Maelfu ya wageni wanaozuru Mji Mkongwe, Zanzibar, mji wa kale uliofahamika kubeba historia kubwa ya visiwa hivyo, hufuatilia sauti ya muziki unaorindima kutoka DCMA, shule ya muziki inayolenga kutangaza na kutunza muziki wa mwambao unaofahamika kuwa na asili yake visiwani humo na maeneo mengine ya pwani ya Bahari ya Hindi. Tangu mwaka 2002, shule hiyo imekuwa ikiutangaza na kuutunza utamaduni huo wa kipekee wa Zanzibar unaochanganya tamaduni za ki-Arab, ki-Hindi na ki-Afrika kupitia muziki.
Miaka 17 tangu kuanzishwa kwa shule hiyo, sasa ni wazi inakabiliwa na hali mbaya ya kifedha inayotishia kufungwa kwake. Karibu asilimia 70 ya wanafunzi 80 wanaosoma shuleni hapo hawana uwezo wa kulipa ada ya masomo, ambayo ni kiasi cha dola za Marekani 13 kwa mwezi, kwa mujibu wa taarifa rasmi ya DCMA kwa umma. Ingawa shule hiyo imekuwa ikipokea misaada kutoka kwa wafadhili wa kimataifa na mashirika ya kirafiki, kwa sasa inakabiliana na ombwe kubwa linaloweza kulazimisha kufunga virago vyake na kuondoka kwenye Jumba hilo la kihistoria mjini Zanzibar, linalofahamika kama Old Customs House.
Bila kupata fedha za haraka kuwezesha shughuli zake kuendelea, wanafunzi na walimu wa DCMA wana wasiwasi kwamba sauti zilizozoeleka kurindima kutoka kwenye viunga vya jengo hilo na kufanya visiwa vipate burudani ya sanaa — zinaweza kukoma. Shule hiyo si tu hufundisha na kutangaza utamaduni na urithi wa asili kupitia muziki, lakini pia hukaliwa na kundi kubwa la wanamuziki vijana wanaotafuta njia mbadala za kuendesha maisha yao kwa kutumia sanaa.
“Tumeanza kukabiliana na hali mbaya ya kifedha,” anasema Alessia Lombardo, Mkurugenzi Mtendaji wa DCMA, kwenye video rasmi ya DCMA. “Kuanzia sasa mpaka miezi sita ijayo, hatuna uhakika kwamba tunaweza kuwa na uwezo wa kuwalipa mishahara walimu na wafanyakazi wengine.”
Hivi sasa, walimu 19 wabobezi na wafanyakazi wengine wachache hawajalipwa mishahara yao kwa zaidi ya miezi sita kwa sababu shule hiyo imekuwa ikihangaika kupata misaada kutoka kwa marafiki wakati huo huo ikijaribu kutengeneza mfumo endelevu wa kupata mapato kwa minajili ya uendashaji wa shule hiyo. Ingawa visiwa hivyo vinafahamika kuvutia watalii wengi shauri ya kuwa na fukwe na hoteli kubwa za kifahari, wenyeji wengi wanateseka na ukosefu mkubwa wa kazi ingawa takwimu zilizotolewa na Benki ya Dunia zinaonesha kuwa umasikini umepungua kidogo visiwani humo.
Kwa zaidi ya miaka 17, DCMA imefanya kazi bila kuchoka kutangaza na kulinda urithi mkubwa wa Zanzibar kupitia muziki. Ikiwa ni mahali alipozaliwa gwiji wa muziki wa taarab na waimbaji maarufu Siti Binti Saad na Fatuma Binti Baraka, au Bi. Kidude, Zanzibar ni makazi ya mahadhi ya muziki ulioibuka kupitia mchanganyiko wa kiutamaduni na ushirikiano baina ya wa-Swahili wa Pwani kwa mamia ya miaka iliyopita. Leo, wanafunzi wanaweza kujifunza muziki wa asili kama taarab, ngoma na kidumbak, sambamba na vyombo vingine kama ngoma, qanun na oud, kama walinzi — na watafsiri — wa utamaduni na desturi.
Neema Surri, mpigaji wa chombo kiitwacho violin shuleni hapo DCMA, amekuwa akijifunza namna ya kucheza chombo hicho tangu akiwa na umri wa miaka 9. “Ninawajua vijana wengi wanaotamani kujifunza muziki lakini hawawezi kumudu ada ndogo shauri ya umasikini na ukosefu wa kazi,” Surri alisema kwenye video ya DCMA.
Baada ya kumaliza warsha za DCMA, kozi za Astashahada na Stashahada, wanafunzi wengi wa DCMA huenda kufanya kazi kwenye majukwaa ya kimataifa wakiwa kama bendi zenye sifa ya kushinda tuzo na wasanii wa kujitegemea. Mzanzibar Amina Omar Juma, mwanafunzi wa zamani wa DCMA na mwalimu wa sasa wa DCMA, hivi karibuni alirudi kutoka kwenye ziara nchini Afrika Kusini akiambatana na bendi yake iliyojipatia sifa “Siti na Bendi Yake,” inayofahamika kwa “kuunganisha mizizi” kwa kuchanganya sauti za taarabu ya asili na sauti za mahadhi ya kisasa. Pia, kwa ushirikiano na wanabendi wenzake, ambao nao ni wanafunzi wa zamani wa DCMA, alitoa alibamu ya kwanza iitwayo, “Fusing the Roots,” mwaka 2018, akiendelea kufanya maonesho kwenye Sauti za Busara, tamasha kubwa zaidi la muziki kwenye ukanda wa Afrika Mashariki, mwaka huo huo.
Hapa unaweza kuusikiliza wimbo wa Bendi hiyo uitwao “Nielewe” pamoja na video yake, ikionesha madhari ya Zanzibar kuelezea simulizi ya mwanamke anayekabiliana na unyanyasaji wa nyumbani na ndoto za maisha ya muziki, kama ilivyo hadithi ya maisha binafsi ya Omar Juma:
Soma zaidi: Wanawake wa Afrika Mashariki kwenye Tasnia ya Muziki Waimba Kupinga Kutawaliwa na Wanaume
Historia ya mwingiliano wa kiutamaduni na ushirikiano
Zaidi ya wageni 15,000 wamewahi kupitia kwenye jengo la shule hiyo kufurahia maonesho mubashara, warsha na madarasa pamoja na kukutana na wanamuziki wa DCMA wanaowakilishia mustakabali wa utamaduni na urithi wa Zanzibar, kwa mujibu wa DCMA. Ikiwa na vionjo vya historia ya India, Urabuni na Afrika, shule hiyo inafurahia kuwa matokeo ya tamaduni za nchi mbalimbali, ikiwa na utamaduni uliunganishwa kwenye eneo lal Bahari ya Hindi na Ghuba ya Uajemi.
Sultani wa Omani, “mfalme maarufu wa kati ya karne ya 17 na 19,” alihamia utawala wake kutoka Muscat kwenda Zanzibar mwaka 1840. Kutoka Mji Mkongwe, watawala wa Omani waliendesha biashara ya baharini, ikiwa ni pamoja na karafuu, dhahabu, nguo, wakitegemea safari za vyombo vilivyoongozwa na upepo kati ya kingo ya Bahari ya Hindi nchini India kwenda Oman na Afrika Mashariki.
Vijana wa Zanzibar wanatambua umuhimu wa kuelewa historia yao ili kubaini ikiwa mustakabali wao na muziki wanaoutengeneza leo unaelezea matamanio ya kuweka daraja kati ya mambo ya kale na haya ya kisasa. Hivi karibuni wanafunzi wa DCMA na walimu wao walianzisha “TaraJazz,” mwuunganiko wa taarab ya asili na jazi ya kisasa. Mwanamuziki wake, Felician Mussa, 20, amekuwa akijifunza kupiga chombo cha muziki kinachoitwa violin kwa miaka mitatu na nusu; TaraJazz ni moja wapo ya bendi zinazotafutwa zaidi visiwani humo, hapa ikiwa imenaswa na mpiga picha Aline Coquelle:
Pwani ya wa-Swahili inaeleza simulizi ya mchanganyiko wa utamaduni na DCMA inaendeleza utamaduni huu kupitia ushirikiano wa kimuziki. Kila mwaka, shule hiyo huandaa mradi unaoitwa “Swahili Encounters,” [Mkutano wa ki-Swahili] unaowakutanisha wanamuziki wanaofahamika kutoka Afrika, Mashariki ya Kati, Ulaya na Amerika ya Kaskazini na wanafunzi wa DCMA kwa minajili ya kutengeneza tungo halisi za muziki ndani ya kipindi cha juma moja. Mwishoni mwa ‘mkutano’, timu mpya za wasanii waliokutanishwa hutakiwa kufanya onesho kwenye Sauti za Busara, na mara nyingi timu hizi huishi kuwa na urafiki unaodumu unaovuka mipaka ya lugha na utamaduni, na hivyo kuthibitisha kuwa muziki ni lugha ya dunia.
Shule ya DCMA inatambua kuwa muziki unawainua na kuwaunganisha watu bila kujali tamaduni zao – na pia inaajiri vijana wenye vipaji wnaaoishi kwenye jamii isiyo na uchumi mzuri na upungufu mkubwa wa fursa za ajira. Kwa idadi ya wanafunzi 1,800 waliopita kwenye mafunzo ya DCMA, shule hii ndiyo makazi pekee ya kimuziki wanayoyafahamu, ambapo wanaweza kujifunza na kukua kama wanamuziki na wasanii mahiri.
Mtalii mmoja kutoka Uhisipania, aliyetembelea shule ya DCMA hivi karibuni, aliandika kwenye mtandao wa TripAdvisor: “Binafsi, kukutana na wanamuziki ule ulikuwa wakati wangu mzuri zaidi nikiwa visiwani pale.”
Wakati sekta ya utalii Zanzibar ikiendelea kukua kwa kasi, shule ya DCMA inaamini kuwa muziki una nafasi muhimu katika kusherehekea, kutunza na kutangaza utamaduni wa wa-Swahili, urithi wao na historia yao. Zanzibar ni zaidi ya fukwe na hoteli zake za kifahari — ni sehemu inayojaa vipaji vinavyochipukia kwenye historia kubwa ya mkusanyiko na miunganiko wa historia.
Nyongeza ya Mhariri: Mwandishi wa makala haya aliwahi kujitolea kwenye shule ya DCMA.