anaweza kuimarisha vita vya nchi dhidi ya VVU na UKIMWI kwa kufuata sera yenye kuzingatia mtizamo wa kisayansi zaidi. Katika picha hii ya video, wanaharakati wa masuala ya UKIMWI wanashangilia uteuzi wa Hogan katika nafasi yake hiyo mpya.
Siku za nyuma Hogan alipata kumkosoa waziwazi Rais wa zamani Thabo Mbeki na msimamo wake juu ya sera ya VVU na UKIMWI. Wastani wa watu milioni 5.7 nchini Afrika ya Kusini wanasemekana kuishi na VVU na kiasi cha watu 350,000 walifariki kutokana na UKIMWI mwaka jana nchini humo (wastani wa watu 1,000 kila siku). Kwa upande mwingine Tshabalala-Msimang amelaumiwa vikali kwa kutofanya juhudi za kutosha kukabili tatizo la VVU na UKIMWI nchini humo. Waziri huyo wa zamani wa afya alihamasisha matumizi ya vyakula kama vile beetroot, vitunguu saumu na vinginevyo kama tiba ya VVU na UKIMWI, jambo lililosababisha watu kumbatiza jina la “Dkt Beetroot”, na zaidi ameshutumiwa kwa kusababisha mkanganyo kuhusu matumizi ya dawa za kurefusha maisha (ARV).
Stephen, akiandika kwenye tovuti ya irreverence, alimuita Tshabalala-Msimang kama aibu ya taifa na papo hapo akimwita Hogan kama tumaini lililorejea. Ciaran Parker, akitumia blogu yake ya Ciaran’s Peculier [sic] Blog, anafafanua kuhusu msimamo wa Tshabalala-Msimang usiokubaliwa na wengi:
“Ingawa Kgalema Motlanthe ameahidi kutoleta mabadiliko makubwa, bado ameatosa baadhi wa mawaziri wenye utata mkubwa waliokuwa kwenye serikali ya Mbeki. Mmoja wao akiwa ni Waziri wa Afya, Dkt Manto
Tshabalala-Msimang, aliyekuwa mwananadharia mkubwa katika hoja ya Mbeki ya sera za kukana uwepo wa UKIMWI. Serikali ya Mbeki ilikataa katakata kuona uhusiano uliopo kati ya VVU na UKIMWI, na waziri wake wa afya alijenga hoja kwamba hata dawa za kurefusha maisha, ambazo kwa kweli zimeonyesha kusaidia katika juhudi za kukabili gonjwa hili, zilikuwa ghali mno … Wataalamu wa afya wanaofanya kazi nchini Afrika ya Kusini na ambao walipingana waziwazi na nadharia za kushangaza za waziri huyu walijikuta wakifanywa kuwa wahanga.”
Mapema juma lililopita, wakati wa uzinduzi wa mkutano juu ya Chanjo ya UKIMWI ya Kimataifa ya 2008 (International AIDS Vaccine 2008) huko Cape Town, Hogan, alitangaza hadharani kwamba VVU husababisha UKIMWI na kwamba ni lazima kukabiliana nao kwa kutumia dawa za hospitalini. Pia alieleza kwamba serikali ilikuwa na nia ya dhati
kuongeza nguvu katika programu za kuzuia uambukizaji wa kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, dawa zinazozuia akina mama wajawazito wenye VVU kuwapatia watoto wao ambao hawajazaliwa maambukizo na kueleza kwamba chango madhubuti ya VVU ilikuwa ikihitajika mno.
Wanasayansi, wanaharakati na wanablogu wengi wameeleza furaha yao kufuatia hotuba iliyotolewa na Hogan. Haley, akiblogu katika tovuti inayoitwa ujasura kama mwanafunzi balozi, ana hili la kusema:
“Kusema kweli, watu wengi ninaozungumza nao wanashangazwa na jambo hili – kwamba maafisa wa serikali waliochaguliwa kwa njia za kidemokrasi wanakana fikra … kwamba … VVU husababisha UKIMWI. Hata hivyo, kwa bahati mbaya, hapa Afrika ya Kusini hivyo ndivyo hali ilivyokuwa … lakini sasa mambo yamebadilika, msimamo si huo tena.”
Ray Hartley, anayeandika katika The Times, Afrika ya Kusini, anablogu akiongeza:
“‘Tunajua kwamba VVU husababisha UKIMWI.’
Kwa kauli hii, Waziri wa Afya, Barbara Hogan, amehitimisha muongo mzima wa aibu ya kukana uwepo wa UKIMWI jambo ambalo limeigharimu Afrika ya Kusini idadi isiyohesabika ya maisha ya binadamu, wakati huohuo wale waliokuwa wakiishi na VVU wakiishia kuishi kana kwamba kwenye kivuli chao wenyewe.”
Ni vigumu kueleza idadi kamili ya watu walioathiriwa na sera zilizopita juu ya VVU na UKIMWI, lakini Shirika la Treatment Action Campaign (TAC) (Kampeni ya Kutetea Tiba) linakadiria kwamba kiasi cha raia milioni mbili wa Afrika ya Kusini walikufa kutokana na kuugua UKIMWI katika kipindi ambapo Mbeki alikuwa madarakani, na kwamba walau jumla ya vifo 300,000 vingeweza kuepukwa endapo tu angetimiza baadhi ya mambo ya msingi ya kikatiba. Baadhi ya wanablogu wanasema kwamba wote wawili, Mbeki na Tshabalala-Msimang wametapakaa damu mikononi mwao. Soneka Kamuhuza, anayeandika kupitia blogu ya Things That Make You Go Mmmh! anamshutumu vikali Mbeki.
“Umawazo mgando wao [Mbeki na Tshabalala-Msimang], umbumbumbu wa kukusudia na kujitia kwao kuwa wanyofu kulichochea tu uendelevu wa janga hili. Kutumia njia ya kutazama tatizo zima kwa upana badala ya chanzo chake, pasipo kuingiza na njia nyingine, hakuwezi kuwa njia madhubuti ya kutibu VVU, waliingiza nchi katika wakati mgumu kwa kutumia umbumbumbu wao ambao waliulinda kwa njia zote. Hivi sasa inakadiriwa kwamba Afrika ya Kusini inaongoza duniani kwa kuwa na idadi kubwa ya watu wanaoishi na VVU. Kwa namna fulani, naona ushawishi wa Mbeki katika jambo hili … Katika nchi ambayo ina utajiri mkubwa wa maliasili, amehadaa rasilimali watu iliyo muhimu sana, kwa kuwanyima fursa ya watu kuamua na kuanza kupambana na tatizo hili la UKIMWI kikamilifu.”
Wengi wanaamini kwamba Hogan atarekebisha mambo yaliyoharibika kwa sehemu fulani. Makala katika Peripheries inaonyesha kwamba watu wanatarajia kwamba wakati wa kuwa na ukanaji wa UKIMWI huku ukipewa nguvu na msukumo wa kisiasa nchini Afrika ya Kusini tayari umefikia kikomo. Hata hivyo, wapo ambao hawako kupaparikia mambo haraka hivyo. BillyC, akitoa maoni yake juu ya makala iliyoandikwa katika The Times, la Afrika ya Kusini anasema:
“Barbara Hogan ana kazi kubwa mbele yake ili kurekebisha mambo ambayo kwa kiasi fulani tayari amekwishasababisha madhara kwa mfumo wa afya katika uangalizi wa Manto. Uwezo wa wafanyakazi, ari ya kazi, na viwango vya utendaji ukiachia mbali sera za afya na sheria, yote ni mambo ambayo hayana budi kushughulikiwa. Zaidi ya hilo, kuna uhamasishaji wa matumizi ya dawa na upungaji pepo wa kivuduu, vilevile uhusianishaji wa kishetani na sayansi ya magharibi vyote vikiwa vimejikita sawasawa katika mfumo wa kufikiri wa taifa. Itachukua miaka mingi ya kazi ngumu, yenye kujaa ujasiri na unyoofu ili kuturejesha katika mfumo wa afya ulio wa heshima na wenye ufanisi. Tumwombee Barbara Hogan apate kasi. Kusema kweli anaihitaji.”
Picha ya Utepe wa Ukimwi wa Afrika ya Kusini imetoka kwa mvcorks katika mtandao wa picha wa Flickr.