Vyombo vya Habari Tanzania Vyapotosha Mgogoro wa Serikali na Kampuni ya Madini

Rais John Magufuli, wa pili kushoto, akiwa na vigogo wa kampuni ya Barrick Gold walipokutana Ikulu mnamo Juni 14. Picha na Ikulu.

Makala haya yalichapishwa awali kwenye Mtega.com, blogu binafsi ya Ben Taylor. Imechapishwa hapa kwa ruhusa.

Mnamo Juni 14, John Magufuli, rais wa Tanzania, alikutana na John Thornton, mwenyekiti wa Barrick Gold—kampuni kubwa zaidi ya uchimbaji wa madini duniani— ambaye alisafiri kwa ndege kutoka Amerika ya Kaskazini kwa lengo mahususi. Taarifa za mkutano wao huo zilitawala vichwa vya habari kwa siku kadhaa zilizofuata.

Kiini cha mkutano huo kilikuwa ni “makinikia” yaliyozalishwa na kampuni tanzu ya Barrick iitwayo Acacia Mining plc kwenye migodi mitatu ya dhahabu nchini Tanzania. Mnamo Machi 5, 2017, idadi kubwa ya makontena yaliyokuwa yamebeba makinikia yalikamatwa kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi, na kufanya taratibu za kuyasafirisha nje ya nchi zilisitishwa. Kamati zilizoteuliwa na rais kufanya uchunguzi ziliituhumu kampuni ya Acacia kwa kufanya udanganyifu mkubwa wa kiasi cha dhahabu na madini mengine yaliyokuwa kwenye makinikia hayo, na hivyo kuinyima Tanzania kiasi kikubwa cha mapato -ambacho inadaiwa kingeweza kuendesha bajeti ya serikali kwa miaka mitatu.

Acacia na Barrick walionesha wasiwasi na kupinga madai hayo yaliyotokana na uchunguzi wa kamati hizo, zikisisitiza kwamba usafirishaji wa makontena hayo kwenda nje ya nchi umekuwa ukifuata taratibu ikiwamo kukaguliwa na kutangaza kiasi kilichomo kwenye makontena hayo kwa usahihi, na kwamba malipo yote ya kodi na murabaha na kadhalika kwenda kwa serikali ya Tanzania yamekuwa yakifanyika. Majuma kadhaa baadae, Acacia wamekuwa wakiomba kufanya mazungumzo na serikali ya Tanzania ili kupata ufumbuzi wa suala hilo. (Posti hii kwenye mtandao wa Bloomberg inatoa maelezo ya kina ya suala hilo).

Baada ya mkutano wa Magufuli na Thornton, ofisi ya rais ilitoa video, iliyokuwa imerekodiwa kwenye eneo la Ikulu, ambapo wazungumzaji wote wawili walielezea upande wap kwa kile kilichokuwa kimetokea kwenye mkutano. Ili kukupunguzia usumbufu wa kulazimika kuitazama video hiyo, muhtasari ni huu hapa: Rais amemshukuru Thornton kwa kufika, na kukubali kulipa kile kinachokubaliwa. Thornton anasema kampuni yake inashukuru kuingia kwenye mazungumzo yenye lengo la kupata ufumbuzi wa mgogoro unaoendelea, na [kampuni yake] iko tayari kulipa kiasi kinachostahili.

Taarifa iliyotolewa baadae na Ikulu ilirudia maelezo kama hayo, ikisema kwamba Barrick imekubali kulipa kile ambacho serikali imesema inawadai.

Mhe. Rais Magufuli amesema pamoja na kukubali kulipa fedha zinazodaiwa Prof. John L. Thornton amekubali kushirikiana na Tanzania kujenga mtambo wa kuchenjulia dhahabu (smelter) hapa nchini.

Kwa mujibu wa taarifa ya Barrick, mkutano huo unaonekana kuhitimishwa kwa makubaliano ya kuwa na majadiliano zaidi, hakuna cha zaidi, hakuna pungufu ya hicho. Hapakuwepo makubaliano yoyote yaliyofikiwa kuhusu kiasi cha fedha -kama kipo- kinachodaiwa na serikali ya Tanzania kwa kampuni ya Acacia/Barrick, na kampuni hiyo haikukiri kuisababishia hasara serikali. Taarifa rasmi ya serikali kuhusu mkutano huo inakubaliana na hitimisho hilo, sawa na tamko la Thornton baada ya mkutano huo na baadae tarifa kwa vyombo vya habari iliyowekwa kwenye tovuti ya Acacia na taarifa mpya ya mwenendo wa soko waliyoitoa asubuhi ya Juni 15.

Siku ya pili baada ya mkutano huo, hata hivyo, magazeti sita ya Kiswahili yaliripoti mkutano huo kwa namna inayompa ushindi mkubwa rais na serikali ya Tanzania, yakienda mbali ya kile kilichosemwa na rais mwenyewe kuhusu mkutano huo. Mengine yalisema kwamba Acacia/Barrick imekubali kulipa kile kilichokuwa kimetajwa kuwa wanadaiwa, au kwamba wamekiri kuhusika na kufanya udanganyifu, madai ambayo hayakuwa sehemu ya makubaliano yaliyofikiwa jana yake.

Kuanzia juu kushoto: Habari Leo, “Kampuni ya Barrick yakubali yaishe”. Amani, “Sikiliza dogo, hapa hakuna kilaza”. Majira, “Acacia yaipigia magoti serikali”. Uhuru, “Acacia yasalimu amri”. Nipashe, “Acacia kulipa”. Mwananchi, “JPM: Wametubu”.

Magazeti mengine mawili ya Kiswahili yalikuwa na mwelekeo tofauti, yakijikita kwenye suala lililotajwa kwenye sehemu ya pili ya kauli iliyotolewa na Rais Magufuli baada ya mkutano huo, ambapo alikemea mashambulizi yaliyofanywa na vyombo vya habari kwa Marais wastaafu, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete vikiwatuhumu kwa kuhusika na matatizo yanayojitokeza kwenye sekta ya madini.

“Nimesoma ripoti zote mbili hakuna mahali ambapo Mzee Mkapa na Mzee Kikwete wametajwa, vyombo vya habari viache kuwachafua hawa wazee, wamefanya kazi kubwa ya kulitumikia Taifa letu, viwaache wapumzike,” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Kuanzia kushoto: Mawio, “Zengwe”. Tanzania Daima, “Marufuku kumgusa Mkapa, Kikwete”.

Gazeti la kila wiki la Mawio, ambalo halikuheshimu kauli hiyo ya Magufuli, lilijikuta likifungiwa kwa miaka miwili na serikali kwa kuwahusisha marais wastaafu kwenye kashfa hiyo.

Magazeti matatu yanayoandikwa kwa lugha ya Kiingereza yalikuwa na mtazamo wenye tahadhari zaidi, lakini bado ni vigumu kukubaliana na hisia zilizojengwa na vichwa vya habari vya magazeti ya The Guardian na Daily News. Je, “Tumeshinda Vita”? Je, Acacia “Ilikuwa Inajificha”? Kichwa cha habari cha gazeti la The Citizen kilikuwa karibu zaidi na ukweli wa kile kilichotokea, kama ilivyokuwa kwenye habari hiyo nzima, na gazeti hilo likawa na tahariri yenye uwiano mzuri na yenye kusadifu hali halisi, iliyosema kwamba:

Sasa ambapo mazingira yametengenezwa kwa ajili ya majadiliano, maombi yetu ni kuwa pande zote zitashiriki kwenye mazungumzo hayo zikiwa na nia njema kwa maslahi ya pande zote mbili. […]

[Ni] kwa maslahi ya pande zote mbili kutafuta muafaka na kufikia mahali pa kila upande kushinda, kwa sababu tusingependa kuona hali hii ikichochea mgogoro kamili unaoweza kuwa na matokeo mabaya.

Hali hiyo inaonekana haikueleweka pia na baadhi ya wachoraji wa katuni. Nipashe na Mtanzania walikwenda nje kabisa ya suala lenyewe, Mwananchi waliweza kubaki kwenye hoja ya msingi, na Daily News walionesha hasira. Mchora katuni wa The Citizen alifanya vizuri zaidi, lakini Gado, ambaye hakuchapisha katuni yake kwenye gazeti lolote, alichukua mtazamo tofauti kabisa na wengine.

Nipashe, 15/6/17: “Yaishe”.

Mwananchi, 15/6/17: “Mnaweza kuyatumia kama mahandaki siku za vita”.

Mtanzania, 15/6/17: “Amekubali kulipa”.

Gado, 15/6/17: “Unataka kukimbia na hauna breki – unategemea nini kitatokea?”.

Daily News 15/6/17: “Wizi wa madini”

The Citizen, 15/6/17: “Tunataka hela zetu zirudi”.

Tafsiri tofauti za matokeo ya mkutano huo kati ya Magufuli na Thornton zilizochorwa na vyombo vya habari vya Tanzania zinaibua swali ikiwa waandishi na wahariri wao wanaelewa kwamba walikuwa wakiupotosha umma; na kama walijua, kwa nini walikuwa wanafanya hivyo? Je, inawezekana haya yote yametokana na sheria inayoiruhusu serikali kufungia gazeti la Mawio kirahisi? Je, inawezekana walikuwa na wasiwasi kwamba kilichotokea kwa gazeti la Mawio kingewatokea na wao pia?

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.