Saudi Arabia: Kina Mama Huru

WAKATI kukiwa hakuna shaka kwamba kuna vizuizi kwa wanawake waishio Saudi Arabia, havifanani na taswira iliyojengwa na wageni dhidi ya taifa hilo. Katika makala hii tunao ushauri kwa wakina mama wanaotaka kutembelea jiji la Jeddah wakiwa peke yao, kuna muhtasari wa hoteli za kina mama pekee jijini Riyadh, na wito kwa wageni wote wanajihisi kuzungumza kwa niana ya kina mama wanaokandamizwa wa Saudia.

Tunaanza na Hala, ambaye anaishi Marekani hivi sasa na anablogu katika blogu yake HALA_IN_USA, anayetoa ushauri kwa marafiki zake akinamama wasio na waume watakaotaka kutembelea jiji la Jeddah kwa mara yao ya kwanza:

Wanawake katika jiji la Jeddah huvaa gauni lijulikanalo kama “Abaya“, gauni hili hupaswa kuvaliwa juu ya mavazi mengine hivyo vaa nguo nyepesi za ndani haswa wakati wa majira ya kiangazi. Ushungi si lazima kwa akina mama wageni lakini ni vazi linalopendekezwa kuvaliwa (kwa ajili ya usalama na kuepuka usumbufu usiokuwa wa lazima) katika maeneo ya kiutamaduni.

Kuna maeneo mbalimbali ya kuyaona jijini Jeddah, ninapendekeza Balad, jiji la kale la Jeddah, likiwa na majengo yaliyosanifiwa kizamani, Jengo la Naseef ni mfano mmojawapo wa majengo ya kale. Unaweza kununua bidhaa za kitamaduni za kale kutoka katika maduka ya kizamani na ukafurahia marashi ya Kiarabu kama vile Udi Bukhour, vilevile kuna bidhaa za kazi za mikono za kitamaduni kama balbu, [fanusi], tende, pipi na vitambaa vya rangi mbalimbali.

Pia kuna barabara maarufu jijini Jeddah iliyokatiza ufukweni mwa bahari . Napendekeza upite katika barabara hiyo mapema alfajiri au jioni saa 12 ili uweze kujionea maumbile ya kupendeza baharini, pia kuna chemchem ya baharini, moja ya chemchem zilizoko juu zaidi kuliko nyingine yoyote duniani. Kuna machaguo mbalimbali ya vyakula katika barabara ya kupendeza ufukweni mwa bahari, kuanzia migahawa ya ya anasa mpaka maduka ya vyakula vya haraka au hata vijiduka vidogo vya biskuti na chipsi. Wenyeji hukuketi katika ufukweni kwa masaa na watoto wao wakicheza karibu yao huku wakiwaangalia wapita njia.

Kwa ushauri zaidi wa Hala kuhusiana na unachotaka kukiona jijini Jeddah, angalia hapa.

Wakati huo huo bloga American Bedu, ambaye ni Mmarekani anayeishi Saudi Arabia, anatueleza kile anachokifikiri kuhusiana na hoteli za kina mama pekee jijini Riyadh.

Hoteli ya Al Luthan na bafu lake ni hoteli ya kwanza kabisa ya wanawake pekee ya aina yake jijini Riyadh. Ni hoteli ya kifahari na ina bafu la chemchem maalumu kwa wanawake pekee. Ni hoteli ya huduma zote yenye kutoa huduma za uhakika na yenye kutoa malazi salama. Al Luthan inapokea wageni wa kike kutoka Saudia na wasio Wasudia. Hivi sasa baadhi ya wanawake wamezungumza na vyombo vya abari wakisema kuwa kuzinduliwa Al Luthan ni mojawapo ya upigani hatua nyuma. Kwa mujibu wa wanawake hawa, wanaona kama ni kupiga hatua kuelekea nyuma kwa ufalme wa taifa hilo kutokana na ukweli kwamba tayari kuna ubaguzi na siyo tu kwamba wanawake wana haki kidogo lakini kwa kushabikia na kuafiki uanzishwaji wa hoteli ya wanawake peke yao yenye eneo la kuogea inarudisha nyuma harakati za kina mama kudai haki. Pengine nimo kwenye kundi dogo katika jamii, lakini nachukua mtazamo mbadala. Al Luthan siyo hoteli ya kipekee ikilinganishwa na hoteli nyingine duniani. Hoteli za wanawake au hoteli zinazotenga safu nzima ya ghorofa kwaa jili ya wanawake zipo karibu katika kila jiji kubwa (na hata kwenye miji isiyo mikubwa) duniani. Siku za nyuma wakati nilipokuwa nikisafiri safari nyingi za kimataifa, nilikuwa nikifurahia kupanga katika hoteli zenye safu maalumu kwa ajili ya wanawake pekee. Haswa katika majiji ya kigeni ambayo hayakuzoea kuwa na wafanyabiashara wanawake wanaosafiri peke yao. Kwa hiyo mimi sioni kama kuanzishwa kwa hoteli hii maalumu kwa wanawake kuwa ni hatua ya kurudi nyuma asilani bali chaguo jema kwa wanawake kuwa nalo ndani ya falme.

Bloga kutoka Riyadh, Sweet Anger amechoshwa na wageni wanaodhani kuwa wanawake wa Kisaudia wanakandamizwa, wakati hawajui lolote kuhusu maisha yao au jamii:

Basi, nilikuwa nikitafiti mtandaoni kitu kimoja au kingine nikakutana na ujumbe kuhusu ripota aliyekuwa Saudia ambaye ni mwanamke na hivyo hakuruhusiwa kukaa kwenye sehemu ya wanaume ndani ya mgahawa wa Starbucks.umm boo hoo hoo. Kitu kilichonishika zaidi siyo ile makala yenyewe, lakini maoni. […] Nataka ieleweke kwamba Saudi siyo mahema machache yanayounganishwa na ngamia wanaorandaranda, na wanaume wenye vilemba waimbao “Allah o akbar” huku wakiwabaka wanawake kwa sababu ni haki yao na wanamiliki nyumba ya harimu yenye vigoli si chini ya 20. Oh, na pia hatutahiri wanawake wetu, hilo ni jambo la hovyo na ni kosa katika ngazi nyingi. Wanawake hawafungiwi nyumbani na yeyote yule ambaye kwamba hilo ni jambo la utamaduni wa familia na siyo nchi, upo? Vyema. Hatuko nyuma nyie mafidhuli, sisi ni wahafidhina, yaani, kama unapotaka kwenda kujichanganya na mtu wa jinsia tofauti kuna maeneo maalumu. […] Sasa hoja yangu ya msingi hapa ni kwamba hivi tangu lini mmeanza kuhukumu watu: “Fungeni Starbucks!! Zisiwe na sehemu zinazokaribisha familia” – umm, hapana samahani? Silalamiki na ninahitaji kahawa yangu, tuache utani, POTEENI MBALI, sikukodi mtu yeyote awe msemaji wangu.

Kwa wale ambao bado mnashawishika kwamba sisi ni taifa kandamizi na kwamba sisi wanawake masikini tunahitaji kufunzwa namna ya kupambana na kama sivyo vyema vyema endeleeni kutupigania, ngojeni niwape maelezo mafupi namna siku ya kawaida inavyokuwa jijini Riyadh. Jana niliamka nikatengeneza kahawa yangu… nikatinga vazi langu la abaya (kama unaona hili linatisha kufikirika, lifikirie kama jaketi), nikamchukua malaika wangu mdogo, nikaingia ndani ya gari yangu iendeshwayo na dereva ndani yake, nikamshusha binti yangu, halafu nikaenda kazini. Mida ya saa 7:30 napata chakula cha mchana na marafiki zangu wa kike kutoka mgahawa wa Subway, halafu nikarejea kazini na kutoka saa 10:30 jioni, narejea nyumbani, napumzika, naoga natinga mavazi yangu, namsubiri dereva anipeleke mgahawa wa Wachina kwani nilikuwa nimewakaribisha marafiki zangu wa kike. Nafika pale mida ya saa 3:45 hivi halafu naondoka kama saa 6, nafika nyumbani, naingia mtandaoni, naangalia facebook na hotmail, halafu naingia kitandani saa 8. MUNGU WANGU, JINAMIZI GANI HILI, NINAWEZAJE KUISHI MAISHA YA KIKANDAMIZWA NAMNA HII, AAAAHHHHHH!!!! […] Hoja yangu ni kwamba baadhi ya watu hawana welewa kuhusu nini kinaendelea ndani ya maisha yetu na bado wanafikiri wana haki ya kuamua na kuwa wakuu. Tuko tofauti, naam, na kwa kuwa tuko tofauti na vile ambavyo unafikiri ni sawa haitufanyi sisi kuwa wabaya au wenye makosa inatufanya sisi kuwa sisi. Kabiliana na ukweli huo au jitoe.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.