‘Jeshi halijamuua Yeyote,’ Asema Bolsonaro Baada ya Wanajeshi Kupiga Risasi 80 Kwenye Gari la Familia huko Brazil Na Kuua Mtu Mmoja

    Maafisa wa jeshi wakiwa katika ulinzi huko Rio de Janeiro, mwaka 2018. Picha: Kwa heshima imeruhusiwa kuchapishwa tena na Tânia Rêgo/Agência Brasil.

Jumapili April 7, mwanamuziki Evaldo dos Santos Rosa, 51, alikuwa njiani kuelekea kwenye sherehe huko Guadalupe, mji mdogo na maskini pembezoni mwa jiji la Rio de Janeiro. Katika gari yake alikuwa na mkewe, baba mkwe wake, mtoto wao wa miaka 7 na rafiki yao. Jua lilikuwa limechomoza na ilionekana kuwa mwisho wa juma wa kawaida katika mji huo mkubwa wa mwambao wa Brazili.

Walipokuwa wanaendesha kupita eneo la karibu na  kambi ya jeshi , wanajeshi waliachilia mvua ya risasi kulielekea gari hilo. Evaldo aliuwawa papo hapo wakati baba mkwe wake na mpita njia mmoja walijeruhiwa katika tukio hilo. Abiria wengine walisalimika.

Jeshi la polisi, ambao ndio waliokagua eneo la tukio baadaye, walitabanaisha kwamba gari hilo lilipigwa risasi 80. Mkuu wa Jeshi la polisi Leonardo Salgado, alisema kuwa anaamini kuwa wanajeshi hao walikosea kwa kulifananisha gari la Evaldo na gari lingine la waalifu walilokuwa wanalifuatilia, na hii ni kutokana na tovuti ya habari ya G1. Aliongeza kuwa polisi hawakukuta silaha yoyote katika gari la Evaldo.

Mke wa Evaldo, Luciana Nogueira mwenye miaka 27 aliyesalimika katika shambulio hilo aliwaambia Estado de S. Paulo kuwa:

Os vizinhos começaram a socorrer (o meu marido), mas eles continuaram atirando. Eu botei a mão na cabeça, pedi socorro, disse pra eles que era meu marido, mas eles não fizeram nada, ficaram de deboche.

Majirani walianza kwa kumsaidia mume wangu lakini askari waliendelea kurusha risasi. Niliweka mikono yangu kichwani, nikiomba msaada, nikiwaambia ni mume wangu lakini hawakufanya chochote, walisimama kwa kiburi.

Wakati mauaji ya kikatili ya mtu asiye na hatia yakifanywa na maafisa wa serikali yakiwashtua wengi, Rais Jair Bolsonaro ameendelea kuwa kimya juu ya jambo hili kwa siku sita.

Hatimaye alipozungumza, katika mkutano na vyombo vya habari Aprili 12, alisema: ” Jeshi halijamuua mtu yeyote, jeshi ni la wananchi na hamuwezi kuwatuhumu wananchi kuua.”

Hapo kabla, maneno pekee yaliyotoka kwa Planalto Palace, nafasi pekee ya utawala, yalikuwa ni kupitia msemaji wa Rais, ambaye alizungumzia mauaji ya Evaldo kama “tukio” tena bila kutoa salamu za rambirambi kwa familia yake.

Jioni ya Aprili 8, gavana wa Rio de Janeiro Wilson Witzel na mshirika wa Bolsonaro, alitangaza kuwa “haikuwa juu yake kuhukumu”

Siku mbili baadaye, katika mahojiano na kituo cha runinga, Waziri wa Sheria na Ulinzi wa Raia Sergio Moro alisema mauaji hayo yalikuwa ya “bahati mbaya” .

Hii ni idadi ya mara walizotajwa baraza la Bolsonaro huko katika mtandao wa Twita kuhusu shambulizi lililolenga gari la familia huko Rio de Janeiro. Ndiyo,  mchoro ni MTUPU kwa sababu hakuna aliyejiweka wazi, hata kwa kusema samahani kwa lililotokea. Gari lilipigwa risasi 80 na wanajeshi .

Upelelezi wa Jeshi

Muda mfupi baada ya taarifa hizi kuanza kusambaa katika vyombo vya habari, jeshi lilitoa waraka unaosema kuwa vijana wake walikuwa wanakutana na “lawama zisizo za haki” kutoka kwa wanaowashambulia. Baadaye, jioni ya Aprili 7, jeshi liliachia taarifa nyingine tofauti kabisa ambapo walisema litafanya uchunguzi.

Ingawa polisi wa kiraia walikagua eneo la tukio, hawataweza kufanya uchunguzi. Jeshi lenyewe litafanya hivyo badala yake na mahakama ya kijeshi itawahukumu wanajeshi hao. Ishukuriwe sheria ya 2017 inayosema kuwa jeshi lenyewe linawajibika kupeleleza mauaji yanayofanywa na watumishi wake wakiwa kwenye majukumu.

Shirika la Haki za binadamu, ambao waliikosoa sheria hiyo wakati wa kupitishwa na Rais Michel Temer, walitoa waraka wao Aprili 9 wakitaka ufanyike uchunguzi yakinifu juu ya mauaji ya Elvado na pia wakitaka sheria hiyo ifutwe.

Aprili 8, jeshi liliwakamata wanajeshi 10 kati ya 12 ambao walikuwa wamepelekwa katika eneo lilipotokea tukio hilo na wameshitakiwa kwa kesi ya mauaji na jaribio la mauaji, kulingana na gazeti la Extra. Jaji alimuachilia huru mmoja wa maafisa hao 10 hapo Aprili 10 baada ya kesi kuanza kusikilizwa.

Siyo mara ya kwanza

Polisi wa Brazili wanafahamika kwa “kupiga risasi kwanza, na kuuliza baadaye” ambapo huu ni msemo ambao umeendelea kuthibitika tena na tena.

Ripoti ya Kimataifa ya shirika la Haki za binadamu iliyotolewa mwaka huu inasema Polisi wa Brazili ni hatari na katili zaidi duniani. Mwaka 2018 pekee asilimia 15.6% ya mauaji yote nchini yalifanywa na maofisa wa vyombo vya kusimamia sheria. Katika jimbo la Rio de Janeiro kwa mwezi Januari 2019, polisi wameshaua watu 160.

Muswada uliopambwa na mfuniko wa” kuzuia uhalifu” ambao serikali ya Bolsonaro umeuwasilisha katika Bunge unaweza kuongeza idadi ya matukio ambayo yamekwisha kutokea. Muswada huo unataka mabadiliko ya baadhi ya maelekezo ambayo huenda yakaondoa au yanalenga kupunguza adhabu kwa polisi na maafisa wa jeshi watakapofanya mauaji ya mtu wakiwa kazini.

Mazingira ya mauaji ya Evaldo, mwanaume mweusi mwenye miaka 51 sio ya kipekee lakini ni ya kawaida sana Brazili kama vile Samira Bueno na Renato Sérgio de Lima, wakurugenzi wa Jukwaa la Ulinzi wa Raia Brazili, walivyosema katika makala ya Folha de São Paulo:

Evaldo teve sua vida ceifada por aqueles que juraram defendê-la. Seu filho jamais se livrará do trauma de ter assistido ao pai ser fuzilado por agentes estatais. Mas que fique claro que a culpa não é apenas daqueles que apertaram o gatilho. Ou começamos a responsabilizar toda a cadeia de comando pelos atos cometidos, ou vamos continuar contando os nossos mortos e desacreditando as nossas instituições.

Evaldo amenyang'anywa maisha yake na wale waliowekwa kuyalinda. Mwanae wa kiume hatatokwa na mshtuko huo wa kumuona baba yake akipigwa risasi na maafisa wa serikali. Lakini tuwekane sawa kwamba makosa sio ya wale tu waliofyatua risasi. Labda tuanze kwa kuuwajibisha mnyororo wote wa mamlaka kwa vitendo vyao au tutaendelea kuhesabu wanaokufa huku tukizilaumu taasisi zetu.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.