Zaidi ya wakazi 20,000 wa eneo la Macau nchini China waliandamana siku ya Jumapili, Mei 25, 2014, kupinga muswada utakaowalipa fidia maafisa waandamizi baada ya kuondoka madarakani na kumkinga mkuu wa serikali na makosa yoyote ya kijinai wakati au baada ya muhula wake wa uongozi.
Macau, ambalo ni jimbo maalum la kiutawala la China, lina idadi ya watu wanaofikia 500,000. Waandamanaji walikuwa ni asilimia nne ya idadi yote ya watu, na hivyo kuwa maandamano makubwa zaidi tangu koloni hilo la zamani la Ureno halijakabidhiwa kwenye mamlaka ya China mwaka 1999. Hasira ya watu hao iliwashangaza wengi, hasa ikizingatiwa kuwa vyama vya upinzani vinaonekana kuwa bado dhaifu kwenye mji huo na pia kwa vile vyombo vingi vya habari vinaonekana kushambikia serikali kwa kuwa vinapokea ruzuku ya serikali.
Muswada huo, unaotarajiwa kupitishwa siku ya Jumanne, Mei 27, 2014, ulitungwa na Waziri wa Macau wa Utawala na Sheria mwezi mmoja uliopita na ulipendekezwa bila ridhaa ya umma. Muswada huo utamhakikishia mkuu wa serikali kinga ya kushitakiwa kwa makosa ya kijinai akiwa madarakani. Vile vile muswada huo utahakikisha kuwa mkuu wa serikali anayeondoka madarakani, sambamba na maafisa wakuu walio chini yake, wataendelea kupata mishahara yao ya kila mwezi yanayofikia asilimia 70 ya mishahara yao ya sasa. Waziri huyo anadai kuwa muswada huo una lengo la kuwavutia wafanya biashara kujiunga na siasa.
Uchaguzi wa mkuu wa serikali utafanyika mwishoni mwa mwaka 2014, na baada ya hapo maafisa wakuu wa serikali nao wataondoka madarakani. Wengi wanaamini kuwa muswada huo umesukwa kwa ajili ya kumnufaisha Mkuu wa Serikali Fernando Chui Sai-on na vigogo wa serikali kwa sababu ndio watakaokuwa wanufaika wa maslahi hayo.
Ingawa muswada huo umejaa utata mwingi, bado serikali imekuwa ikishinikiza baraza la kutunga sheria kuupitisha. Wengi wa watunga sheria ama wamechaguliwa na makundi yao au wameteuliwa na mkuu wa serikali.
Kuishinikiza serikali kuutupilia mbali muswada huo, kikundi cha raia wanaoguswa na hali hiyo wanaoitwa “Macau Conscience” [Dhamira ya Macau] waliandaa maandamano kupinga “Muswada wa Ulafi na Upendeleo.”
Chombo huru cha habari cha All About Macau kilimwomba mmoja wa waandamanaji kwenye kundi la Facebook kwa nini alijiunga na maandamano hayo:
市民林小姐認為特首在有可能臨離任的時候通過這個法案,是「打劫澳門市民」,根本是與民為敵;
Mama Lam anaamini kuwa mkuu wa Serikali atakayefurahia maslahi hayo manono atakuwa “anawaibia raia wa Macau” na atakuwa anajigeuza kuwa adui wa watu.
Watu wengi walionyesha hasira yao kupitia mabango wakati wakiandamana.
Baada ya mkutano, baadhi ya watunga sheria na madiwani wanaounga mkono serikali waliviambia vyombo vya habri kuwa watashauri utawala wa Baraza la Wawakilishi kuunda kamati ya kuupitia upya muswada huo. Kwa wakati huo huo, waandaaji wa maandamano hayo ya “Macau Conscience” walisema wataendelea kuchukua hatua zaidi kama muswada huo utapitishwa na baraza la kutunga sheria siku ya Jumanne.
1 maoni