Ujerumani yakiri kuhusika na mauaji ya kimbari nchini Namibia enzi za ukoloni, lakini wahanga wasema haitoshi

Kampeni ya kupinga mauaji ya jamii ya Herero na Nama nchini Namibia yaliyofanyika Ujerumani. Picha na Uwe Hiksch, Machi 22, 2012, (CC BY-NC-SA 2.0)

Baada ya zaidi ya karne ya ukimya wa serikali, Ujerumani hatimaye imetoa tamko la kukubali kuhusika na mauaji ya halaiki ya raia wa Namibia kati ya 1904 na 1908 wakati ambao Ujerumani wakati huo ikiitawala Namibia ilifanya mauaji ya kutisha ya maelfu ya watu kutoka jamii ya Herero (wanaofamika pia kama Ovaherero) na Nama.

Ujerumani ilitangaza kutoa Euro bilioni 1.1 (takribani bilioni 1.3 za dola za Kimarekani) baada ya miaka mitano ya majadiliano baina ya serikali ya Ujerumani na Namibia. Malipo hayo yatafanyika kwa kufadhili miradi mbalimbali nchini Namibia kwa kipindi cha miaka thelathini. Hata hivyo, serikali ya Ujerumani inasisitiza kwamba malipo hayo sio fidia, kwa sababu hakuna madai ya kisheria yalishafanyika kuhusu suala hilo, bali sehemu ya hatua zake za kuwajibika kimaadili.  

Serikali ya Namibia imekubaliana na kauli hiyo ya serikali ya Ujerumani. Hata hivyo, kizazi cha wahanga wa mauaji hayo, ambao hawakuhusika kwenye mazungumzo hayo, kinapiga vikali masharti ya makubaliano hayo wanayosema yatafanywa kupitia ufadhili wa miradi ya maendeleo na si moja kwa moja kuwafikia wahanga hao.

Tunachokifanya hivi sasa ni “kutambua mateso yasiyopimika yaliyofanywa kwa wahanga. Lengo letu ni kupata njia ya pamoja ya kuelekea kwenye mazungumzo ya kuaminiana kwa kukumbuka wahanga hao,” waziri wa masuala ya kigeni wa Ujerumani Heiko Maas alisema kwenye  tamko lake kwa vyombo vya habari lililotolewa mnamo Mei 28, 2021. “Hatua hii ni pamoja na kuyatambua matukuo ya kipindi cha ukoloni wa Wajerumani kwa nchi ambayo sasa ni Namibia na kipekee zaidi ukatili uliofanyika katika kipindi cha kuanzia mwaka 1904 na 1908 tena bila kuwahurumia au kufanya chochote cha kuwasaidia. Sasa tutayaita matukio haya kama yalivyokuwa kipindi hicho: Mauaji ya kimbari,” alisema Maas. 

Tunalo neno moja tu leo kwa kile wakoloni wa Ujerumani walifanya Namibia kati ya mwaka 1904 na 1908: mauaji ya kimbari. Ninachoamini ni kwamba leo tunaweza kuchukua hatua muhimu kuelekea maridhiano. Tutaiomba msamaha Namibia na kizazi cha wahanga. Kama alama ya nia njema, tutatoa bilioni 1.1 kwa kipindi cha miaka 30, kwa ajili ya, mfano, kilimo na elimu. Hatuwezi kuyabadili yaliyopita, lakini pamoja tunaweza kutazama tuendako. 

Mnamo Juni 4, 2021, wakati akizungumza na vyombo habari katika Ikulu ya Namibia iliyopo Windhoek, makao makuu ya nchi hiyo, Makamu wa Rais  Nangolo Mbumba alisema majadiliano na Ujerumani yamekuwa magumu sana. “Hatufurahii kabisa hali ilivyokuwa (…) sehemu ngumu zaidi ilikuwa malipo ya fidia hiyo. Ujerumani imekubali kuwajibika kimaadili kulipa fedha hizo” lakini “imekataa kuiita fedha hiyo fidia,” alisema Mbumba kwa mujibu wa taarifa kutoka gazeti la kila siku, The Namibian. 

Mauaji ya 1904 – 1908

Genozid-Denkmal vor der Alten Feste [Eneo la Makumbusho ya Mauaji ya Kimbari” mbele ya ngome ya zamani jijini  Windhoek] Pemba.mpimaji via Wikimedia Commons (CC BY-SA 4.0). 

Kati ya 1884 na 1915, Namibia lilikuwa koloni la Ujerumani likiitwa Ujerumani Afrika ya Kusini Magharibi. Wanahistoria wanakubaliana kwamba kati ya 1904 na 1908, walowezi wa Ujerumani waliua watu wasiopungua 65,000 kati ya watu 80,000 wa kabila Ovaherero na Wanama wasiopungua 10,000 kati ya 20,000. 

Mauaji hayo yalichochewa na vuguvugu la kuwapinga Wajerumani lililofanywa na watu wa kabila la Herero waliokuwa wakitumikishwa kwenye mashamba na shughuli za kiuchumi za Wajerumani. Matokeo yake, kamanda wa majeshi ya kikoloni ya Ujerumani Luteni Jenerali  Lothar von Trotha aliwaamuru askari wa Kijerumani 15,000 kuzima vuguvugu hilo. 

Waherero walikimbilia kwenye jangwa la Omaheke, eneo lenye maji kidogo sana, mashariki mwa Namibia lakini Von Trotha aliagiza jangwa hilo lifugwe na hivyo kuwafukuzia mbali, waende sehemu isiyo na maji kabisa. Hatua hiyo ilifanya maelfu ya Waherero kufa kwa kukosa maji. Kama vile haitoshi, Von Trotha alitoa amri ya kuwatenga watu hao: “Waherero sio sehemu ya Ujerumani tena. (…) ndani ya mipaka ya Ujerumani, kila Mherero awe na silaha au la, awe na ng'ombe au la, atapigwa risasi; sitachukua wanawake wala watoto, wafukuzeni waende kwa watu wao au wapigeni risasi na wao.”

Watu wa kabila la Namas nao waliwaunga mkono wenzao wa Herero. Hata hivyo, walikwepa kupigana moja kwa moja na majeshi ya Ujerumani. Badala yake, walianzisha vita vya msituni. Baada ya viongozi wao Hendrik Witbooi na Jakob Morenga kufa, walikata tamaa.

Mwishoni mwa maasi hayo, majeshi ya Ujerumani yalipokuwa yameshinda, “waasi, yaani watu wa kabila la Herero walikuwa kama wamefutika. Kutoka idadi ya awali ya Waherero 80,000 walibaki hai 20,000 pekee,” kwa mujibu wa wasomu wa masuala ya mauaji ya kimbari Samuel Totten and William S. Parsons.

Upinzani dhidi ya mkataba wa fidia 

Vyama vya upinzani na jamii zilizoathiriwa wamepiga vikali mkataba huo, ulioshirikisha kwa uchache sana kizazi cha wahanga wa mauaji hayo.

Kwa macho ya Wanama na Waovaherero, mkataba huu unaashiria kukosekana kwa utashi wa maridhiano ya kweli na serikali ya Ujerumani.

‘SI HAKI HATA KIDOGO’ …uongozi wa Waovaherero na Wanama, pamoja na mambo mengine, wanapinga kile walichokiita makubaliano yasiyo haki kati ya serikali ya Namibia na Ujerumani. Video: Puyeipawa Nakashole pic.twitter.com/5RQhdcqPBK

Kwa mujibu wa gazeti la The Namibian, machifu wa kimila kutoka nyumba za kiutawala za Maharero, Kambazembi, Gam, Zeraeua na Mireti kwenye kabila la Ovaherero wamekataa pesa hizo zinazotolewa na Wajerumani. Wanataka euro bilioni 478  (takribani trilioni 8 za dola za Namibia) kama fidia ya fedha kwa mauaji hayo ya mwaka 1904 hadi 1908, wakitaka zilipwe kwa zaidi ya miaka 40 kama pesheni kwa wajukuu wa wahanga hao. 

Hivyo hivyo, mnamo Juni 1, 2021, mwenyekiti wa Umoja wa Mauaji ya Namibia, Laidlaw Peringanda alisema katika mahojiano na Al Jazeera: “Kama serikali ya Ujerumani inataka maridhiano, wanahitaji kuturejeshea utu wetu kwanza. Lakini hilo haliwezekani kama wanaendelea kututenga.”

Mtumiaji huyu wa Twita aliyaeleza mazungumzo hayo kama “ujinga wa kijinga” uliosababisha “sherehe za aibu kabla hata ya muda wake kuelekea ‘maridhiano’”:

Mambo mawili muhimu kwenye suala hili:

  1. Rais wa zamani Khama anawatambua Waovaherero wanaoishi nje ya nchi (hatimaye!) yaani Wanaherero wa Bostswana waliokimbia nchi yao wakati wa mauaji hayo
  2. Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Maas anaahirisha ziara yake kwenda Namibia “kwa muda usiojulikana”

Baadhi ya Wanamibia wanakosoa ahadi hiyo ya fedha, wanayosema itakuwa na matokeo hafifu. 

Howard Rechavia-Taylor, mtaalam wa ukoloni wa Kijerumani kwenye Chuo Kikuu cha Columbia alisema kwamba athari za ukoloni wa Ujerumani bado zinaonekana mpaka leo, kwa kutolea mfano ugawaji ardhi usio wa haki: 

Ukweli mchungu: wazungu bado wanaishi kwenye maeneo makubwa ya ardhi ya Herero na Nama – mara nyingine hukaa kwenye makaburi ya mababu ambao watu wa Herero na Nama mpaka leo wanahitaji idhini kuyaona. “Maridhiano” bila kushughulikia suala la ardhi ni sawa na propaganda za kujisafisha tu.

Lakini ukosoaji huo haufanyiki Namibia pekee. Sauti mbalimbali zinasikika hata Ujerumani kwenyewe. 

“Ujerumani ilifanya mazungumzo na serikali ya Namibia, lakini haikujihangaisha kukutana na wawakilishi halali wa watu wa Herero na Nama,” alisema mwanaharakati wa haki za Waherero anayeishi Berlin Israel Kaunatjike kwenye mahojiano yake na Redaktionsnetzwerk Deutschland. “Kile kilichoamuliwa sasa hivi ni mradi mdogo wa misaada ya kimaendeleo, ambao hakuna uhusiano wowote na fidia,” alisema Kaunatjike. 

Umoja wa vyama vya watu weusi nchini Ujerumani, hali kadhalika, uliandaa maandamano jijini Berlin kuunga mkono matamako ya watu wa Herero na Nama. 

Tunatoa wito wa kushiriki kwenye maandamano ya kile kinachoitwa Mkataba wa makubaliano kati ya Namibia na Ujerumani – ambao haukuhusisha makundi yanayowatetea jamii ya Herero na Nama. Tangu mwaka 2016 ukweli ulikuwa: Haiwezi kuwa kwa ajili yetu bila kutushirikisha. Chochote kinachotuhusu bila kutushirikisha kiko kinyume na sisi!”

Hata hivyo, si kila mtu yuko kinyume na makubaliano hayo. Mnamo June 3, mwenyekiti wa Baraza la Ovaherero/OvaMbanderu, Gerson Katjirua, alitangaza kwamba baraza zima linakubaliana na makubaliano hayo na litakuwa moja wapo wa watia saini wa makubaliano hayo:

Tunaunga mkono makubaliano haya …Mwenyekiti wa Baraza la Ovaherero/OvaMbanderu na Nama Gerson Katjirua mnamo asubuhi ya Alhamisi jijini Windloek alisema baraza lote linapokea kitita hicho cha Euro bilioni 1.1 kutoka serikali ya Ujerumani. Video: Shelleyaan Pertersen wa jarida la @TheNamibian

Katjirua alisema kwamba wajukuu wa wahanga wanapinga fidia. “Tutakuwa watia saini kwa makubaliano haya,” alisema.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.