Miradi Ifuatayo Inalenga Kuifanya Simu yako Ikusemeshe kwa Kiswahili

Picha ya Eli Duke kupitia mtandao wa Flickr (CC BY-SA 2.0)

Kikiwa na idadi ya wazungumzaji wanaokadiriwa kufikia milioni 100 , Kiswahili ni lugha ya pili inayozungumzwa zaidi barani Afrika, baada ya Kiarabu. Pamoja na umaarufu huo, huduma za kiteknolojia kama vile mfumo wa kutambua sauti ya mzungumzaji (ASR) hazipatikani katika lugha hii. Kukosekana kwa huduma kama hizo kunawanyima watumiaji wengi wenye ulemavu na wale wasiojua kusoma na kuandika fursa ya kupata taarifa wanazozihitaji kwa ajili ya kuendesha maisha yao ya kila siku. Hali hii, hata hivyo, inaweza kubadilika hivi karibuni, kufuatia jitihada zinazofanywa na makampuni mapya ya utafiti na teknolojia kushirikiana ili kutoa teknolojia itakayowasaidia wazungumzaji wa Kiswahili.

Upatikanaji wa mtandao kwa simu ya kawaida ya kiganjani

Moja ya jitihada za kiuvumbuzi unaoleta matumaini unakaribia kuanza kutumika nchini Kenya. Uliza ni mradi unatooa huduma ya sauti inayomwezesha mtumiaji kupata taarifa kutoka kwenye mtandao wa intaneti kwa kutumia simu ya kawaida ya kiganjani.

Wanachohitaji kufanya watumiaji wake ni kupiga simu na kuuliza swali kwa lugha ya Kiswahili. Ndani ya dakika 15 hadi 90, “wakala wa kutafuta majibu” (ambaye ni mtu halisi anayefanya kazi nyuma ya pazia) atakuwa amepata jibu na kumpigia simu mwuulizaji. Mpaka sasa, “kundi” la mawakala wapatao 50 linafanya kazi ya kusikiliza na kushughulikia matatizo ya watumiaji kwa kurekodi sauti, kutafuta majibu mtandaoni kwa lugha mbalimbali, kutafsiri taarifa na kuzituma kwa muhitaji kwa mfumo wa sauti inayosikika kwa Kiswahili.

Wakati wa majaribio ya mradi yaliyofanyika kwenye mji mkuu wa Kenya, Nairobi, na Magharibi mwa Kenya, watumiaji wapatao 600 walituma maswali yao kuhusu masuala kama wawakilishi wa maeneo yao, kuomba msaada kwa ajili ya kufanya kazi za kimasomo, na kuomba taarifa nyeti za kitabibu ambazo inawezekana isingekuwa rahisi kumwuuliza mtu ana kwa ana.

Wakati wa majaribio ya mradi wa Uliza, haya ndio maneno yaliyotumika kwenye maswali mengi yaliyoulizwa na watumiaji.

Uliza itatatua tatizo jingine kwa watumiaji wake wa baadae: kukosekana kwa taarifa zinazohifadhiwa kwenye mtandao wa Intaneti. Kuna sababu nyingi zinazoweza kuelezea hali hii: gharama kubwa ya vifurushi ya data kwa ajili ya simu za kiganjani, umbali kwenda kwenye mgahawa wa kuuza intaneti, kutokujua lugha zinazotumika zaidi kwa mawasiliano, ikiwamo kukosekana au kupungua kwa maudhui katika lugha zinazotumiwa na wenyeji.

Si tatizo la kiteknolojia

Mradi wa Uliza unawafikia walengwa kwa utaratibu unaohitaji wafanyakazi wengi lakini ina faida moja kubwa: kuwa na watu wanaoweza kufanyia kazi mahitaji ya watu kwa kuyageuza kuwa sauti na kuyatafsiri, na hivyo kutatua tatizo la kukosekana kwa hifadhi za kutosha za sauti hali ambayo ndicho kikwazo cha jitihada za kutengeneza mfumo wa kutambua sauti ya mzungumzaji (ASR) kwa lugha za Afrika. Kadhalika, utendaji kazi wa mradi wa Uliza unasaidia kukusanya takwimu kutoka kwa wazungumzaji halisi wenye lafudhi na lahaja tofauti. Mwanzilishi wa mradi wa Uliza Grant Bridgman anapanga kutumia hifadhi ya sauti hizo kutengeneza mashine ya kujenga uwezo wa kujifunzia na hata mfumo wa kutambua sauti ya mzungumzaji katika siku za usoni. Katika mazungumzo yake kwenye chuo kikuu cha Tufts, Bridgman alielezea wazo hili ambalo ndilo msingi wa mradi huo:

Kwa kiwango kikubwa utafiti umeshafanywa kuwezesha kutengenezwa kwa mfumo wa kutambua sauti ya mzungumzaji kwa lugha ya Kiswahili na lugha nyinginezo zinazozungumzwa zaidi Afrika, lakini bado itachukua muda kwa teknolojia hiyo kuanza kutumiwa na watu wanaoihitaji. Katika mahojiano na Global Voices, Bridgman alieleza:

Teknolojia ipo na hayo yote yanapatikana tayari kwa lugha kubwa zinazozungumzwa duniani. Kwa sasa tunahitaji kupata mfumo utakaowezeshwa kibiashara kufanya teknolojia hiyo ipatikane kwa lugha zenye rasliali chache.

Makampuni ya kiteknolojia yanaangalia uwezekano wa kutengeneza “laini” za simu kwa ajili ya kuwafikia wateja wa vijijini kwa gharama nafuu katika hatua za awali za ukuaji wa mradi wa Uliza. Hatimaye, huduma kamili inayowaruhusu watumiaji wa simu za kiganjani kupata majibu ya maswali yao na kutuma sauti zao bila kulazimika kuunganishwa na mtandao wa intaneti itatekelezwa. Gharama kwa mtumiaji zinakuwa za chini kabisa -karibia na bei ya kawaida ya kutuma arafa (ujumbe mfupi wa maandishi).

Mfumo wa utendaji wa mradi wa Uliza unaweza kutumika kwa ajili ya lugha nyinginezo zenye idadi ya kutosha ya wazungumzaji. Lakini kwa lugha nyingi zizungumzwazo barani Afrika zipatazo 2,000 hatua hii bado haiwezekani. Hata hivyo, ufumbuzi unaweza kuletwa na mradi wa utafiti unaoongozwa na Preethi Jyothi wa Taasisi ya Beckman, ambako timu ya watafiti waliweza kutumia utaratibu wa nakisi kutafuta sauti za maneno yanayozungumzwa zaidi na wazungumzaji wa lugha ya kujifunza. Utakapokamilishwa, utengenezaji wa sauti kwa njia ya nakisi unaweza kufungua uwezekano wa mfumo wa utambuzi wa sauti ya mzungumzaji (ASRP) kwa lugha zisizo na wazungumzaji wengi, bila sahaka kwa gharama nafuu.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.