Katika Kutafuta Haki, Mtumishi Huyu wa Kanisa Katoliki Ameandika Nyaraka Kuhusu Mauaji na Dawa za Kulevya Nchini Ufilipino

Wahanga wengi wa tokhang (operesheni ya kukomesha dawa za kulevya) ni wakazi maskini wa mijini. Picha na Ciriaco Santiago, imetumika kwa ruhusa.

Ciriaco Santiago anaweza kuonekana kama Mmisionari wa kawaida katika kanisa la Baclaran mjini Manila lakini pia ni mpiga picha wa usiku ambaye huungana na waandishi wengine wa habari wanaoandika kuhusu operesheni hatari ya kudhibiti dawa za kulevya inayofanywa na polisi wa Ufilipino.

Kwa mujibu wa kumbukumbu za polisi, zaidi ya watu 2,000 wameuawa katika operesheni ya kukomesha dawa za kulevya kuanzia Juni mpaka Disemba 2016. Ila baadhi ya makundi yanaamini kuwa idadi inaweza kuongezeka kama mauaji yatokanayo na matumizi ya nguvu kubwa kinyume na sheria yatajumuishwa.

Kama kazi ya vyombo vya habari itakuwa ni kuripoti majeruhi wapya katika vita ya serikali dhidi ya dawa za kulevya, majukumu ya Santiago ni kupiga picha na kuweka kumbukumbu za wahanga wa operesheni dhidi ya dawa za kulevya autokhang na mauaji ya yanayofanyika kutokana na kutumia nguvu nyingi kinyume na sheria ili zitumike hapo baadaye katika upelelezi wa uvunjaji wa Haki za Binadamu.

Katika mahojiano na Vatican Insider, Santiago alielezea ni kwa nini ni muhimu kufichua ukatili unaofanyika katika vita dhidi ya dawa za kulevya:

Kuufanya ulimwengu ufahamu kuhusu unyama huu uliohalalishwa ni kazi ya Kibinadamu kabla haijawa habari. Kukuza uelewa wa jamii kuhusu ukiukwaji wa sheria ulio wazi na halali na kukomesha mauaji. Uandishi wa habari unaweza kuyatumikia matakwa ya umma na kufanya kazi kwa maslahi mema.

Kazi za Santiago zimewahi kutumika kwenye maonesho kadhaa katika makanisa na shule. Mtandao wa Haki za Binadamu wa The Rise-Up (Inuka) pia ulikabidhi picha zake kama ushahidi unaowahusisha polisi na mauaji yatokanayo na matumizi makubwa ya nguvu yakiwalenga watu maskini wa maeneo ya mjini katika jiji la Manila, ambao ni mji mkuu wa Ufilipino.

Vita dhidi ya dawa za kulevya ilikuwa jambo la kitaifa mwaka 2016 pale Rais mpya mteule alipoapa kulimaliza janga hilo kwa kuwaua viongozi wa vikundi vya wafanyabiashara za dawa hizo na wanaowalinda.

Kuna mifano mingi ya wananchi wasio na hatia kuuawa kwenye operesheni za tokhang . Polisi wanatuhumiwa kwa mauaji ya washukiwa wasio na silaha na watu wengine wadogo wadogo wanaojihusisha na dawa za kulevya, lakini mamlaka imelaumu na kuvihusisha vikundi vya wauzaji wa dawa za kulevya kuwa vinasafisha makundi pinzani katika biashara hiyo.

Bruda Ciriaco Santiago wa Kanisa Katoliki la Redemptorist. Chanzo: Facebook

Santiago, ambaye ni msimamizi wa masuala ya migogoro kanisani kwake, alianza kuandika kazi yake Disemba 2016 ikiwa ni mwitikio wa ongezeko la kesi na malalamiko yaliyowahusisha waumini masikini wa mjini.

Wakati akitembelea moja ya jumuiya za watu maskini, Santiago aligundua kuhusu kisa cha matineja waliouawa na wanaume waliokuwa wameficha sura zao. Viongozi wa jamii hiyo walishuhudia kuwa vijana hao hawakuwa wakijihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya. Wengi wanaamini kuwa mauaji hayo yanaweza kuwa ni ya operesheni ya tokhang .

Santiago aliandika kuhusu habari ya vijana hao wadogo na akaandika waraka kwa maandamano wakati wa mazishi:

Walikuwa na ndoto. Kila mmoja wao alitaka kumaliza masomo yao, wakiamini wangepata kazi nzuri wakishamaliza mafunzo yao rasmi.

Kwa sababu ya umasikini, ilibidi wafanye kazi na kuweka akiba. Walikuwa na msimamo kuhusu kumaliza kusoma, bila kujali itachukua muda mrefu kiasi gani.

Lakini ndoto ile pamoja na mazingira ya amani ya kijiji hiki vilitoweka usiku wa tukio lile.

Tukio lilikuwa la muda mfupi. Familia za wahanga na ndugu zao hawawezi kumudu maziko ya heshima kwa wafu wao. Uamuzi wao ukawa ni kuwazika katika kaburi la pamoja – kila mwili pembeni ya mwingine.

Matineja waliouawa katika operesheni inayofanana na tokhang walizikwa katika kaburi la pamoja kila mmoja pembeni ya mwenzake kwa ajili ya kuokoa gharama. Viongozi wa jamii walishuhudia vijana hao kutokuwa na hatia. Picha na Ciriaco Santiago, imetumika kwa ruhusa.

Kazi ya Santiago inawiana na ripoti za mwandishi wa habari nguli zilizotoa mwelekeo kwa wahanga wa tokhang na hatari ya madhara ya vita hii ya madawa ya kulevya katika maeneo ya miji ya jamii masikini.

Santiago anawatia moyo wapiga picha vijana kumwaga nuru katika hali za watu masikini hasa wale waliohathiriwa na vita ya serikali dhidi ya dawa za kulevya:

Kama mwandishi wa habari picha, mara zote kuwa na masikini na elewa ukweli wa jamii yao. Mara zote kuna mgongano wa maslahi ya matabaka, katika hilo kuwa upande wa wale wanaoonewa na upande wa watu masikini.

Hapo chini ni baadhi ya picha zilizopigwa na Santiago, zikionesha tokhang ina maana gani kwa wa-Filipino wa kawaida katika vijiji vya watu masikini:

Maafisa wa polisi wakiangalia maiti ya mtu anayedhaniwa kuwa mtuhumiwa wa dawa za kulevya. Karibu na mwili huo ni lori lenye bango la matangazo na jina la Rais wa nchi. Picha na Ciriaco Santiago, imetumika kwa ruhusa.

Mwili wa mhanga wa tokhang ukipitishwa mbele ya familia inayoomboleza. Picha na Ciriaco Santiago, imetumika kwa ruhusa.

Sekta ya dini imekuwa ikiwafikia wahanga wa tokhang ili kuchunguza na kukomesha mauaji yanayohusishwa na dawa za kulevya nchini. Picha na Ciriaco Santiago, imetumika kwa ruhusa.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.