Mfanyabiashara Marián Kočner ameshtakiwa kwa kuamuru mauaji ya mwanahabari Ján Kuciak na mchumba wake Martina Kušnírová mwaka 2018, kulingana na tamko la Machi 15 la Ofisi Maalum ya Mashtaka ya Slovakia.
Kabla ya kuuawa Kuciak alikuwa akifanya kazi na Mradi wa Kupambana na Uhalifu na Kuripoti Rushwa na chombo chake, Aktuality.sk, kupeleleza uhusiano baina ya kikundi cha uhalifu cha Waitalia na uwepo wake nchini Slovakia. Pia alikuwa akiandika kuhusu masuala ya biashara za Kočner.
Wauaji walisababisha hofu kusambaa nchini. Watu waliokuwa wakitaka haki itendeke waliongoza maandamano makubwa yaliyolazimisha kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Robert Fico.
Kuciak ndiye alikuwa mlengwa wakati Kušnírová aliuawa kwa sababu alikutwa nyumbani wauaji walipoingia. Wote walikuwa na umri wa miaka 27 na walikuwa wamepanga kuoana Mei 2018.
Kulingana na mashtaka, Kočner mwenyewe alishamtishia Kuciak kwa njia ya simu Septemba 2017 na kisha aliamuru mauaji yaliyofanyika Februari 21, 2018 katika kijiji cha Veľká Mača.
Mamlaka za sheria za Slovakia ziliwatia nguvuni watu wanne kwa kumuua Kuciak na Kušnírová. Msaidizi wa Kočner, Alena Zsuzsová alituhumiwa kwa kulipa yuro 50,000 (karibu dola $57,000 za Marekani) na kusamehe zaidi ya yuro 20,000 (karibu dola $22,700) alizokuwa akiwadai watu watatu ambao ni mmiliki wa mgahawa wa pizza, askari polisi wa zamani na mwanajeshi wa zamani ili waweze kupanga na kutekeleza mauaji.
Wakati wa majira ya joto, Kočner alikamatwa kwa makosa ya kifedha na alichunguzwa na Kuciak, lakini ilizichukua mamlaka miezi sita zaidi kuwakamata wahusika wadogo wa mwekezaji huyo mtata na kumuunganisha moja kwa moja na mpango wa mauaji.
“Sababu za mauaji ni kazi za uhandishi wa habari za mlengwa,” mwendesha mashtaka maalum, ambaye hakutajwa jina kwa sababu za kiusalama, aliwaambia wanahabari hapo Machi 15, katika mkutano wa habari karibu na Bratislava.
Mashtaka yalipokelewa na Taasisi za Haki za Vyombo vya Habari na Mawakili wa Haki za Binadamu Huko twita, Mwanakamati ya Kulinda wanahabari’ Gulnoza Said alisema:
Tunapokea habari kuwa mamlaka za Slovakia zimemshtaki mtuhumiwa aliyechora mpango wa kumuua mwanahabari za uchunguzi
#JánKuciak. Hii ni hatua muhimu na ya kipekee katika mauaji ya wanahabari. Tunaamini mamlaka zitatimiza ahadi yake ya kuwaleta wahusika wote mbele ya sheria, hivyo basi kuwafanya wanahabari wote kuwa salama dhidi ya uhalifu nchini Slovakia.
Harlem Desir kutoka Taasisi ya Ulinzi na Ushirikiano ndani ya Ulaya aliandika:
Ninapongeza mashtaka ya leo dhidi ya mchochezi wa mauaji ya mwanahabari #JanKuciak huko #Slovakia. Alilipa gharama ambayo hakustahili kwa sababu ya kuchunguza rushwa kwa viwango vya juu kabisa, amekuwa alama ya uhuru wa vyombo vya habari kupambana na uhalifu wa mafioso. Taarifa nzima: https://t.co/BB8bsemt6K
— OSCE Uhuru wa vyombo vya habari (@OSCE_RFoM) March 14, 2019
Mei 2018, baada ya kifo chake Kuciak alipewa tuzo ya Mwanahabari, Mfichuaji Maovu na Mlinda Haki ya Kuhabarishwa, na Umoja wa Ulaya Magharibi/Nordic Green Left (GUE/NGL) ndani ya Bunge la Umoja wa Ulaya. Ikiitwa kwa jina la mwanahabari wa Maltese aliyeuawa Daphne Caruana Galizia, tuzo hiyo imekusudiwa kuzitambua kazi na ushupavu wa watu katika kufichua uhalifu na rushwa kwa nguvu.
Kuendeleza Urithi wa Ján Kuciak
Baada ya Kuciak kuuawa, OCCRP na vituo vyake wanachama walimalizia na kuchapisha baadhi ya tafiti zake zilizokuwa hazijakamilika.
Februari 2019, walitoa ripoti iliyokuwa na kichwa cha habari “Maisha Yasiyokamili, Haki Isiyokamili. ” Hii ilikamilishwa na OCCRP, Mradi wa Ripoti za Uchunguzi Italia, Investigace.cz na Kituo cha Uchunguzi cha Ján Kuciak (ICJK) ikihusika na ripoti za Kuciak, akiripoti kuhusu mipango ya uhalifu nchini Slovakia na uhusiano katika siasa na vyombo vya kusimamia sheria.
Lakini ICJK iliweka wazi kupitia twita jinsi baadhi ya mamlaka hazitoi ushirikiano na pia walizuiwa kushiriki katika mkutano wa waandishi wa habari ambapo mashtaka dhidi ya Kočner yalitangazwa.
Leo saa saba mchana, mkutano wa waandishi wa habari kuhusu upelelezi juu ya kifo cha Martina na Jan utafanyika katika ofisi za Mwendesha mashtaka maalum. Hatutakuwa pale. Kulingana na mashtaka, sisi sio wanahabari ni raia wadadisi tu ambao tunaweza kusoma tu gazetini. #justice4jan
— Kituo cha upeleleze cha Jan Kuciak (@icjkuciaka) March 14, 2019
Pamoja na ukweli kwamba mamlaka sasa zimewashtaki wahusika wa mpango wa mauaji, wanahabari na mawakili wa habari wanasisitiza kuwa bado haujapatikana ufumbuzi wa maswali kuhusiana na kesi kama vile tetesi za kuhusika kwa mwanasiasa mkubwa. Hasa hasa mawakili wanania ya kufahamu waziri mkuu wa zamani Fico na Robert Krajmer, Mkuu wa idara ya kupambana na rushwa na kitengo cha uhalifu nchini Slovakia wanajua nini kuhusu mauaji.
Marafiki na familia za Kuciak na Kušnírová tayari zimeshazitaka mamlaka kuchunguza uhusiano uliopo baina ya mshtakiwa mpya Kočner na maafisa wenye mamlaka ambao walikuwa wakimlinda kwa miongo miwili iliyopita. Mwanasheria wa familia ya Kušnírová anahofia kuwa urafiki wa karibu baina ya Kočner na mwendesha mashtaka mkuu wa zamani wa Slovakia, Dobroslav Trnka, unaweza kuathiri mwenendo wa kesi.